Dar/ Nairobi. Ukanda wa hifadhi za Taifa za Serengeti na Maasai Mara
nchini Kenya ambao una mojawapo kati ya maajabu manane ya dunia
yanayovutia watalii, unakumbwa na tishio la kimazingira kutokana na nchi
hizo mbili kuingia katika mgogoro wa kugombania maji.
Ajabu lililopo baina ya hifadhi hizo ni lile la kuhama kwa wanyama waitwao nyumbu.
Mvutano huo mpya unaibua mgogoro kati ya nchi hizo jirani ambazo ni vigogo ndani ya Jumuiya Afrika Mashariki (EAC).
Mgogoro huo unatokana na uamuzi wa Serikali ya Kenya kujenga mabwawa
mawili katika Mto Mara ambayo wataalamu wanaonya kuwa yatakausha ukanda
huo na kuathiri uzao wa ndege katika Ziwa Natron, huku Tanzania ikipanga
kuvuna maji katika mto huo na kuufanya usitiririshe ipasavyo maji yake
katika Ziwa Victoria.
Kenya inatarajia mradi huo utasaidia kumwagilia mashamba karibu na
chanzo cha mto huo katika Msitu wa Mau na kumaliza tatizo la maji kwa
wakazi wa maeneo hayo. Hata hivyo, wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa
hatua hiyo itaathiri zaidi upatikanaji wa maji ukanda mzima hasa mwisho
wa mto huo na madhara hayo kuathiri hadi Tanzania.
Mto Mara ni maarufu duniani kutokana na wanyama hao kuuvuka hususan
uhamaji wao wa kila mwaka kutoka upande mmoja wa nchi kwenda mwingine.
Kati ya Julai na Septemba kila mwaka, idadi kubwa ya nyumbu huwasili
katika kingo za mto huo na hujikusanya kwa muda katika eneo hilo na
baadaye huanza safari ya kuhamia upande wa pili kwa kuchagua sehemu moja
ya kuvukia katika mto huo.
Kitendo cha wanyama hao kuhama kila mwaka kwa kujikusanya kwa pamoja na
kujitupa kwenye mto wenye mamba lukuki ili kuvuka upande wa pili,
kimelifanya tukio hilo kuwa ni moja ya maajabu manane yaliyopo duniani.
Inakadiriwa kuwa nyumbu takriban milioni 1.5 wakisindikizwa na kundi
kubwa la pundamilia, pofu, swala na digidigi huhama kila mwaka kutoka
Serengeti Tanzania na kwenda Hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya katika
jitihada za kutafuta chakula.
Asili ya mvutano huo wa maji upo katika mpango kazi wa mwaka 2002 wa
Kenya unaopanga kuhamisha kiwango kikubwa cha maji kutoka Mto Emala
kwenda Ewaso Ngiro katika eneo la chanzo cha maji cha Bonde la Ufa.
Ripoti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Maji ya Mpango wa Uhamishaji wa Maji,
Bonde la Mto Mara ya Kenya (2017-2022) inaeleza kuwa umwagiliaji
utakunywa kiasi kikubwa cha maji kutokana na kutumia kati ya asilimia 70
hadi 80 ya maji yote. Jambo hilo limewavuta wanamazingira wa Tanzania
walioeleza ujenzi huo wa mabwawa Kenya utasababisha madhara makubwa
katika mazingira ya Serengeti, huku wakitanabaisha kwamba asilimia 75 ya
ndege aina ya flamingo wadogo huzaliwa maeneo ya Ziwa Natron.
Hata hivyo, kaimu mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya maji yanayohusu
nchi mbili wa Kenya, Gladys Wekesa anasema hadi sasa ujenzi wa mabwawa
hayo haujaanza na hawana mpango wa kuhamisha maji yote kutoka Mto Mara
na kwamba, mradi huo unafanywa kwa kuzingatia masilahi ya pande zote
mbili.
Wekesa alisema Bwawa la Amala ni sehemu ya mpango wa uendelezaji
rasilimali maji wakati lile la Norera linalotarajiwa kuendesha mradi
mdogo wa umeme wa kilowati 90 litakuwa na ukubwa wa mita za ujazo
450,000.
Alisema mradi huo ulipangwa na kukubaliwa na pande zote mbili lakini anashangaa kuona maofisa wa Tanzania wanageuka.
Hata hivyo, Bakari Mnaya na Mtango Mtahiko wa Mamlaka za Hifadhi za
Taifa (Tanapa) pamoja na Profesa Eric Wolanski wa Chuo Kikuu cha James
Cook cha Australia wanasema katika ripoti yao kuwa, kutokana na kiwango
cha maji kilichopo mahitaji ya sasa yanaweza kutimizwa bila kuharibu
hifadhi ya maji.
Katika ripoti hiyo wanaeleza kuwa hakuna uhakika kuwa maji yaliyopo
yatatimiza mahitaji ya baadaye hususan kipindi cha kiangazi kikali iwapo
nchi zitaendelea kuendeleza miradi mikubwa inayotumia maji mengi.