Jumatatu, 11 Juni 2018

BAWACHA Wamtaka Mwigulu Nchemba Ajiuzulu

Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) limelaani vikali kitendo cha udhalilishaji kilichofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya Amina Mapunda aliyejifungua kituo cha polisi bila msaada wowote baada ya kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu ilhali akiwa mjamzito.

Vilevile, baraza hilo limemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba kujiuzulu nafasi yake kutokana na mfululizo wa matukio ya polisi kunyanyasa wananchi.

Mbali na Mwigulu, Bawacha imetaka pia naibu wa Mwigulu, Hamad Yussuf Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kuachia nafasi zao pia.

Amina (26), mkazi wa Kiswanya, Kijiji cha Mgundeni, Tarafa ya Mang'ula wilayani Kilombero mkoani Morogoro, alijifungua nje ya kituo cha polisi Mang'ula muda mfupi baada ya kutolewa mahabusu baada ya kulalama kwa muda mrefu kuumwa uchungu wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Masauni, mama huyo alikamatwa na polisi kutokana na tuhuma za mumewe kuuziwa vitu vya wizi vilivyokutwa ndani ya nyumba yao.

Wakati serikali ikiendelea na uchunguzi dhidi ya askari waliohusika na mkasa huo, uongozi wa Bawacha umesema kitendo cha mwanamke huyo kujifungulia nje ya kituo cha polisi bila msaada wowote "ni cha kinyama" na kinatoa picha mbaya kwa Jeshi la Polisi kwamba linafanya kazi yake bila kuzingatia weledi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Katibu Mkuu wa Bawacha Taifa, Grace Tendega, alisema baraza hilo linalaani kitendo hicho na viongozi ndani ya Jeshi la Polisi wanatakiwa kujipima na kujitafakari kama kweli wanatosha.

Alisema kitendo cha jeshi hilo kusababisha mwanamke huyo kujifungua kwenye mchanga hakimdhalilishi yeye peke yake, bali kinawadhalilisha kina mama wengi wa Kitanzania na ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

"Hapa unaweza kujiuliza mama anahusikaje na wizi wa mume wake? Hata kama kweli waliona kuna vifaa vya wizi, kwanini hawakuchukua vifaa hivyo kama ushahidi?" Alihoji.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) pia, Tendega alisema zaidi: "Lakini inashangaza hao polisi hawakuona kama huyo mama ni mjamzito au hawajui mtu ambaye ni mjamzito? Haya ni mambo ya ajabu sana kwa Jeshi la Polisi."

Alisema kitendo hicho ni kibaya na kuna kila sababu ya viongozi wa Jeshi la Polisi kuanzia ngazi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kilombero, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Jeshi la Polisi Taifa (IGP) pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na naibu wake kujitafakari na kujipima kama kweli wanastahili kuendelea na kazi.

Alisema matukio ya aina hiyo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na Jeshi la Polisi limekuwa likikaa bila kuonyesha juhudi yoyote ya kuwachukulia hatua wanaohusika na ukiukwaji huo wa haki za binadamu kwa kuwatesa wananchi au kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji.

Tendega alisema pamoja na kuwapo kwa vitisho mbalimbali, Chadema na Bawacha hawatanyamaza na badala yake watapaza sauti kwa ajili ya kuwatetea wanyonge na kudai haki bila kuwa na uoga.

==

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni