MZIMBABWE Donald Dombo Ngoma leo ameinusuru timu yake, Yanga SC
kupoteza mechi mbele ya Maji Maji baada ya kuifungia bao la kusawazisha
kipindi cha pili, timu hizo zikitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Maji Maji
mjini Songea katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ngoma alifunga bao la kusawazisha dakika ya 79 kwa kichwa akimalizia
krosi ya Mzambia, Obrey Chirwa kumtungua kipa wa zamani wa Simba, Andrew
Ntalla.
Hiyo ilifuatia Maji Maji kutangulia kwa bao la Peter Mapunda dakika ya
54 akimalizia pasi ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Jerson John
Tegete kumtungua kipa Mcameroon Youthe Rostand.
Kipindi cha kwanza wenyeji Maji Maji walitawala mchezo na kufika mara
nyingi kwenye eneo la hatari la Yanga, lakini hawakuweza tu kufunga
kutokana na utulivu wa safu ya ulinzi ya mabingwa hao watetezi chini ya
beki mkongwe, Kevin Yondan.
Sifa zaidi zimuendee kipa Mcameroon, Rostand aliyeokoa michomo mingi ya
hatari likiwemo shuti la mpira wa adhabu la Mapunda kutoka upande wa
kushoto ambalo alilipangua pembezoni mwa lango juu na kuwa kona ambayo
haikuzaa matunda.
Yanga walicheza kwa kasi nzuri ya kushambulia kwa dakika 10 tu za
mwanzo, baada ya hapo wakalizimika kucheza kwa kuwadhibiti zaidi wenyeji
walioanza kutawala mchezo.
Lakini dakika tano kuelekea mapumziko, Yanga nao wakaanza kuwasukuma
langoni mwao Maji Maji ambao nao walisimama imara kuondoa hatari zote
upande wao.
Kipindi cha pili, Maji Maji walikianza vizuri baada ya mabadiliko
yaliyofanywa na kocha Habib Kondo akiwaingiza wakongwe, kiungo wa zamani
wa Simba, Abdulhalim Humud na mshambuliaji Tegete kuchukua nafasi za
Yakubu Kibiga na Danny Mrwanda.
Maji Maji ikaenda kuuteka kabisa mchezo katika safu ya kiungo na kuanza
kuwashambulia Yanga mfululizo kabla ya kupata bao la kuongoza. Baada ya
kufungwa, Yanga wakaamua kutoka kwenda kushambulia hadi kufanikiwa
kupata bao la kusawazisha.
Na baada ya Yanga kusawazisha timu hizo zilianza kushabuliana kwa zamu,
huku zikicheza kwa tahadhari zaidi. Winga wa Yanga, Emmanuel Martin
aliumia na kukimbizwa hospitali dakika ya 85 baada ya kugongana na
mchezaji wa Maji Maji, Marcel Kaheza.
Kwa matokeo hayo, Yanga inafikisha pointi tano baada ya kucheza mechi
tatu, ikitoa sare mbili na kushinda moja, lakini Maji Maji inafikisha
pointi mbili baada ya kufungwa mechi moja na sare mbili.
Kikosi cha Maji Maji kilikuwa; Andrew Ntala, Juma Salamba, Mpoki
Mwakinyuke, Kennedy Kipepe, Tumba Sued, Hassan Hamisi, Suleiman Kassim
‘Selembe’, Yakubu Kibiga/Abdulhalim Humud dk46, Danny Mrwanda/Jerry
Tegete dk46, Marcel Kaheza na Peter Mapunda.
Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassan Kessy dk65, Gardiel Michael,
Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey
Chirwa, Raphael Daudi, Donald Ngoma, Ibrahim Hajib na Geoffrey
Mwashiuya/Eammnuel Martin dk75/Said Juma ‘Makapu’ dk85.