Serikali kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Habari, Zamaradi
Kawawa ,imejibu madai yalitolewa jana na Mwanasheria Mkuu wa Chadema,
Tundu Lissu kuwa ndege ya Tanzania, Bombadier kuwa imeshikiliwa nchini
Canada kutokana na serikali kudaiwa.
Soma taarifa kamili:
Mnamo tarehe 18 Agosti, 2017 siku ya Ijumaa, kuna taarifa zimetolewa
kwenye vyombo vya habari kwamba kuna mgogoro wa utekelezaji wa ununuzi
wa Ndege ya tatu inayonunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kutoka kampuni ya Bombadier ya Nchini Canada.
Taarifa hiyo iliendelea kudai kwamba kuna wanasheria wa Kampuni
fulani ya Nchini Italia, walioweka zuio la ununuzi wa Ndege hiyo kwa
maelezo kwamba, wanakamata mali hiyo ya Serikali kwa kuwa kuna Kampuni
inayodai Serikali ya Tanzania.
Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa
Serikali inapenda kuufahamisha Umma kuwa mgogoro huo upo ila kimsingi ni
mgogoro ambao umetengenezwa na Watanzania wenzetu ambao kwa bahati
mbaya sana wameweka maslahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya
maslahi ya Taifa.
Mambo Muhimu ambayo Umma Ufahamu
Ndege zinazonunuliwa ikiwepo hii ambayo imetengenezewa Mgizengwe na
hao Watanzania wenzetu sio ya Rais Magufuli bali ni za watanzania wote.
Hawa baadhi ya viongozi wa kiasiasa wanaoshabikia migogoro inayokumba
jitihada za Rais wetu, za kutuletea maendeleo, hawana Uzalendo.
Serikali imesikitishwa sana tena sana kwa hujuma zinazofanywa
waziwazi tena kwa ushabiki wa hali ya juu na baadhi ya viongozi wa
kisiasa wa chama hicho, kupingana na mwelekeo mzuri wa Mhe. Rais
kutuletea maendeleo
Kwa mtu yeyote mwenye uchungu na Nchi yake,angepambana ili jambo
linalohusu maslahi ya Taifa, likiwepo la kununua Ndege, lisikwame na
kama kuna mkwamo basi ashilirki kukwamua badala ya kushabikia.
Serikali pia ina fununu kwamba watu hawahawa wanaohujumu jitihada za
kimaendeleo, pia wanahujumu hata hali ya usalama wa raia wetu kwenye
baadhi ya maeneo ya Nchi yetu. Hili nalo linaendelea kufanyiwa kazi kwa
kina.Wanaopinga mambo ya Maendeleo hawapingani na Mhe. Magufuli bali
wanapingana na Watanzania wote kwa ujumla.
Hivyo basi ni vyema Watanzania mkaelewa ukweli wa hali halisi na
mkapuuzia mambo ambayo yanashabikiwa na baadhi ya viongozi hao wa
kisiasa wanaotafuta umaarufu rahisi (Cheap Popularity). Endeleeni
kumuombea Rais wetu na Tanzania kwa Ujumla kwani Chini ya Uongozi wake,
amedhamiria kwamba hakuna kurudi nyuma (no reverse gear).
Serikali ilikuwa inawahisi baadhi ya wanasiasa kuhusika na hujuma hizi
na sasa sio hisia tena bali baadhi yao wameshaanza kujitokeza hadharani.
Hatua za Kuchukuliwa/Zianzochukuliwa:
Kuhusiana na Mgogoro kwenye ununuzi wa Ndege, hatua za Kidiplomasia na
za kisheria zimeanza kuchukuliwa ili kumaliza jambo hili. Aidha kwa wale
wanaoshabikia na kutengneza migogoro na hujuma mbalimbali dhidi ya
maendeleo ya Nchi yetu, Serikali itaendelea na taratibu za kiuchunguzi
na haitasita kuchukua hatua za kisheria zinazostahili.
Serikali inatumia pia fursa hii kuwaomba Watanzania wasiwe na
wasiwasi wala tashwishi kuhusu mpango wa Ndege kununuliwa na kwamba
waendelee kuiamini Serikali yao iliyopo madarakani inayoongozwa na Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli. Uzalendo wetu uwe ndio mtaji mkubwa kuliko
siasa, dini au ukabila.
Serikali ilikuwa na fununu kwamba kuna viongozi wa baadhi ya Vyama
vya Siasa ambao kwa namna moja au nyingine wangependa kuhujumu jitihada
za Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kuwaletea
Watanzania (hasa wanyonge) maendeleo.
Wanasheria hao waliokwenda kufungua madai kwamba Serikali yetu
inadaiwa na kwamba Ndege hiyo ishikiliwe, hawana uhalali wowote wa
kufanya hivyo na ni matapeli tu ambao wamesukumwa na baadhi ya viongozi
wa kisiasa wasioitakia mema Nchi yetu.
Kwa kuwa Serkali ilishapata fununu kwamba kuna baadhi ya viongozi wa
chama cha siasa wana mpango huo, sasa watu hao wamejidhihirisha
hadharani kwamba wao ndio wako nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za
Serikali ya Awamu ya Tano kwa maslahi yao ya kisiasa.
Serikali ya awamu ya Tano Inawahakikishiwa Watanzania kwamba Ndege
itakuja. Wanaokwamisha jitihada za Serikali za kuleta ndege watapanda na
ndugu zao watapanda na wafuasi wao watapanda .
Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe
Magufuli haibagui watanzania kwa itikadi za Kisiasa, Dini, Kabila, rangi
au utofauti wowote.
Kundi hilo la baadhi ya Viongozi wa siasa walishatoa maelezo ya
kuvuruga au kukejeli jitihada za Serikali. Mambo ambayo wanasiasa hao
walishayakingia kifua ni pamoja na;
Kushawishi wafadhili wasilete misaada tena Tanzania.Watu hawahawa
walishawahi kuomba kwamba Washirika wetu wa Maendeleo wasilete tena
misaada Tanzania.
Tunachojiuliza kama Serikali, hivi misaada isipoletwa anayekomolewa
ni Rais Magufuli? Au ni Watanzania wanyonge ambao wangekosa madawa,
Huduma za Maji, Umeme, n.k.
Jambo la kutia faraja ni kwamba pamoja na jitihada za hali ya juu za
watu hao, Washirika wa Maendeleo sasa wameongeza kasi ya ushirikiano na
Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Mifano ya wazi
ya hivi Karibuni ni tamko la Serikali ya Marekani kupitia Balozi wake
kwamba Marekani itaogeza kiasi cha Misaada Tanzania, Ziara ya Tajiri
Masuhuri Duniani Bill Gate ambaye pia ameonyesha kuguswa na kasi ya
uongozi wa Mhe. Magufuli na kuahidi kutoa fedha zaidi, Ujio wa Viongozi
wakuu wa Nchi 15 ndani ya muda ambao Mhe. Magufuli amekuwa Madarakani na
mambo mengine mengi.
Kubeza Juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli; Imekuwa ni hulka
ya hao baadhi ya viongozi wa siasa kufanya kila jitihada za kubeza
jitihada za dhati ambazo Mhe. Rais anafanya kuwaletea Wananchi Maendeleo
tena hata bila kujali kwamba eneo husika linaongozwa na Kiongozi wa
Chama gani. Hata tukio ka Kihistoria lililofanyika hivi karibuni Jijini
Tanga, la kuweka jiwela msingi Ujenzi wa Bomba la Mafuta, Mhe. Rais
alionyesha dhahiri kutobagua hata maeneo yale ambayo hayaongozwi na CCM.
Tulitegemea huu uzalendo wa Mhe. Rais Ungeungwa mkono na watanzania
wote.
Kubeza jitihada za Kunusuru madini yetu na Maliasili. Mhe. Rais
Magufuli anafanya jitihada za dhati kabisa kunusuru mali asili zetu na
ndio maana akasimamia kwa uadilifu, uaminifu na uwajibikaji suala zima
la Makinikia. Hii ilimfanya hata Rais wa Kampuni ya Barick kukodisha
Ndege kuja kumuona Mhe. Rais, na tunaamini jitihada hizi zitazaa
matunda. Lakini baadhi ya viongozi haohao wa siasa wamekuwa mstari wa
Mbele kupingana na jitihada hizi kwamba tutashitakiwa kwa hiyo bora
tuache makinikia yapelekwe tukiendelea na majadiliano.
IMETOLEWA NA
Idara ya Habari (MAELEZO)
19/08/2017.