mwana wa liganga blog ni blog ya kutoa taarifa, matukio, yaliyotokea katika ulimwengu hususani katika nchi yaTanzania blog hii inasimamiwa na mwandishi wa habari kitaaluma bwana Deus Thomas liganga.lengo ni kutoa taarifa kwa umma,kwa maendeleo ya taifa na Dunia kwa ujumla kwa mawasiliano kuhusu mtangazo, habari, wasiliana nasi 0659944423,deusliganga@yahoo.com,mzeeliganga@gmail.com
Jumanne, 31 Oktoba 2017
Zitto Kabwe afunguka baada ya kuachiwa
Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema asingekamatwa na polisi angeshangaa.
Amesema hilo linatokana na kauli ambazo zilitolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali kuhusu takwimu alizotoa.
"Kila mtu alijua tutakamatwa na kama tusingekamatwa basi tungeshangaa,” amesema Zitto leo Jumanne Oktoba 31,2017 baada ya kuachiwa kwa dhamana na polisi.
Zitto amesema maelezo ya kina na ufafanuzi wa kauli zake zinazodaiwa kuwa za uchochezi atayatoa atakapofikishwa mahakamani.
Ufafanuzi mwingine anaodai atautoa atakapofikishwa mahakamani ni kuhusu masuala ya takwimu na makosa ya mtandao.
Pia, amewataka wanachama wa ACT Wazalendo kuendelea na shughuli zao kama kawaida na hasa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017.
Zitto baada ya kuachiwa, mwanasheria wake Stephen Mwakibolwa amesema akiwa Kituo cha Polisi Chang'ombe, mteja wake alihojiwa kwa kosa la uchochezi alilolifanya wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani Kijichi jijini Dar es Salaam, Jumapili Oktoba 29,2017.
"Pale Chang'ombe alihojiwa kwa uchochezi na baada ya mahojiano aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kurudi Jumatatu ijayo, lakini baada ya kuachiwa alikamatwa tena na kuletwa hapa (kituo cha polisi cha upelelezi wa makosa ya kifedha)" amesema Mwakibolwa.
Amesema makosa aliyohojiwa akiwa katika kitengo hicho ni kuchapisha au kutoa taarifa zisizo sahihi kinyume cha sheria ya takwimu na kusambaza taarifa za uongo kinyume cha makosa ya mitandao.
Mwakibolwa amesema Zitto amepewa dhamana
Mvua kubwa zatarajiwa kuanza kunyesha usiku wa leo
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa(TMA) imetangaza vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya masaa 24 vinatarajiwa kuanza usiku wa kuanzia leo Jumanne.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo leo Jumanne imeeleza kuwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani pamoja visiwa vya Unguja na Pemba yataaririka.
“Mvua hiyo inatarajiwa kusambaa katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Lindi kuelekea siku ya Ijumaa ya tarehe 3 Novemba 2017.”
“Hali hii inatokana na kuwepo na kuimarika kwa ukanda wa mvua (Inter Tropical Convergency Zone –ITCZ) katika maeneo hayo.”
Mamlaka hiyo imewataka wakazi wa maeneo yaliyotajwa kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa pamoja na tahadhari zinazotolewa
“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo kila itakapobidi.”
Ongezeko la walaji wa nyama ya mbwa nchini China lazua taharuki mitaani
Serikali nchini China kupitia wizara yake ya Afya ya Wanyama na Ukaguzi imedai kuwa ongezeko la walaji wa nyama ya mbwa nchini humo kumepelekea ongezeko la kesi za watu kupotelewa na mbwa kuongezeka.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la Change.Org nchini China kwa mwaka zaidi ya mbwa milioni 20 huchinjwa kwa kitoweo ambapo inakadiliwa kuwa mbwa milioni 2 huchinjwa kwa mwezi ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 ukilinganisha na mwaka 2015.
Serikali ya China tayari imeanzisha msako wa kukagua leseni za bucha zinazotoa huduma ya kuuza nyama ya mbwa ili kubaini ukubwa wa ongezeko la bucha zinazofanya kazi bila kibali maalumu.
Wiki iliyopita maafisa usalama nchini humo walikamata lori lenye mbwa 200 wakisafirishwa bila kibali maalumu na tayari mbwa hao wameshapata wenyewe.
aarifa hiyo imekuja baada ya maafisa usalama nchini humo kueleza kuwa kuna ongezeko la kesi za watu wakiripoti kila siku kupotelewa na mbwa majumbani kwao.
Tayari wanaharakati nchini China wameungana na nchi nyingine kulaani utumiaji wa nyama ya mbwa kama kitoweo huku wakidai kuwa sio unanyanyasaji wa Wanyama.
Nchini China baadhi ya watu hutumia nyama ya Mbwa kama kitoweo kama sehemu ya utamaduni wao.
Wakati hayo yanajiri, jana mtandao wa kupambana na ulaji wa nyama ya mbwa duniani wa Fight Dog Meat umeripoti kuwa nchini China kuna watu wanawauwa mbwa hao kwa kuwachoma kwa moto wa gesi hadi kufa na kuwafanya vitoweo.
Hata hivyo tayari wanaharakati wameanza kupiga vita tamasha kubwa la ulaji nyama ya mbwa la The Yulin Dog Meat Festival linalofanyika mjini Yulin nchini China kila mwaka ambapo inakadiliwa zaidi ya mbwa elfu 10 huchinjwa.
Vyanzo – TheFightDogMeat & Change Org
Manara: Tulinyimwa penati mbili dhidi ya Yanga
KLABU ya Simbe imelalamika kunyimwa penalti mbili na refa Hery Sasii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC uliomalizika kwa sare ya 1-1 Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara amesema refa alikwenda na matokeo yake uwanjani.
Manara aliwawekea Waandishi wa Habari video ya mchezo huo kuwaonyesha namna ambavyo refa Sasii hakutoa penalti licha ya mpira kuwagonga mikononi beki, Kevin Yondan na kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi Jumamosi.
Manara aliyewabeza watani wao hao wa jadi, kwamba ni kawaida yao kupendelewa na marefa kila wanapokutana na Simba amesema watapeleka malalamiko Bodi ya Ligi dhidi ya refa huyo na wengine walioionea timu yao katika mechi zilizotangulia.
Akasema huo ni mwendelezo wa matukio ya klabu yake kutotendewa haki na marefa katika mechi za Ligi Kuu msimu huu, akidai walinyimwa pia penalti mbili katika mechi dhidi ya Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kabla ya wapinzani wao wengine, Singida United kupewa penalti ya utata Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga.
Simba ilitoa sare ya 2-2 na Mbao FC kabla ya kushinda 3-1 dhidi ya Stand United, katika mchezo ambao pia walikataliwa bao zuri la mshambuliaji wao, Laudit Mavugo.
Pamoja na hayo, Manara amelalamikia kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kukataa ombi la klabu, Simba na Yanga kutaka mchezo wao ufanyike Uwanja mkubwa wa Taifa na kuupeleka Uwanja mdogo wa Uhuru.
Manara amesema hali hiyo ilizikosesha klabu fedha kutokana na watazamaji kutojitokeza kwa wingi kwa kuhofia usalama wao kutokana na udogo wa Uwanja wa Uhuru.
Aidha, Manara amesema kwamba kikosi cha Simba sasa kinaelekeza nguvu zake katika mchezo wake ujao dhidi ya Mbeya City Jumapili Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kikosi kitaondoka Ijumaa kwenda Mbeya na kitakaa kwa muda mrefu kutokana na kukabiliwa na mechi nyingine pia za Ligi Kuu Nyanda za Juu Kusini.
Jumatatu, 30 Oktoba 2017
Lazaro Nyalandu ajiuzulu Ubunge
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Nyalandu ameandika Ujumbe huu kama unavyosomeka hapo chini.
NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama
Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama
kuanzia leo, Oktoba 30, 2017.
HALIKADHALIKA, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job
Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la
Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa
vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo
mwaka 2000 hadi Sasa.
AIDHA, Nimechukua UAMZI huo kutokana
na kutoridhishwa kwangu na mwenendo wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni
pamoja na ukiukwaji wa HAKI za Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya
dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa
mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama)
kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia
Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.
VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna
namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa
ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge
na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha
kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba
Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.
MIMI Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia
kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa
Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa
hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM
imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo
awali. AIDHA, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na
Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna
Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama
kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya
Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.
HIVYOBASI, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na
haki ya KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na
nitaomba IKIWAPENDEZA wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA, basi waniruhusu kuingia MALANGONI mwao, niwe mwanachama, ili
kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya
kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru
wa mawazo.
VILEVILE, nimemua kujiuzulu KITI Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini
kuruhusu kufanyika kwa UCHAGUZI mwingine ili wananchi wapate fursa ya
kuchagua ITIKADI wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye
changamoto lukuki nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya
bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili
kwamba, SOTE kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi
ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania.
Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo
yote ya kiitikadi za Kisiasa, na makabila yote nchini uimarike.
Tushindane ki sera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama
ndugu, na TAIFA lililo imara na nchi yenye ADILI.
#MunguIbarikiTanzania.
Lazaro S. Nyalandu.
Jumapili, 29 Oktoba 2017
Rais Magufuli kufanya ziara na kuzindua miradi minne Mwanza
Rais John Pombe Magufuli anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili ya kikazi mkoani Mwanza na kufungua miradi minne inayolenga kuboresha uchumi wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema rais ambaye atafanya ziara kesho na kesho kutwa, ataongozana na viongozi wengine hadi katika Daraja la Furahisha na kulizindua.
Daraja hilo limejengwa ili kurahisisha mawasiliano kati ya waenda kwa miguu na vyombo vya moto.
Mkuu huyo wa mkoa alisema baadaye rais ataelekea Nyakato wilayani Nyamagana kufungua Kiwanda cha Sayona Drinks Limited na kuhitimisha ziara kwa siku hiyo.
Jumanne, rais atafungua Kiwanda cha Victoria Moulders and Polybags, kilichopo Igogo jijini Mwanza.
Alisema siku hiyo hiyo, ataelekea Buhongwa kwa ajili ya kufungua Kiwanda cha Dawa cha Prince Pharmaceutical Industry.
Mkuu huyo wa Mwanza aliomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na wadau wengine ili kufanikisha ziara ya Rais Magufuli.
“Naamini mkoa wetu umejaaliwa amani na ulinzi wa kutosha, hivyo basi, sitarajii kusikia ripoti yeyote ya utovu wa nidhamu,” alisema Mongella.
Mawakili watatu watimuliwa nchini
Serikali ya nchini Tanzania imewafukuza mawakili watatu wa Afrika Kusini waliokamatwa wiki hii Jijini Dar es Salaam wakituhumiwa kwa kuchochea mapenzi ya jinsia moja.
Mawakili hao waliofukuzwa ni wale waliokuwa miongoni mwa watu 13 waliokamatwa katika hoteli moja mjini Dar es Salaam wakijiandaa kufanya mkutano wa kujadili iwapo wakabiliane na uamuzi wa serikali ya Tanzania kuzuia utoaji wa baadhi ya huduma za afya au la kwa mujibu wa mawakili hao.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jana wakati akizungumza na wanahabari amewaambia kuwa kabla ya mawakili hao kukamatwa kwamba walikuwa wakichochea mapenzi ya jinsia moja.
Mapema mwaka huu, serikali ilipiga marufuku baadhi ya kliniki za kibinafsi kutotoa huduma za ugonjwa wa HIV na ukimwi ikisema zilikuwa zikukuza mapenzi ya jinsia moja ambayo ni haramu nchini Tanzania.
Hata hivyo kukamatwa kwa Mawakili hao kunatokea kufuatia hotuba ya mwezi Septemba iliotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Hamis Kingwangala (kwa sasa ni Waziri wa Maliasili) ambaye aliapa mbele ya bunge kukabiliana na makundi yoyote yanayounga mkono wapenzi wa jinsia moja nchini.
Jumamosi, 28 Oktoba 2017
MSIMAMO WA LIGI:
MSIMAMO WA LIGI: Kukiwa bado kuna mechi sita za mzunguko wa nane zinasubiri kupigwa kesho na kesho kutwa, huu ndiyo msimamo wa #VPL hadi sasa baada ya #KariakooDerby iliyomalizika kwa sare ya 1-1.
Endapo Mtibwa itashinda katika mchezo wake wa kesho dhidi ya Singida United, itakaa kileleni.
Ijumaa, 27 Oktoba 2017
kesho ndio kesho hatumwi mtoto dukani
Makocha wa Yanga na Simba, George Lwandamina na Joseph Omog, wanakutana kwa mara ya nne kwenye mashindano tofauti, lakini mwenye hasira zaidi ni Mzambia Lwandamina kwani mchezo wa Ligi kuu Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita uliochezwa Februari 25 mwaka huu, alichapwa 2-1, huku Nusu fainali ya kombe la Mapinduzi 2017 na Ngao ya Jamii 2017 akipoteza kwa mikwaju ya penati dhidi ya Mcameroon Omog, kufuatia kutoka suluhu ndani ya dakika 90'.
Safari hii kuelekea 'Dabi ya Kariakoo' mzani umebalansi, timu zote zinaingia dimbani zikitoka kupiga 4G.
Yanga SC yaonyesha jeuri yazindua Magazine siku moja kabla ya Darby
Klabu ya soka ya Yanga hii leo imezindua rasmi Magazine yake ikiwa imesalia siku moja kabla ya mchezo wao wa Dar es salaam Darby dhidi ya hasimu wake Simba SC ikiwa na lengo la kujiongezea kipato.
Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram wa klabu ya Yanga hapo jana imeeleza kuiingiza rasmi sokoni Magazine hiyo hii leo siku ya Ijumaa.
Tunapenda kuwataarifu wanachama, mashabiki na wadau mbalimbali wa soka kuwa ‘Yanga Magazine’, itaanza kuuzwa rasmi kesho (Ijumaa) kuanzia saa 3:00 Asubuhi Makao Makuu ya Klabu.
Morogoro – Kwa Hamad Islam
Kwa wale wanaohitaji kuwa mawakala, wanakaribishwa.
Simba yatua Dar kimyakimya
Kikosi cha Simba kimeondoka Visiwani Zanzibar leo asubuhi kwa ndege kurejea jijini Dar es Salaam kwa maandalizi ya mwisho ya mechi yao ya kesho ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Yanga kwenye uwanja wa Uhuru.
Afisa Habari wa Simba Haji Manara amesema akili yao yote ni kuifunga Yanga kesho kwenye uwanja wa Uhuru huku akiwataka Mashabiki wa Simba waende uwanjani kwa wingi kuishangilia timu yao.
“Kambi ya Zanzibar ilikuwa nzuri sana naamini tumefikia malengo yetu, hapa tunaondoka na leo jioni Dar tutafanya mazoezi ya mwisho, nawaomba Mashabiki wa Simba wazidi kuishangilia timu yao,” Manara ameuambia mtandao huu wakati waondoka hapa Zanzibar kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Simba walikuwa kambini mjini hapa tangu Jumatatu ya Oktoba 23 na leo Ijumaa Oktoba 27 wamerejea nyumbani Dar es salam kuwavaa Yanga.
SIMBA WANATUA DAR NA NDEGE ZA KUKODI TAYARI KWA GAME YA KESHO
Kikosi cha Simba kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam leo kwa maandalizi ya mwisho ya mechi yao ya kesho dhidi ya Yanga.
Simba
walikuwa kambini mjini Zanzibar kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara
itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Taarifa zinaeleza, Simba watawasili kwa kutumia ndege za kukodi tayari kwa ajili ya mechi hiyo.
Kikosi hicho kitaingia kambini jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mwisho.
Hata
hivyo, Simba wamekuwa wakifanya uficho kuhusiana na sehemu watakayokaa
jijini Dar es Salaam wakimalizia maandalizi yao hayo ya mwisho kabla ya
kesho.
YANGA SC WAREJEA LEO DAR TAYARI KUIVAA SIMBA KESHO
YANGA SC wanaondoka mchana wa leo Morogoro baada ya mazoezi ya asubuhi kurejea Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC kesho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Na wakifika Dar es Salaam, watakwenda kuweka kambi nyingine katika hoteli moja nzuri katikati ya Jiji, ambako ndiko wataondokea kesho kwenda Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya mchezo huo utakaoanza Saa 10:00 jioni.
Yanga ilikuwa Morogoro tangu Jumanne jioni ikitokea Shinyanga, ambako Jumapili walishinda 4-0 dhidi ya wenyeji Stand United katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Baada ya mazoezi ya siku tatu, mabingwa hao watetezi wanarejea Dar es Salaam kujaribu kusaka ushindi wa kwanza dhidi ya Simba baada ya mechi nne za mashindano yote tangu msimu uliopita.
Mara ya mwisho Yanga kuvuna ushindi kwa Simba ilikuwa ni Februari 20, mwaka 2016 wakishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu, mabao ya Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72.
Baada ya hapo, mechi nne zilizofuata, Yanga wakafungwa tatu, moja ya Ligi Kuu na nyingine za Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii.
Oktoba 1, mwaka walitoa sare ya 1-1, Amissi Tambwe akianza kuifungia Yanga dakika ya 26, kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 87, kabla ya Januari 10, mwaka huu Wekundu wa Msimbazi kushinda tena kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Februari 26, Simba wakatoka nyuma kwa bao la penalti la Simon Msuva dakika ya tano na kushinda tena Simba 2-1 kwa mabao ya Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 66 na Kichuya dakika ya 81, kabla ya Agosti 23, mwaka huu kushinda tena kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
Na kesho Yanga watatafuta ushindi wa kwanza dhidi ya Simba ndani ya mechi tano.
Joti akana utani wa ndoa, afanya kweli
Mchekeshaji mkongwe Bongo, Joti hatimaye ameamua kuachana na utani wa
kudai anaoa na kuamua kufanya kweli kwa kudhihirisha yupo serious
kidogo kwa jambo la mahusiano kwa kutarajia kuvuta jiko hivi karibuni.
Joti ambaye anafahamika kwa kufanya matangazo mengi ikiwemo ya kufunga ndoa , aliambatana na watu wake wa karibu katika sendoff yake iliyofanyika siku ya jana( Alhamisi) akiwa na mchekeshaji Seki.
Mchekeshaji huyo mwenye dili kibao town anatarajia kufunga ndoa rasmi hivi karibuni na atakuwa ameingia kwenye orodha ya mastaa wa Bongo waliopo katika ndoa kama Babuu wa Kitaa, Mx Carter, Kenedy The Remedy, Professa Jay, ZamaradI Mketema na Frola Mbasha.
Joti ambaye anafahamika kwa kufanya matangazo mengi ikiwemo ya kufunga ndoa , aliambatana na watu wake wa karibu katika sendoff yake iliyofanyika siku ya jana( Alhamisi) akiwa na mchekeshaji Seki.
Mchekeshaji huyo mwenye dili kibao town anatarajia kufunga ndoa rasmi hivi karibuni na atakuwa ameingia kwenye orodha ya mastaa wa Bongo waliopo katika ndoa kama Babuu wa Kitaa, Mx Carter, Kenedy The Remedy, Professa Jay, ZamaradI Mketema na Frola Mbasha.
Mvua Yasababisha Madhara Makubwa Jijini Dar.......Watu 6 Wahofiwa Kusombwa na Maji
Mvua
iliyonyesha usiku wa kuamkia jana, iligeuka kuwa balaa baada ya
kusababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na watu sita kutojulikana
walipo na zaidi ya nyumba kubomoka eneo la Mbezi.
Kama ilivyo kawaida jijini Dar es Salaam, mvua hiyo iliharibu miundombinu ya usafiri ya maeneo kadhaa, ikisababisha baadhi ya barabara kutopitika na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Kasi (Udart) kulazimika kusimamisha shughuli zake.
Udart
imesema jana kuwa ilisitisha huduma kutokana na eneo la Jangwani,
ambako kuna ofisi zake, kujaa maji hivyo kuathiri shughuli zake.
“Tumesitisha
huduma za mabasi yote kutokana na eneo la Jangwani kujaa maji,” alisema
mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Udart, Deus Bugaywa.
Barabara
kadhaa zilikuwa hazipitiki magari na watembeao kwa mguu, huku mitaa
kadhaa ya maeneo ya Jangwani ikiwa imefurika maji na kusababisha wakazi
kukimbilia Barabara ya Kigogo-Mabibo kushuhudia maji hayo, ambayo pia
yalifurika hadi juu ya daraja la Kigogo Mwisho.
Wakazi
wa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam walikumbwa na mshangao
jana alfajiri wakati walipokuta maeneo yao yamefurika maji kutokana na
mvua hiyo iliyonyesha kuanzia juzi jioni na kuendelea usiku kuamika
jana. Baadhi walishuhudia nyumba zao zikibomka na madaraja kukatika.
Mvua
hizo zilisababisha daraja eneo la Mbezi kuvunjika na hivyo basi la
daladala lililokuwa limebeba abiria kutoka Segerea kuelekea Mbezi Mwisho
lilikwama daraja baada ya kuzidiwa na kasi ya maji yaliyofunika daraja
hilo.
Abiria waliokuwa ndani ya daladala hilo waliokolewa wote huku mmoja wao akizimia na kupelekwa hospitali.
Mvua
hiyo pia ilisimamisha shughuli za kijamii, wananchi walishindwa kwenda
kazini wakiwamo wanafunzi ambapo walishindwa kufika shuleni kutokana.
Maji
yalijaa barabarani huku shughuli za usafiri zikisimama , maduka na
vibanda vya biashara vilifungwa na vingine vikisombwa na maji.
Pia
mwenyeki wa Mtaa wa Kiluvya kwa Komba, Julius Mgini alisema watu sita
wanasadikiwa kusombwa na maji eneo hilo akiwamo mtoto mmoja na nyumba za
familia tatu zimebomoka.
“Katika
eneo langu kuna daraja limekatika na watu sita wanasadikiwa kusombwa na
maji. Waliosombwa ni pamoja na mtoto mdogo ambaye bado hatujajua umri
wake,” alisema.
Hata
hivyo, kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Jumanne Muliro alisema bado
wanakusanya taarifa za mafuriko hayo na baadaye kuzipeleka kwa kamanda
wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.
Kamanda Mambosasa pia alisema wanafanya tathimini ili kujua athari za mafuriko.
==> Picha zote na Iman Nsamila
==> Picha zote na Iman Nsamila
Polepole awatahadharisha wanaotaka kuhamia CCM
Katibu
wa Itikadi na wa na Uenezi CCM Taifa, Ndg. Humphrey Polepole
amewatahadharisha watu wanaotaka kujiunga ndani ya Chama Cha mapinduzi
kwa kudhani kwamba kuna namna rahisi ya kupata pesa asiende ndani ya
Chama hicho kwa sasa.
Akifanya
mahojiano maalumu na East Africa Tv, Polepole amesema kwamba mambo
ambayo yanatajwa na kuhusishwa kwenye CCM kama Rushwa na ununuzi wa
madiwani hayana nafasi ndani ya chama chao kwani havina mashiko kwani ni
kinyume na misingi pamoja na imani ya chama hicho hivyo watu wasijipe
imani kuhamia huko wakidhani watapata nafasi.
Polepole
amesema kwamba anafahamu kwamba wapo viongozi wengi sana wanaotaka
kuingia kwenye chama cha mapinduzi kuliko hata wale ambao tayari
wamekwisha pokelewa na hiyo ni kwa sababu chini ya uongozi wa awamu ya
tano wameweza kufikia matarajio na yale ambayo yalikuwa yakipigiwa
kelele.
"Waliokuja
CCM ni wachache mno. Bado wapo viongozi wengi sana ambao wapenda kuja
kwenye chama chetu, nikiri ni wengio kuliko ambao tumewapa ridhaa.
"Wengi ambao wanaomba kurejea kwenye chama cha mapinduzi ni wale waliokuwa tofauti na CCM lakini kinachofanya na ndugu yetu Magufuli ndicho walichokuwa wakitaka kukiona kwa muda mrefu.....
"Watu wengi waliamini CCM ni ileile ni kweli lakini ni ilele imekuwa chama ambacho kinaongozwa katika misingi ambayo ipo kwenye katiba...." Amesema Polepole
"Wengi ambao wanaomba kurejea kwenye chama cha mapinduzi ni wale waliokuwa tofauti na CCM lakini kinachofanya na ndugu yetu Magufuli ndicho walichokuwa wakitaka kukiona kwa muda mrefu.....
"Watu wengi waliamini CCM ni ileile ni kweli lakini ni ilele imekuwa chama ambacho kinaongozwa katika misingi ambayo ipo kwenye katiba...." Amesema Polepole
Polepole
amesema kwamba kwa sasa CCM imejikita kuwa chama cha wanachama wenyewe
na siyo kuwa kikundi cha watu ambacho kinatatua matatizo ya watanzania.
Jinsi Mgonjwa wa Kisukari anavyoweza kuepuka Kiharusi (Kupooza) au Stroke
Ni dhahiri kuwa wagonjwa wengi siku hizi wamekuwa wakikumbwa na tatizo hili la kupooza ambalo wengi huwakumba ghafla wakiwa hawana ufahamu wowote nini ambacho kimetokea.
Kabla zijakuelimisha mengi mpendwa msomaji wangu wa Makala zangu, basi leo nakupa maana ya baadhi ya maneno haya:
1. KUPOOZA
Hii ni ile hali ya kiungo kupoteza utendaji kazi wake kwa sababu ya neva za fahamu kuathiriwa.
2. KIHARUSI AU STROKE
Hii ni ile hali ya ubongo kupata hitilafu katika kupokea damu na hatimaye kupelekea kupooza kwa viungo baadhi au mwili mzima. Na endapo seli za ubongo zikikosa damu na oksijeni kwa dakika 3 zinaanza kufa na kupoteza utendaji kazi wake na endapo hili tatizo lispo shughurikiwa ndani ya masaa matatu dalili zake zinakuwa zimefikia pabaya sana katika matibabu.
Sasa basi ningependa kuongelea kidogo kuhusu ugonjwa huu na jinsi gani unaweza kujizuia.
SABABU ZISIZO EPUKIKA
Napenda kusema kwamba, Katika kitabu cha The China Study kilicho andikwa na Prof. Collin Campbell kinasema kwamba, kila binadamu ana chembe chembe za vina saba yani DNA za urithi kutoka kwa wazazi wetu ambazo zinarithishwa kila kizazi. Hivyo kila mtu ana viini vya urithi vya magonjwa mbalimbali kutoka kwa wazazi wetu, ni jukumu lako kufanya chembe chembe hizo zijioneshe wazi wazi. Hivyo bwana Campbell ambaye ni mtafiti mashuhuri wa lishe na magonjwa alisema kuwa, ni jukumu lako wewe kuuchokoza mwili wako uwezo kuonesha magonjwa ambayo umeyarithi kutoka katika ukoo wenu. Endapo ukiishi maisha ya kiafya, kula vizuri vyakula vya asili hutasumbuka na magonjwa tabia kama kisukari,shinikizo la damu,uvimbe kwenye kizazi,ugumba,kansa nk.
Kwa sababu tumeshindwa kuishi maisha ya uhalisia wetu,tunaishi kwa kufurahia vyakula vilivyofanyiwa marekebisho na binadamu na kufurahia bei yake ilivyo ndogo katika kiwango cha kujitosheleza, Basi swali la kujiuliza ni kwa nini vyakula hivyo vya viwandani vinauzwa bei ya chini sana kuzidi vyakula asili? Hebu nenda leo ukanunue nyanya ambazo unaweza kukamua ukapata chupa moja ya 400mls! UTAGHARIMIKA PESA KUBWA KULIKO YULE ALIYENUNUA Nyanya iliyotengenezwa kiwandani na kuwekwa kwenye chupa maalumu, Jiulize tena Kwa nini vinauzwa bei ya kiwango cha chini kiasi hicho?
Mwenendo huo wa maisha ya ulaji vyakula vya viwandani,vinywaji vyenye sukari nyingi,radha,rang ink, unatufanya tuwe na vihatarishi vya kupata ugonjwa wa kupoooza bila kuwa na uwezo wa kuepuka hadi pale tutakapo badili mwenendo wa maisha yetu.
1. UMRI
Tafiti zinaonesha kuwa kadri umri wako unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo unavyozidi kuwa hatarini sana kukumbwa na tatizo la kupooza. Umri Zaidi ya miaka 50 upo katika hatari kubwa sana ya kupata magonjwa yatakayokupelekea kupata kiharusi. Kwani kiharusi ni ugonjwa moja wapo utakao kupelekea kupooza kwa baadhi ya viungo vya mwili wako na haimaye mwili mzima.
Hivyo kama wewe bado hujafikia katika umri huu, basi ni wakati wa kuishi katika lishe asili Inatoka katika mashamba yetu ya wakulima.
2. JINSIA
Tafito zinaonesha kwamba wanaume wako hatarini sana kupata kiharusi ukilinganisha na jinsia ya kike. Lakini pia tafiti zinaonesha kuwa kati ya mwanamke na mwanaume, mwanamke ndiye yupo hatarini sana kupata kifo kitokanacho na kiharusi. Hivyo endapo mwanamke akipatwa na kiharusi maendeleo yake kuanzia anapopatwa na tatizo huwa sio mazuri sana ukilinganisha na mwanaume. Hivyo mwanamke huwahi kukutwa na kifo Zaidi ukilinganisha na mwanaume anaweza kukaa muda mrefu sana.
3. URITHI
Kuna watu wenye historia kuwa katika ukoo wao kuna watu wenye matatizo ya kiharusi au babu, bibi alikumbwa na tatizo hilo. Hivyo hata wewe unaweza ukawa hatarini kupata tatizo kama hilo endapo tu maisha unayo ishi nayo yakiwa ni maisha yasiyo jumuisha lishe ya asili ninayopenda kuita lishe ya dawa.
4. KAMA UMESHAWAHI KUPATWA KIHARUSI KIDOGO
Hii ni aina ya kiharusi inayotokea kwa muda mfupi na kupotea. Muda mwingine huwa ni vigumu kutofautisha na kiharusi chenyewe. Maana kiharusi kidogo (Transient Ischemic Attach) husababisha pia viungo kupoteza utendaji kazi wake na inaweza pia kuathiri utendaji kazi wa ubongo kiakiri pia. Hivyo kama umeshaga wahi patwa na TIA kipindi cha nyuma, uwezekano wa kupata tena ni mkubwa sana, na unaweza kupata kiharusi kabisa chenyewe.
Hapo juu nimesema kuwa ni vihatarishi visivyozuilika LAKINI ni kwa wale wasioweza kubadili mienendo ya maisha ya kifahari na kujiepusha na magonjwa tabia kama kisukari,shinikizo la damu na kiwango kikubwa cha lehemu mwilini mwako
SABABU UNAZOWEZO KUZISABABISHA WEWE MWENYEWE NA KUKUPELEKEA KUPATA KIHARUSI ( STROKE)
1. MAGONJWA YA MOYO
Magonjwa ya moyo kwa umri Zaidi ya miaka 60 imekuwa ni kawaida kutokana na miili yetu kuwa na kiwango kikubwa cha sumu mwilini mwetu na miili yetu kuwepo katika mazingira ya kupokea vyakula visivyo vya msingi katika kuboresha utendaji kazi wa mwili wako na tofauti na kuharibu uwezo wa mwili wako kufanya kazi ipasavyo.
Moja wapo ya magonjwa yanayopelekea kupata kiharusi, ni pale moyo wako unaposhindwa kutengeneza umeme wa kutosha kutoka juu kwenye vyumba vya moyo viitwavyo Atria na hatimaye kusambaa kwenye vyumba vya chini vya moyo viitwavyo Ventriko. Hivyo basi napenda kukuambia kuwa, moyo hutengeneza umeme, na umeme huo huzunguka kwenye sakiti ya umeme wa moyo, sakiti hio huanzia kwenye vyumba vya juu vya moyo na kushuka vyumba vya chini na hatimaye kusambaa katika misuli yote ya moyo na hatimaye kusukuma damu kutoka kwenye moyo.
Hivyo kunapokuwa kuna hitirafu katika utengenezwaji wa umeme kuanzia sehemu husika, umeme unatengenezwa usiotosheleza na unatoka sehemu mbalimbali (sio maalumu) unajikuta misuli ya moyo inapata umeme kutoka katika vyanzo tofauti na umeme huo hautoshelezi kuweza kusukuma damu ipasavyo. Ugonjwa huu kwa lugha ya kiratini tunaita Atrial Fibrillation. Hivyo moyo wako unapokuwa na tatizo hili, hata mapigo ya moyo hubadirika.
Njia pekee ambayo unaweza ukajigundua kuwa una tatizo hili, ni kuangalia kiashiria cha mapigo ya moyo sehemu mbali mbali kama shingoni,juu ya mkoni wako karibu na kiganja kama mapigo ya moyo yanaenda sawa au laa! Pia unaweza kwenda Zaidi kufanya uchunguzi kama kipimo cha ELECTROCARDIOGRAM (ECG) unaweza kupata majibu halisi kuwa umeme huo unajitosheleza au laa! Na unatengenezwa kutoka katika chanzo kimoja au laa! Pia moja ya sababu moja wapo ni kuangalia misuli ya moyo na kiwango cha damu kinachosukumwa na myo wako, ni vyema pia ukipata kipimo kingine cha moyo kinaitwa ECHOCARDIOGRAM(ECHO) hiki kinakupa taarifa zote za kiwango cha damu kinachosukumwa,ukubwa wa misuli ya moyo, na taarifa zinginezo. Kumbuka vipimo hivi vinapatikana katika hospitali kubwa za rufaa na vinategemea umahili wa mpimaji na msomaji wa majibu yako.
Ugonjwa huu wa moyo unaweza kusababisha kiharusi kwa sababu moja kuu kwamba, pale moyo unaposhindwa kutenegeneza umeme wa kutosha kusukuma damu, kutakuwa na mrundikano wa tamu kwenye moyo na damu hio inaweza kuganda na hatimaye kusukumwa kwenda kwenye mishipa midogo ya ubongo na kusababisha kizuizi cha damu kufika kwenye ubongo kwa sababu ya kutwama kwa damu iliyo ganda. Hivyo ndivyo unaweza kupata kiharusi endapo moyo wako hautengenezi vizuri umeme wake.
2. KIWANGO KINGI CHA CHOLESTERO(LEHEMU) MBAYA MWILINI MWAKO
Lehemu kwa tafsiri nyepesi ni fati(mafuta) ambayo ipo kama nta ( wax) huzunguka sehmu mbalimbali katika mwili wako kwa kupitia mfumo wa mzunguko wa damu.
Ikumbukwe Lehemu ina kazi kubwa sana miilini mwetu kama kutengeneza seli za mwili na kutengeneza homoni za miili yetu na kazi zingine nyingi. Hivyo basi ningependa kukuambia kuwa kuna ina kuu tatu za lehemu ambazo ningependa kuzitaja kwa ufupi katika makundi makuu mawili, Lehemu mbaya ambayo inajulikana kama Low density Lipoprotein (LDL) pia na Triglycerides na aina ya pili ni lehemu nzuri ijuilikanayo kama Hingh density Lipoprotein –HDL.
Lehemu inaweza kusababisha kiharusi kwa sababu ya tabia yake mbaya ya kunasa kiurahisi kwenye kuta za mishipa ya ateri na hatimaye kupunguza kipenyo cha mshipa wa damu au kuziba kabisa na hatimaye kuzuia damu kufika vizuri katika ubongo na hatimaye ubongo hukosa damu na oxygen.
Tafiti zinaonesha kwamba ulaji wa nyama za aina yoyote ile, zina kiwango kingi sana cha lehemu mbaya ambayo inaenda kutuathiri sana. Lakini pia tafiti zinaonesha kwamba ulaji wa vyakula vya mboga za majani, matunda vinasaidia sana kuepukana na lehemu mbaya na kumaliza kabisa matatizo yanayo sababishwa na lehemu mbaya mwilini mwako.
Rehemu hujulikana kama kisababishi kikubwa cha aina moja wapo ya kiharusi kinachosababishwa na mishipa midogo ya damu kutopitisha damu na kuulisha ubongo wako vizuri na hatimaye seli za ubongo huanza kufa nah ii hutokea baada tu ya ubongo kukosa damu kwa muda wa dakika tatu.
Aina hii ya kiharusi huitwa ISCHEMIC STROKE (Ischemia, Ni ile hali cha seli za mwili kufa Kwa kukosa oxygen, na Stroke ni kupooza). Hivyo Ischemic stroke ni kupooza kunako sababishwa na kukosa hewa ya oksijeni kwenye ubongo kwa sababu ya kukosa damu kwenye ubongo kunakosababishwa na kuziba kwa mishipa midogo midogo inayopeleka damu kwenye ubongo.
Unaweza kuchunguza kiwango chako cha lehemu kama kingi au laa! Unaweza kwa kuchunguza kitalamu kwa kuchukua sampuli ya damu na kupeleka maabala (Biochemistry Lab) na hatimaye utapata majibu yako. Pia unaweza ukatumia vipimo vingine vya picha vinavyopima kiwango cha lehemu mbaya moja kwa moja kwenye mishipa ya damu Angiogram na pia unaweza kupima kwa kutumia Kipimo cha kuangalia uzalishaji wa umeme kwenye moyo kwani lehemu ni chanzo kikubwa sana cha kuharibu utendaji kazi wa moyo hivyo kipimo cha Electrocardiogram kinaweza pia kutumika na kuangalia moja kwa moja.
Note: Napenda kutoa angalizo kuwa vipimo vingi ninavyotaja hapo ni vikubwa sana na gharama yake kidogo kubwa na vingi vinapatikana hospitali ya rufaa na kwenye vituo mbali mbali binafsi. Na hivyo wengi wenu mmekuwa mkiniuliza kama Dr Boaz Mkumbo naweza kuwasaidia kwa hilo.
Napenda kuwasaidia kama ninavyokupatia elimu hii ya afya bure kabisa, ushauri wangu ni kwamba vipimo vyote vya kitaalamu vinategemea na mpimaji na msomaji ana taaluma gani katika kusoma majibu. Kama mpimaji akipotosha na daktari anayetibu atapotoka na hapa ndipo madhaifu makubwa ya vipimo hivi vingi na ndio maana magonjwa mengi tunashindwa kuyabaini mapema kwa kukosekana kwa ufanisi kwa watu wanaopima.
Sasa ningependa kukupa siri moja ya vipimo vyote nilivyo vitaja hapo juu, Vina hitaji umahili mkubwa wa kusoma majibu, na vituo vingi binafsi havina watu mahili wa kusoma vipimo hivi ,viko pale kama kitega uchumi kukushusha roho kuwa umepima. Tatizo sio kupima, Kiu ni kugundua ugonjwa sahihi na utibiwe upone. Ningependa kukushauiri kama unahitaji vipimo hivi, fika hospitali yenye wataalamu wa kutosha wenye uwezo mkubwa wa kukupa majibu ya uhakika ya kukata kiu yako.
- American Diabetes Association Inashauri kiwango cha LDL cholesterol kuwa chini ya 100 mg/dl kwa watu wenye kisukari na chini ya 70 mg/dl kwa watu wenye magonjwa ya moyo.
-Pia inashauri kuwa kiwango cha lehemu nzuri yani HDL iwe 50 mg/dl au Zaidi kwa wanawake na kwa wanaume HDL iwe 40 mg/dl au Zaidi.
3. SHINIKIZOLA JUU LA DAMU( HIGH BLOOD PRESSURE)
Shinikizo la damu ni msukumo wa damu ndani ya mishipa ya damu thidi ya ukuta wa mishipa. Shinikizo la damu lenye takwimu ya Zaidi 140/90 mmhg kwa muda mrefu utakuwa unastahili kuitwa mgonjwa wa shinikizo la juu la damu.
Shinikizo kubwa la damu husababisha kiharusi kwa kusababisha mishipa midogo ya damu ya ubongo kupasuka na hatimaye damu kuvia kwenye ubongo. Aina hii ya kiharusi huitwa Hemorrhegic Stroke. Aina hii ya kiharusi ni mara chache sana kutokea na huwa ni nadra sana kukuta mtu ana aina hii ya kiharusi lakini ndio aina nambari moja inayoweza kusababisha kifo haraka sana kwa mgonjwa. Kwani wagonjwa wengi wanaopata aina hii ya kiharusi huwa maendeleo yao sio mazuri na wengi hufika hospitali wakiwa hawajitambui kabisa.
Ugonjwa wa Shinikizo la damu unazuilika kabisa kwa kufuata masharti machache kama haya hapa chini:
- Ulaji wa vyakula vya madini ya potasiamu hadi kufikia 3900mg kwa siku kutoka kwenye ndizi,machungwa,matunda yaliyo kaushwa,viazi vitamu nk
- Ulaji wa Madini ya Calcium angalau 1200mg kila siku kutoka kwenye vyakula kama mtindi na maziwa ya kuwaida
- Ulaji wa vyakula vyenye magnesium angalau 420mg kwa siku kwa wanaume na 320mg kwa wanawake kutoka kwenye vyakula kama Spinachi, nafaka isiyokobolewa, Ndizi nk
4. KUTOFANYA MAZOEZI YA VIUNGO
Mazoezi siku hizi yamekuwa yakitumiwa na watu pekee wanao hitaji kupunguza mwili na kupunguza nyama uzembe ( belly fats) ,inapendeza sana wadada wengi kuchukia kubadirika kwa miili yao unaotokana na ulaji wa vyakula visivyo asili, Napenda kukuambia kuwa Mazoezi pekee sio SULUHISHO LA KUPUNGUZA MWILI WAKO, NA WALA SIO SULUHISHO LA KUONDOA NYAMA UZEMBE. Bali siku ukijifunza kubadili mwonekano wa sahani yako mezani utafurahia jinsi uzito unavyopungua! Najua huamini, lakini unapokuwa unaanza safari ya kupunguza uzito na nyama uzembe ujue ni safari nzito kama vile safari ya kutafuta pesa. Kupungua uzito sio kurahisi ingekuwa rahisi wengi hawapendi wangekuwa wameshapungua ! Njia pekee ni kujidhatiti na kudhubutu pekee katika kubadili lishe yako, mchawi mkubwa ni sahani yako unayoiweka mbele yako kila utakapo kuweka kitu kinywani mwako.
Mazoezi huimarisha viungo na mzunguko wa damu na kusaidia mwili wako kutoa taka ambazo zimepatikana kutokana na shughuli za mwili.
Tafiti zinaonesha kwamba watu ambao hawafanyi mazoezi ya kutosha katika umri mkubwa huwa hatarini kupata kiharusi aina ya Ishemic stroke inayosababishwa na damu kutosukumwa ipasavyo katika mishipa ya damu na kusababisha emboli kunasa kwenye mishipa ya damu na kuzuia damu kufika vizuri katika ubongo.
MAKUNDI MENGINEYO AMBAYO SITAPENDA KUYAELEZA KWA KINA LEO
5. Walevi wa pombe na sigara
6. Wanaotumia njia za uzazi wa mpango kwa muda mrefu
7. Watu wenye kisukari kwani kisukari na shinikizo la damu ni bwana harusi na bibi harusi mara nyingi hutembea kwa umoja.
90 DAYS CARDIO FUNCTION-REVERSE PACKAGE
Hii ni program maalumu kwa wasomaji wetu ambao wamekuwa wakisumbuka na magonjwa sugu kama kisukari,shinikizo la juu la damu n ahata shinikizo la chini la damu, kiharusi n ahata tatizo la kupungua kwa utendaji kazi wa ubongo.
Hii program imeandaliwa na Boaz Mkumbo ambapo inawafaa wale wachache wanaohitaji msaada wangu pale walipofikia kutumia elimu hii ya afya ambayo nimekuwa nikiitoa kila siku.
NDANI YA CARDIO FUNCTION REVERSE PACKAGE
1. Unajipatia msaada wa kupata Suluhisho la kuondoa lehemu zote mbaya mwilini mwako na kuimarisha mzunguko wa damu kwenda sehemu mbalimbali za mwili na kuimarisha damu inayoenda kulisha ubongo.
2. Utajipatia Kiondoa sumu makini kabisa chenye kuzuia mchakato unaendelea mwilini mwako ( Gut and systemic Inflammation) chenye kusheheni madini mengi ambayo ni catalyst ya shughuri nyingi za mwili madini haya husaidia kuupooza mwili kutoka katika mpambano wa maradhi mbali mbali yanayoendelea mwlini mwako, Madini mengi ya Manganeze,zinc,selenium,Iron na mengine mengi kwani kimekuwa ni chakula nambari tatu kama lishe bora duniani
3. Unaweza kupatiwa ushauri kwa wale waliotayari pata tatizo la kupooza kutokana na kiharusi na presha yako haijakaa sawa, Utapewa huduma nzuri namna gani unaweza pia ukanufaika na mazoezi ya viungo na bidhaa zetu unapokuwa katika matibabu chini ya ushauri wetu.
4. Napenda kuwaambia kuwa msaada huu ndani ya package hii ya siku 90 tutakusaidia endapo tu , unahitaji kwani wengi wanafurahia huduma zetu za tiba asili na pia ushauri tunatoa kwa watu wenye matatizo ya magonjwa haya sugu.
CHADEMA kwenda Mahakamani kumnasua Mkurugenzi wake Polisi
aada ya Polisi kuendelea kumshikilia Mkurugenzi wa Chadema wa Operesheni na Mafunzo, Kigaila Benson chama hicho kimesema kimekwenda Mahakama Kuu kuiomba itoe amri kwa jeshi hilo kumfikisha kortini.
Wakati Chadema ikisema hayo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jana Alhamisi Oktoba 26,2017 alisema, “Upelelezi unaendelea na huenda kesho(Ijumaa hii) akafikishwa mahakamani.”
Kigaila anashikiliwa na polisi tangu Jumatatu Oktoba 23,2017 aliporipoti Kituo Kikuu cha Polisi cha kanda hiyo kuitikia wito wa jeshi hilo.
Taarifa ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene iliyotolewa jana Oktoba 26,2017 imesema baada ya kumaliza mahojiano, askari kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), waliokuwa wakimhoji Kigaila walisema hawana mamlaka ya kumwachia kwa dhamana.
Makene alisema sababu waliyoitoa ni kwamba wakubwa na wenye mamlaka ya kuruhusu dhamana au kutoa dhamana hawakuwepo ofisini.
“Juhudi za mawakili waliokuwepo polisi kumpatia Kigaila msaada wa kisheria, kueleza kuwa dhamana ni haki yake kwa mujibu wa sheria, huku wakihoji ni kwa nini kusifanyike mawasiliano ili hao wakubwa watoe ruhusa hiyo hata kama wako nje ya ofisi, hazikufua dafu!” alisema Makene.
Alisema tuhuma alizohojiwa Kigaila zilihusu kauli za uchochezi anazodaiwa kuzitoa Septemba 12,2017 siku chama hicho kilipotoa tamko la maazimio ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu iliyoketi kujadili tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.
Makene alisema kwa kuitikia wito wa Jeshi la Polisi na kwenda mwenyewe kituoni, ni sababu inayojitosheleza kuonyesha kuwa Kigaila ni mwaminifu na anatoa ushirikiano kwa sheria za nchi.
“Bila kumfikisha mahakamani au kumwachia huru, tafsiri yake ni kwamba Kigaila anashikiliwa na jeshi hilo kinyume cha sheria za nchi,” alisema.
Alisema Chadema imeagiza Kurugenzi ya Katiba na Sheria kuratibu na kusimamia hatua za kisheria ili kuhakikisha Kigaila anapata haki zake za msingi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Dawa za kulevya zakamatwa
Mwanza. Maofisa wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama usiku wa kuamkia juzi walikamata zaidi ya kilo 100 za mihadarati aina ya heroin zilizokuwa zikisafirishwa kwenye jahazi kutoka Unguja kwenda Dar es Salaam.
Maofisa hao wa nchini wakishirikiana na vyombo vingine vya kimataifa walilitilia shaka na kuamua kulizuia jahazi hilo lililokuwa na raia kumi wa Iran na Wazanzibari wawili.
Kamishna wa sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki amesema baada ya upekuzi wa awali walifanikiwa kukamata paketi 104 za dawa wanazoshuku kuwa ni heroin ambazo watazipeleka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa vipimo.
“Tunaendelea na ukaguzi wa jahazi na sasa tumepeleka mbwa kusaidia kazi hiyo,” alisema Kakolaki.
Hadi jana jioni maofisa wa DCEA walikuwa wakifanya upekuzi kwa kusaidiwa na mbwa wanusaji kuona kama kuna mizigo zaidi.
Habari zaidi zinasema baada ya kuona wamezungukwa, raia hao wa Iran walijaribu kubadili mwelekeo, lakini walizidiwa nguvu na kuanza kutupa baadhi ya mizigo kwenye maji ya Bahari ya Hindi.
Kamishna Mkuu wa DCEA, Rodgers Siyanga amesema kiwango hicho cha dawa kingekuwa kikubwa zaidi isingekuwa kitendo cha watu hao kutupa kiasi kingine baharini.
“Nasema vyombo vya dola viko imara kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya na hatutaacha kuyadhibiti magenge na mitandao yao. Kwa hiyo mtu yeyote anayepanga kuingiza dawa za kulevya ni vema ajiulize mara mbili na aache, tutampata tu,” alisema Siyanga.
Meli iliyotumika katika operesheni hiyo ya usiku wa manane ilitumika pia kulivuta jahazi hilo na kulifikisha Bandari ya Dar es Salaam juzi saa nne usiku.
Ofisa mwingine aliyeshiriki operesheni hiyo alisema baada ya kukamatwa raia hao wa Iran walijitetea kuwa wao ni wavuvi. “Tulipowabana wakadai wanakwenda nchini Somalia kusaka chombo cha wenzao walichodai kutaarifiwa kimeharibika huko.”
Imeelezwa pia kuwa Wazanzibari wawili waliokutwa kwenye meli hiyo walijitetea kuwa wao walitumwa tu kupeleka chakula katika jahazi hilo.
Raisi John Magufuli aliwahi kusema Serikali yake haitakuwa na huruma na watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ambazo zimeharibu nguvu kazi ya Taifa kwa kiasi kikubwa.
Akiamuapisha Siyanga mwezi Aprili, Rais Magufuli alisema, ‘isingekuwa sheria imesema, yeye mwenyewe angekuwa mwenyekiti badala ya waziri mkuu’, huku akimtaka Kamishna Siyanga kufanya kazi bila woga.
Rais Magufuli kuwaapisha viongozi wapya walioteuliwa leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Oktoba, 2017 saa 8:00 mchana atawaapisha Makatibu Wakuu wapya, Naibu Makatibu Wakuu wapya na Wakuu wa Mikoa wapya baada ya jana tarehe 26 Oktoba, 2017 kufanya mabadiliko katika safu ya uongozi wa nyadhifa hizo.
Kufuatia mabadiliko hayo safu ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu itakuwa kama ifuatavyo;
Ofisi ya Rais Ikulu.
Katibu Mkuu – Bw. Alphayo Kidata
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Katibu Mkuu (Utumishi) – Dkt. Laurian Ndumbaro
Naibu Katibu Mkuu – Dorothy Mwaluko (ATAAPISHWA)
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Katibu Mkuu – Mhandisi Mussa Iyombe
Naibu Katibu Mkuu(Afya) – Dkt. Zainabu Chaula
Naibu Katibu Mkuu(Elimu) – Bw. Tixon Nzunda
Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Katibu Mkuu – Mhandisi Joseph Kizito Malongo (ATAAPISHWA)
Naibu Katibu Mkuu – Bi. Butamo Kasuka Phillipo (ATAAPISHWA)
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Katibu Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) – Bw. Erick Shitindi
Katibu Mkuu(Bunge na Waziri Mkuu) – Maimuna Tarishi
Katibu Mkuu(Sera na Uratibu) – Prof. Faustine Kamuzora
Wizara ya Kilimo.
Katibu Mkuu – Mhandisi Methew Mtigumwe
Naibu Katibu Mkuu – Dkt. Thomas Didimu Kashililah (ATAAPISHWA)
Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Katibu Mkuu (Mifugo) – Dkt. Maria Mashingo
Katibu Mkuu (Uvuvi) – Dkt. Yohana Budeba
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Katibu Mkuu (Ujenzi) – Mhandisi Joseph Nyamuhanga
Katibu Mkuu (Uchukuzi) – Dkt. Leonard Chamriho
Katibu Mkuu (Mawasiliano) – Dkt. Maria Sassabo
Naibu Katibu Mkuu (Mawasiliano) – Mhandisi Anjelina Madete
Wizara ya Fedha na Mipango.
Katibu Mkuu – Doto James Mgosha
Naibu Katibu Mkuu (Utawala) – Bi. Susana Mkapa (ATAAPISHWA)
Naibu Katibu Mkuu (Fedha za Nje) – Bi. Amina Shaaban
Naibu Katibu Mkuu (Sera) – Dkt. Khatibu Kazungu
Wizara ya Nishati.
Katibu Mkuu – Dkt. Hamis Mwinyimvua
Wizara ya Madini.
Katibu Mkuu – Prof. Simon S. Msanjila (ATAAPISHWA)
Wizara ya Katiba na Sheria.
Katibu Mkuu – Prof. Sifuni Mchome
Naibu Katibu Mkuu – Amon Mpanju
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu – Prof. Adolf F. Mkenda
Naibu Katibu Mkuu – Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Katibu Mkuu – Dkt. Florence Turuka
Naibu Katibu Mkuu – Bi. Immaculate Peter Ngwale
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katibu Mkuu – Meja Jen. Projest Rwegasira
Naibu Katibu Mkuu – Balozi Hassan Simba Yahaya
Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katibu Mkuu – Meja Jen. Gaudence Milanzi
Naibu Katibu Mkuu – Dkt. Aloyce K. Nzuki
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Katibu Mkuu – Dorothy Mwanyika (ATAAPISHWA)
Naibu Katibu Mkuu – Dkt. Moses M. Kusiluka
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Katibu Mkuu – Prof. Elisante Ole Gabriel
Naibu Katibu Mkuu (Viwanda) – Ludovick J. Nduhiye (ATAAPISHWA)
Naibu Katibu Mkuu (Biashara na Uwekezaji) – Prof. Joseph Buchwaishaija (ATAAPISHWA)
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Katibu Mkuu – Dkt. Leonard Akwilapo
Naibu Katibu Mkuu – Prof. James Epiphan Mdoe
Naibu Katibu Mkuu – Dkt. Ave-Maria Semakafu
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Katibu Mkuu (Afya) – Dkt. Mpoki Ulisubisya
Katibu Mkuu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) – Bi. Sihaba Nkinga.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katibu Mkuu – Bi. Suzan Paul Mlawi (ATAAPISHWA)
Naibu Katibu Mkuu – Nicholaus B. William (ATAAPISHWA)
Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Katibu Mkuu – Prof. Kitila Mkumbo
Naibu Katibu Mkuu – Mhandisi Emmanuel Kalobelo
Mhe. Rais Magufuli atawaapisha Wakuu wa Mkoa 6 aliwateua jana kama ifuatavyo;
Mhe. Rais Magufuli atamuapisha Bw. Alexander Pastory Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Kabla ya uteuzi huu Bw. Mnyeti alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Joel Bendera ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli atamuapisha Bw. Joackim Leonard Wangabo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Kabla ya uteuzi huu Bw. Wangabo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu na anachukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Zelote Stephen ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli atamuapisha Bw. Robert Gabriel Luhumbi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Kabla ya uteuzi huu Bw. Luhumbi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe na anachukua nafasi ya Meja Jen. Ezekiel Kyunga ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli atamuapisha Bw. Adam Kigoma Malima kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara. Bw. Adam Kigoma Malima anachukua nafasi ya Dkt. Charles Mlingwa.
Mhe. Rais Magufuli atamuapisha Bi. Christine Solomon Mndeme kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Kabla ya uteuzi huu Bi. Mndeme alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini na anachukua nafasi ya Bw. Jordan Rugimbana.
Mhe. Rais Magufuli atamuapisha Bw. Gelasius Gasper Byakanwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Bw. Byakanwa alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai na anachukua nafasi ya Bi. Halima Dendego.
Tukio la kuapishwa kwa viongozi hawa litarushwa moja kwa moja (Live) kutoka Ikulu Jijini Dar es Salaam kupitia vyombo vya habari vya Redio na Televisheni pamoja na tovuti rasmi ya Ikulu ambayo ni www.ikulu.go.tz
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Oktoba, 2017
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)