Jumamosi, 19 Agosti 2017

Serikali yamjibu Lissu kuhusu ujio wa Bombadier

Serikali kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa ,imejibu madai yalitolewa jana na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kuwa ndege ya Tanzania, Bombadier kuwa imeshikiliwa nchini Canada kutokana na serikali kudaiwa.





Soma taarifa kamili:
Mnamo tarehe 18 Agosti, 2017 siku ya Ijumaa, kuna taarifa zimetolewa kwenye vyombo vya habari kwamba kuna mgogoro wa utekelezaji wa ununuzi wa Ndege ya tatu inayonunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kampuni ya Bombadier ya Nchini Canada.
Taarifa hiyo iliendelea kudai kwamba kuna wanasheria wa Kampuni fulani ya Nchini Italia, walioweka zuio la ununuzi wa Ndege hiyo kwa maelezo kwamba, wanakamata mali hiyo ya Serikali kwa kuwa kuna Kampuni inayodai Serikali ya Tanzania.
Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali inapenda kuufahamisha Umma kuwa mgogoro huo upo ila kimsingi ni mgogoro ambao umetengenezwa na Watanzania wenzetu ambao kwa bahati mbaya sana wameweka maslahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya maslahi ya Taifa.
Mambo Muhimu ambayo Umma Ufahamu
Ndege zinazonunuliwa ikiwepo hii ambayo imetengenezewa Mgizengwe na hao Watanzania wenzetu sio ya Rais Magufuli bali ni za watanzania wote.
Hawa baadhi ya viongozi wa kiasiasa wanaoshabikia migogoro inayokumba jitihada za Rais wetu, za kutuletea maendeleo, hawana Uzalendo.
Serikali imesikitishwa sana tena sana kwa hujuma zinazofanywa waziwazi tena kwa ushabiki wa hali ya juu na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa chama hicho, kupingana na mwelekeo mzuri wa Mhe. Rais kutuletea maendeleo
Kwa mtu yeyote mwenye uchungu na Nchi yake,angepambana ili jambo linalohusu maslahi ya Taifa, likiwepo la kununua Ndege, lisikwame na kama kuna mkwamo basi ashilirki kukwamua badala ya kushabikia.
Serikali pia ina fununu kwamba watu hawahawa wanaohujumu jitihada za kimaendeleo, pia wanahujumu hata hali ya usalama wa raia wetu kwenye baadhi ya maeneo ya Nchi yetu. Hili nalo linaendelea kufanyiwa kazi kwa kina.Wanaopinga mambo ya Maendeleo hawapingani na Mhe. Magufuli bali wanapingana na Watanzania wote kwa ujumla.
Hivyo basi ni vyema Watanzania mkaelewa ukweli wa hali halisi na mkapuuzia mambo ambayo yanashabikiwa na baadhi ya viongozi hao wa kisiasa wanaotafuta umaarufu rahisi (Cheap Popularity). Endeleeni kumuombea Rais wetu na Tanzania kwa Ujumla kwani Chini ya Uongozi wake, amedhamiria kwamba hakuna kurudi nyuma (no reverse gear).
Serikali ilikuwa inawahisi baadhi ya wanasiasa kuhusika na hujuma hizi na sasa sio hisia tena bali baadhi yao wameshaanza kujitokeza hadharani.
Hatua za Kuchukuliwa/Zianzochukuliwa:
Kuhusiana na Mgogoro kwenye ununuzi wa Ndege, hatua za Kidiplomasia na za kisheria zimeanza kuchukuliwa ili kumaliza jambo hili. Aidha kwa wale wanaoshabikia na kutengneza migogoro na hujuma mbalimbali dhidi ya maendeleo ya Nchi yetu, Serikali itaendelea na taratibu za kiuchunguzi na haitasita kuchukua hatua za kisheria zinazostahili.
Serikali inatumia pia fursa hii kuwaomba Watanzania wasiwe na wasiwasi wala tashwishi kuhusu mpango wa Ndege kununuliwa na kwamba waendelee kuiamini Serikali yao iliyopo madarakani inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Uzalendo wetu uwe ndio mtaji mkubwa kuliko siasa, dini au ukabila.
Serikali ilikuwa na fununu kwamba kuna viongozi wa baadhi ya Vyama vya Siasa ambao kwa namna moja au nyingine wangependa kuhujumu jitihada za Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kuwaletea Watanzania (hasa wanyonge) maendeleo.
Wanasheria hao waliokwenda kufungua madai kwamba Serikali yetu inadaiwa na kwamba Ndege hiyo ishikiliwe, hawana uhalali wowote wa kufanya hivyo na ni matapeli tu ambao wamesukumwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wasioitakia mema Nchi yetu.
Kwa kuwa Serkali ilishapata fununu kwamba kuna baadhi ya viongozi wa chama cha siasa wana mpango huo, sasa watu hao wamejidhihirisha hadharani kwamba wao ndio wako nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa maslahi yao ya kisiasa.
Serikali ya awamu ya Tano Inawahakikishiwa Watanzania kwamba Ndege itakuja. Wanaokwamisha jitihada za Serikali za kuleta ndege watapanda na ndugu zao watapanda na wafuasi wao watapanda .
Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli haibagui watanzania kwa itikadi za Kisiasa, Dini, Kabila, rangi au utofauti wowote.
Kundi hilo la baadhi ya Viongozi wa siasa walishatoa maelezo ya kuvuruga au kukejeli jitihada za Serikali. Mambo ambayo wanasiasa hao walishayakingia kifua ni pamoja na;
Kushawishi wafadhili wasilete misaada tena Tanzania.Watu hawahawa walishawahi kuomba kwamba Washirika wetu wa Maendeleo wasilete tena misaada Tanzania.
Tunachojiuliza kama Serikali, hivi misaada isipoletwa anayekomolewa ni Rais Magufuli? Au ni Watanzania wanyonge ambao wangekosa madawa, Huduma za Maji, Umeme, n.k.
Jambo la kutia faraja ni kwamba pamoja na jitihada za hali ya juu za watu hao, Washirika wa Maendeleo sasa wameongeza kasi ya ushirikiano na Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Mifano ya wazi ya hivi Karibuni ni tamko la Serikali ya Marekani kupitia Balozi wake kwamba Marekani itaogeza kiasi cha Misaada Tanzania, Ziara ya Tajiri Masuhuri Duniani Bill Gate ambaye pia ameonyesha kuguswa na kasi ya uongozi wa Mhe. Magufuli na kuahidi kutoa fedha zaidi, Ujio wa Viongozi wakuu wa Nchi 15 ndani ya muda ambao Mhe. Magufuli amekuwa Madarakani na mambo mengine mengi.
Kubeza Juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli; Imekuwa ni hulka ya hao baadhi ya viongozi wa siasa kufanya kila jitihada za kubeza jitihada za dhati ambazo Mhe. Rais anafanya kuwaletea Wananchi Maendeleo tena hata bila kujali kwamba eneo husika linaongozwa na Kiongozi wa Chama gani. Hata tukio ka Kihistoria lililofanyika hivi karibuni Jijini Tanga, la kuweka jiwela msingi Ujenzi wa Bomba la Mafuta, Mhe. Rais alionyesha dhahiri kutobagua hata maeneo yale ambayo hayaongozwi na CCM. Tulitegemea huu uzalendo wa Mhe. Rais Ungeungwa mkono na watanzania wote.
Kubeza jitihada za Kunusuru madini yetu na Maliasili. Mhe. Rais Magufuli anafanya jitihada za dhati kabisa kunusuru mali asili zetu na ndio maana akasimamia kwa uadilifu, uaminifu na uwajibikaji suala zima la Makinikia. Hii ilimfanya hata Rais wa Kampuni ya Barick kukodisha Ndege kuja kumuona Mhe. Rais, na tunaamini jitihada hizi zitazaa matunda. Lakini baadhi ya viongozi haohao wa siasa wamekuwa mstari wa Mbele kupingana na jitihada hizi kwamba tutashitakiwa kwa hiyo bora tuache makinikia yapelekwe tukiendelea na majadiliano.
IMETOLEWA NA
Idara ya Habari (MAELEZO)
19/08/2017.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni