Alhamisi, 24 Agosti 2017

Hiki ndicho chanzo cha ugonjwa wa Bulaya





 Dar es Salaam. Wakati Mbunge wa Bunda Ester Bulaya akitarajia kufanyiwa kipimo cha CT Scan katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), chanzo cha ugonjwa unamsumbua kimetajwa.

Bulaya ambaye alipata tatizo la kupumua baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi mjini Tarime, alifikishwa hospitalini hapo juzi usiku na kulazwa katika wodi namba 18, Sewahaji.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mbunge wa Kawe Halima Mdee alisema chanzo cha Bulaya kuugua ghafla ni athari aliyoipata baada ya kukamatwa na polisi.

“Walipomkamata walimpakia kwenye gari na kupita katika barabara yenye vumbi jingi wakati wakielekea Tarime na yeye ana matatizo ya kifua na hata selo waliyomuweka haikuwa rafiki,” alisema Mdee.

Hata hivyo, alifafanua kuwa baada ya kuzidiwa ilichukua muda mrefu kufikishwa hospitalini.

Alisema baada ya kuonekana anahitaji huduma ya dharura na rufaa hakupewa nafasi hiyo kwa wakati.

“Hali ilikuwa mbaya na kama angeendelea kubaki kule tulikuwa tunampoteza, tunashukuru madaktari wamempokea vizuri na leo (jana) amekuja mtaalamu wa kifua, amemhudumia vizuri,” alisema Mdee.

Lowassa amtembelea wodini

Kwa siku ya jana wabunge mbalimbali walikuwa wakimtembelea mbunge huyo kiasi cha ulinzi kuimarishwa huku baadhi ya wafuasi wa Chadema wakizuiliwa kuingia katika wodi aliyolazwa mbunge huyo.

Lakini, alipofika aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais wa mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa aliingia wodini na kuonana na mbunge huyo ambaye kwa siku ya jana afya yake ilikuwa imeimarika.

Hata hivyo, Lowassa aliyetumia dakika 20 kusalimiana na mbunge huyo, alimpa pole na baadaye aliondoka na hakutaka kuzungumza chochote.

Akizungumza kwa tabu, Bulaya alisema, “Nashukuru Mungu sasa afya yangu imeimarika, ninaendelea vizuri.”

Baba wa mbunge huyo, Paul Bulaya alisema mwanaye ameonekana na matatizo ya nyama za pua hivyo anasubiri matibabu hayo pia.

“Tangu amekuja mpaka sasa hivi hali yake inaendelea vizuri, amefanyiwa vipimo mbalimbali vya kifua na maeneo ambayo madaktari wanahitaji uchunguzi kinachosubiriwa sasa ni kipimo cha CT Scan,” alisema Mzee Bulaya.

Akizungumzia hali ya mbunge huyo, Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Stephen alisema Bulaya amepata ahueni kiafya na anaendelea vizuri na matibabu.

“Sasa ameanza kujihudumia mwenyewe, anakula vizuri na bado anaendelea na matibabu,” alisema Stephen huku akisisitiza kuwa mgonjwa bado anahitaji utulivu kwa kipindi hiki.

Bulaya alisota rumande tangu akamatwe Ijumaa ya Agosti 18 kwa madai ya kuingia Jimbo la Tarime na kufanya shughuli za kisiasa pamoja na kutoa msaada wa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule za msingi.

Mbunge huyo alikwenda jimboni humo baada ya kualikwa na mbunge mwenzake Ester Matiko.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni