Serikali imetangaza usitishaji wa usajili wa mashirika yasiyo ya
kiserikali (NGO’s) kuanzia Agosti 21 hadi Novemba 30, mwaka huu ili
kufanya uhakiki wa NGO’s zilizosajiliwa.
\
Hatua hiyo imetangazwa jana na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii,
Sihaba Nkinga, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.
“Napenda pia kuujulisha umma kuwa kuanzia Agosti 21, 2017
hadi Novemba 30, 2017 usajili wa NGO’S mpya utasimamishwa, ili kutoa
fursa kwa wataalamu kuchakata taarifa kutoka kwenye vituo vingine
kuhakiki NGO’s zilizosajiliwa,”amesema Nkinga.
Bw. Nkinga amesema baada ya uhakiki huo unaotarajia kufanyika nchi
nzima kukamilika, NGO’s zote ambazo hazitakuwa zimefanyiwa uhakiki
zitafutwa kwenye Rejista na hazitaruhusiwa kuendesha shughuli zao
nchini.
“Wakati tunaendelea na zoezi la uhakiki tutafanya tathmini ya
mwenendo wa uhakiki katika kanda zote nchini na hatimaye kutoa uamuzi
stahiki, ili kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanikiwa na wadau wetu
wanahudumiwa kwa ufanisi mkubwa,”amesema Nkinga huku akiwakumbusha wahusika wa NGO’s kuwasilisha vyeti vyao vya usajili mapema kwa njia ya mtandao.
“Niwakumbushe pia, kuwa ni vema kuzingatia kuwa wakati wa
uhakiki kila NGO’s inatakiwa kuwasilisha cheti halisi cha usajili na
nakala ya cheti hicho, NGO-Fomu/UHK/2017 iliyojazwa vizuri. Fomu hii
inapatikana katika tovuti ya uratibu wa NGOs kwa anuani ya
www.tnnc.go.tz, stakabadhi za malipo ya ada ya mwaka au hati ya malipo
benki toka kusajiliwa kwa shirika, Barua kutoka kwa ofisa maendeleo ya
jamii (Mkoa/ wilaya/halmashauri au Manispaa) ikithibitisha uwapo wa
ofisi ya shirika na nakala ya katiba ya NGO iliyothibitishwa na msajili
wa NGOs,” amesema Nkinga.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika yasiyo ya
Kiserikali nchini Tanzania, Nicholaus Zacharia, amewatoa hofu wamiliki
wa mashirika hayo na kuwataka kila mmoja kushiriki katika uhakiki huo.
“Sisi kama viongozi wenu tumejilidhisha serikali haina mpango
wowote mbaya na Azaki zetu, hivyo mtu atakayekwambia usishiriki katika
uhakiki anakutakia uende jehanamu,”amesema Zacharia.
Hata hivyo, Zacharia ameiomba serikali kuona ni jinsi gani inaweza
kuanzisha bodi itakayokuwa inasimamia mashirika hayo tofauti na baraza
hilo ambalo limekuwa likidumu kwa miaka mitatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni