Jumatatu, 11 Juni 2018

Spika Ndugai Akerwa na Gawio Kiduchu la Benki ya NBC Kwa Serikali

Sika wa Bunge, Job Ndugai, ameitaka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kutoa maelezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) kuhusu kiasi kidogo cha gawio wanachokitoa kwa Serikali. Kwa mwaka 2016-2017 ilitoa Sh bilioni 1.2.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati akifungua semina kwa wajumbe wa PIC na baadhi ya wajumbe wa kamati nyingine ikiwamo bajeti, uongozi wa NBC na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Pamoja na mambo mengine, Ndugai alisema kwa hisa ya asilimia 30 ambazo Serikali inazo kwa benki hiyo, gawio hilo ni kidogo sana na linatia shaka.

“Hisa zenu hazitofautiani sana na za Serikali zilizopo Benki ya NMB, lakini wenzenu wamekuwa wakitoa gawio kubwa kuliko ninyi, hapa mna kazi kubwa ya kuishawishi kamati ili iweze kukubaliana na majibu yenu juu ya kiasi hicho cha gawio.

“Inadhihirisha wazi kwamba hakuna urafiki na wananchi kutokana na kutokuwa karibu nao kwa kushindwa kufungua matawi wala kutoa mikopo kwa wananchi kama zinavyofanya NMB na CRDB,” alisema.

Aliutaka uongozi huo wa NBC kulitafakari hilo na kulifanyia kazi ili benki hiyo iwe karibu na wananchi.

“PIC imepewa jukumu la kuangalia mashirika yote na kuona utendaji kazi wao kwa sababu kuna takribani mashirika 272 ambayo ni muhimu na itasaidia Serikali kujua nini kinaendelea kabla ya kuingia mikataba na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwepo,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Raphael Chegeni, aliitaka NBC kuacha kulala na kuanza kufanya kazi kwa ufanisi na Serikali.

Kuhusu agizo hilo la Spika, Chegeni alimwomba kwa kuwa Bunge linaendelea, awape nafasi ili wakutane na taasisi hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa NBC, Theobald Sabi, alisema watapata nafasi ya kuzungumza na kamati kuwaeleza juu ya mwenendo wa benki, mafanikio na changamoto mbalimbali ambazo inazipitia.

Kuhusu gawio, alisema hivi sasa wanasonga mbele wakiendelea kuikuza benki hiyo na mwaka 2000 ilikuwa na jumla ya mtaji wa Sh bilioni 326, lakini sasa mtaji ni Sh trilioni moja.

Alisema hayo ni mafanikio na watajitahidi kusonga mbele na mwaka 2017 walilipa gawio kwa Serikali Sh bilioni 1.2 na wanategemea wamiliki wa benki watafanya uamuzi juu ya ulipaji wa gawio miaka ijayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni