Inawezekana wewe ni moja kati ya ambao wamewahi kukosa usingizi
wakati wa usiku. Hii huwa ni hali ambayo mara nyingi inasumbua na kukera
hususani kama mtu umechoka.
Hata hivyo wataalamu wanashauri kufanya vitu vifuatavyo ili
kutengeneza mazingira mazuri ya kulala na kuepukana na tatizo la kukosa
usingizi
1.Fanya mazoezi wakati wa mchana
Inashauriwa kuwa pindi ukigundua unapata wakati mgumu kulala wakati
wa usiku mara kwa mara, tengeneza utaratibu wa kufanya mazoezi nyakati
za mchana. Kwa kufanya hivi mwili na akili huandaliwa kwa ajili ya
kupata usingizi wakati wa usiku.
2. Kuwa na muda binafsi na tafakari ilivyokuwa siku yako.
Kabla ya kulala pia inashauriwa kupata muda binafsi ili kutafakari
yaliyotokea kwa siku hiyo na jinsi siku inayofuata inaweza kuwa nzuri na
ya mafanikio. Katika hili inashauriwa kuacha kutumia simu au komputa
pindi unapopanda kitandani badala yake funika macho na tafakari kuhusu
siku hiyo, itakusaidia kulala.
3. Fanya Sala
Inashauriwa pia kwa dini na imani yoyote, kufanya ibada au sala
kunasaidia akili ku relax na kufanya usingizi uje na unaweza kulala kwa
amani.
4. Soma kidogo vitu chanya
Jambo jingine ni kutafuta kitu cha kusoma chenye ujumbe au taarifa za
msingi na zilizo chanya. hatahivyo inashauriwa kisiwe kitu kirefu.
Inaweza kuwa kitabu cha hadithi, jarida, makala na vinginevyo.
5. Kuwa na ratiba maalumu ya kulala
Hii ni pale ambapo unakuwa na muda maalumu wa kulala na kuamka kila
siku bila kuivuruga. Suala hili litautengenezea mwili mazoea ya
kupumzika kwa wakati fulani lakini pia litakusaidia kuamka bila uchovu
au maumivu yoyote ya mwili. Hii pia itasaidia kulala bila shida kwa
wakati uliozoea.
6. Chunga tabia yako ya kulala
Ni muhimu sana kuzingatia kuachana na vitu vinavyoweza kusababisha
tatizo la kushindwa kulala wakati wa usiku ikiwa ni pamoja na kulala
wakati wa jioni jambo linaloweza kukata usingizi pindi muda wa kulala
unapofika wakati wa usiku.
7. Acha kuangalia TV nyakati za usiku sana
Pia ni muhimu kuachana na tabia ya kukaa macho na kuangalia TV
nyakati za usiku mwingi kwani mwili hujijengea kutolala wakati huo
unapofika kwani huwa ni muda ambao kwa kawaida unakuwa unaangalia TV.
Pia mwanga wa TV unaelezwa kukandamiza homoni ya melatonin
inayosaidia mwili wa binadamu kulala au kuamka pindi muda muafaka
unapofika.
8. Chunga unachokula au kunywa kabla ya kulala
wataalamu pia wanashauri kuwa ni muhimu kuangalia vitu vya kula au
kunywa unapoelekea muda wako wa kulala. Inashauriwa kuepuka kunywa
kahawa au pombe kabla ya kwenda kulala kwa sababu ni vitu ambavyo
vinachukua muda mrefu kuyeyushwa tumboni.
9. Andaa mazingira mazuri ya kulala
Kulala kwenye mazingira mazuri ni muhimu. Inashauriwa kulalia mashuka
masafi na mito misafi, huku eneo zima kama chumbani liwe safi lisilo na
vumbi wala harufu.
Pia kama huwezi kulala kukiwa na muziki usiwashe muziki lakini pia
kama kukiwa muziki unapata usingizi mzuri basi unashauriwa kufanya
hivyo.
10. Tumia choo kabla hujalala
Baadhi ya watu hupoteza kabisa usingizi na kushindwa kuupata tena
pindi wanapoamka usiku ili kwenda chooni au kwa sababu nyingine zozote.
Kwa mantiki hiyo wataalamu wanashauri ni vyema kwenda haja kabla ya
kwenda kulala ili kwamba mwili usisumbuliwe wakati umelala.