Mvua
iliyonyesha usiku wa kuamkia jana, iligeuka kuwa balaa baada ya
kusababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na watu sita kutojulikana
walipo na zaidi ya nyumba kubomoka eneo la Mbezi.
Kama ilivyo kawaida jijini Dar es Salaam, mvua hiyo iliharibu miundombinu ya usafiri ya maeneo kadhaa, ikisababisha baadhi ya barabara kutopitika na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Kasi (Udart) kulazimika kusimamisha shughuli zake.
Udart
imesema jana kuwa ilisitisha huduma kutokana na eneo la Jangwani,
ambako kuna ofisi zake, kujaa maji hivyo kuathiri shughuli zake.
“Tumesitisha
huduma za mabasi yote kutokana na eneo la Jangwani kujaa maji,” alisema
mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Udart, Deus Bugaywa.
Barabara
kadhaa zilikuwa hazipitiki magari na watembeao kwa mguu, huku mitaa
kadhaa ya maeneo ya Jangwani ikiwa imefurika maji na kusababisha wakazi
kukimbilia Barabara ya Kigogo-Mabibo kushuhudia maji hayo, ambayo pia
yalifurika hadi juu ya daraja la Kigogo Mwisho.
Wakazi
wa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam walikumbwa na mshangao
jana alfajiri wakati walipokuta maeneo yao yamefurika maji kutokana na
mvua hiyo iliyonyesha kuanzia juzi jioni na kuendelea usiku kuamika
jana. Baadhi walishuhudia nyumba zao zikibomka na madaraja kukatika.
Mvua
hizo zilisababisha daraja eneo la Mbezi kuvunjika na hivyo basi la
daladala lililokuwa limebeba abiria kutoka Segerea kuelekea Mbezi Mwisho
lilikwama daraja baada ya kuzidiwa na kasi ya maji yaliyofunika daraja
hilo.
Abiria waliokuwa ndani ya daladala hilo waliokolewa wote huku mmoja wao akizimia na kupelekwa hospitali.
Mvua
hiyo pia ilisimamisha shughuli za kijamii, wananchi walishindwa kwenda
kazini wakiwamo wanafunzi ambapo walishindwa kufika shuleni kutokana.
Maji
yalijaa barabarani huku shughuli za usafiri zikisimama , maduka na
vibanda vya biashara vilifungwa na vingine vikisombwa na maji.
Pia
mwenyeki wa Mtaa wa Kiluvya kwa Komba, Julius Mgini alisema watu sita
wanasadikiwa kusombwa na maji eneo hilo akiwamo mtoto mmoja na nyumba za
familia tatu zimebomoka.
“Katika
eneo langu kuna daraja limekatika na watu sita wanasadikiwa kusombwa na
maji. Waliosombwa ni pamoja na mtoto mdogo ambaye bado hatujajua umri
wake,” alisema.
Hata
hivyo, kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Jumanne Muliro alisema bado
wanakusanya taarifa za mafuriko hayo na baadaye kuzipeleka kwa kamanda
wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.
Kamanda Mambosasa pia alisema wanafanya tathimini ili kujua athari za mafuriko.
==> Picha zote na Iman Nsamila
==> Picha zote na Iman Nsamila
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni