Serikali
ya Saudi Arabia imesema itagharamia matibabu nchini humo kutenganisha
pacha walioungana, Anisia na Almesia, wenye umri wa miezi mitano,
yatakayofanyika nchini Saudi Arabia.
Watoto
hao walizaliwa Januari 29, wilayani Misenyi katika Kituo cha Masista
cha St. Theresa Omukajunguti Kata ya Kyaka na kufikishwa Hospitali ya
Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam mapema mwezi Februari, ambako
wamewekwa kwenye wodi maalumu ya jengo la watoto ya Magufuli, wakipatiwa
matibabu ya awali kabla ya kupelekwa Saudia Arabia kwa matibabu.
Watoto hao wa Jonisia wameungana eneo kubwa la kifua na tumbo, lakini kila mmoja ana mfumo wake wa hewa.
Naibu
Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al – Hazani
amesema kuwa watoto hao watafanyiwa upasuaji huo wa kuwatenganisha
katika Hospitali ya Mfalme Abdulaziz Medical iliyopo Riyadh, mji mkuu wa
Saudi Arabia, ambako kuna madaktari bingwa wa upasuaji.
Alisema
mpango huo wa kufanikisha matibabu ya upasuaji wa kuwatenganisha
mapacha hao, unafanywa kwa ushirikiano wa ubalozi wa Saudi Arabia nchini
chini ya balozi wake Mohamed Bin Mansour, uongozi wa Hospitali ya
Muhimbili na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga.
“Mara
tu mipango na maandalizi itakapokamilika, tunatarajia watoto kuondoka
kwenda Riyadh mwishoni mwa mwezi huu," alisema Al-Hazani.
Hospitali
ya Mfalme Abdulaziz Medical huko Riyadh, ina uwezo mkubwa ikiwa na
vifaa vya kisasa na vitanda 1,501 na ilianza shughuli zake Mei 1983.
Tangu wakati huo, imeendelea kupanuka, huku ikitoa huduma kwa idadi ya wagonjwa wanaokua kwa kasi katika maeneo yote.
Mama
wa pacha hao, Jonisia Jovitus (21) alisema tayari watoto wake
wamechukuliwa vipimo mbalimbali na jopo la madaktari wa Hospitali ya
Muhimbili na kuvituma Saudi Arabia.
"Madaktari
wameniambia walishatuma vipimo Saudi Arabia na uwezekano wa watoto
wangu kutenganishwa upo, naomba Mungu asaidie hili lifanikiwe… ila
walichoniambia ni kuwa wanangu wakifanikiwa kutenganishwa salama
watakuwa walemavu, mmoja atakuwa na mguu mmoja na mwingine ana miguu
miwili, lakini huo mmoja hauna nguvu umepooza. Ninachoomba kwa sasa ni
kuwaona watoto wangu wametenganishwa na kuwa salama, naomba jamii
iniombee ili lifanikiwe.”- Jonisia
Uongozi
wa Hospitali wa Muhimbili kupitia kwa Ofisa Uhusiano, Aminiel Eligaesha
ulisema kuwa utaweka wazi kuhusu mchakato mzima wa watoto hao madaktari
watakapokuwa tayari.
Awali,
uongozi huo wa Muhimbili ulikuwa uzungumze na vyombo vya habari juzi,
lakini waliahirisha kwa kile kilichoelezwa kuwa wahusika wamepata
dharura, hivyo vyombo vya habari vitaarifiwa siku itakayoitishwa upya
mkutano huo.
Credit: Habarileo