Ijumaa, 27 Oktoba 2017

CHADEMA kwenda Mahakamani kumnasua Mkurugenzi wake Polisi


 aada ya Polisi kuendelea kumshikilia Mkurugenzi wa Chadema wa Operesheni na Mafunzo, Kigaila Benson chama hicho kimesema kimekwenda Mahakama Kuu kuiomba itoe amri kwa jeshi hilo kumfikisha kortini.

Wakati Chadema ikisema hayo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jana  Alhamisi Oktoba 26,2017 alisema, “Upelelezi unaendelea na huenda kesho(Ijumaa hii) akafikishwa mahakamani.”

Kigaila anashikiliwa na polisi tangu Jumatatu Oktoba 23,2017 aliporipoti Kituo Kikuu cha Polisi cha kanda hiyo kuitikia wito wa jeshi hilo.

Taarifa ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene iliyotolewa jana Oktoba 26,2017 imesema baada ya kumaliza mahojiano, askari kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), waliokuwa wakimhoji Kigaila walisema hawana mamlaka ya kumwachia kwa dhamana.

Makene alisema sababu waliyoitoa ni kwamba wakubwa na wenye mamlaka ya kuruhusu dhamana au kutoa dhamana hawakuwepo ofisini.

“Juhudi za mawakili waliokuwepo polisi kumpatia Kigaila msaada wa kisheria, kueleza kuwa dhamana ni haki yake kwa mujibu wa sheria, huku wakihoji ni kwa nini kusifanyike mawasiliano ili hao wakubwa watoe ruhusa hiyo hata kama wako nje ya ofisi, hazikufua dafu!” alisema Makene.

Alisema tuhuma alizohojiwa Kigaila zilihusu kauli za uchochezi anazodaiwa kuzitoa Septemba 12,2017 siku chama hicho kilipotoa tamko la maazimio ya kikao cha dharura cha Kamati Kuu iliyoketi kujadili tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa  mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.

Makene alisema kwa kuitikia wito wa Jeshi la Polisi na kwenda mwenyewe kituoni, ni sababu inayojitosheleza kuonyesha kuwa Kigaila ni mwaminifu na anatoa ushirikiano kwa sheria za nchi.

“Bila kumfikisha mahakamani au kumwachia huru, tafsiri yake ni kwamba Kigaila anashikiliwa na jeshi hilo kinyume cha sheria za nchi,” alisema.

Alisema Chadema imeagiza Kurugenzi ya Katiba na Sheria kuratibu na kusimamia hatua za kisheria ili kuhakikisha Kigaila anapata haki zake za msingi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni