Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeitoza faini ya Sh100 milioni
kampuni ya Star Media kwa kuwatoza fedha watazamaji wa chaneli
zinazotakiwa kuonekana bila kulipiwa kupitia king’amuzi cha Star Times.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mkuu
wa TCRA, James Kilaba alisema kitendo hicho ni kinyume cha kanuni ya
14(2) (a) ya kanuni za Digital and Broadicasting Networks za mwaka 2011.
“TCRA inaendelea kufuatilia kuhakikisha kuwa ving’amuzi vya Star Times,
Continental, Digitek na Ting vinaendelea kuonyesha chaneli zote za
kitaifa za FTA (Free to Air) bure kwa mujibu wa sheria,” alisema Kilaba.
Chaneli zinazotakiwa kuonekana bila kulipiwa ni TBC1, ITV, EATV, Channel
Ten, Star TV na Clouds TV. Kampuni hiyo imetozwa faini kuanzia Desemba
22 na inatakiwa kuwa imelipa kabla ya Januari 30.
Akizungumzia uamuzi huo, mkazi wa jijini Mwanza, Pius Rugonzibwa
alipongeza akisema wamekuwa wakipata usumbufu kwa kukatiwa huduma.
Gharama mpya za mtandao
Mbali ya adhabu hiyo kwa Star Media, Kilaba pia alitangaza viwango vipya
vya gharama za mwingiliano baina ya mitandao inayotoa huduma za
mawasiliano ya simu nchini vitakavyoanza kutumika Januari Mosi baada ya
vinavyotumika sasa kufikia kikomo Desemba 31.
Alisema kampuni za simu zimekuwa na kigugumizi kukubaliana kuhusu
viwango hivyo na kuingia mikataba ya mwingiliano kwa sababu ya masilahi
ya kibiashara hivyo TCRA ililazimika kuingilia kati na kuvipanga kwa
kufuata utaratibu kama ilivyoainishwa katika sheria namba 12 ya
kuanzishwa kwake mwaka 2003.
Alisema kampuni hizo hulipana kufidia ya gharama ya kupokea simu
inayotoka mtandao mwingine na kuifikisha kwa mteja aliye ndani ya
mtandao unaopigwa.
Kilaba alisema TCRA iliweka viwango kwa mtiririko wa kipindi cha miaka mitano kinachoishia Desemba 31.
Gharama za mwingiliano zitakazotozwa kwa dakika na mwaka kwenye mabano
ni Sh15.60 (Januari Mosi, 2018), Sh10.40 (2019), Sh5.20 (2020), Sh2.60
(2021) na Sh2.00 (2022).
Alisema viwango hivyo vimepungua kulinganisha na miaka mitano iliyopita
ambayo gharama zake za mwingiliano zilizokuwa zikitozwa kwa dakika na
mwaka wake kwenye mabano ilikuwa Sh34.92 (2013), Sh32.40 (2014), 30.58
(2015), Sh28.57 (2016) na Sh26.96 (2017).
“Kupungua kwa gharama hizi kutawezesha na kuongeza ufanisi katika
shughuli za sekta zingine kiuchumi na kijamii, pia kutaongeza mapato ya
watoa huduma na Serikali kutokana na ongezeko la matumizi ya huduma za
mawasiliano,” alisema.
Alisema kwa sasa simu za mezani ni 127,976 na watumiaji wa simu za
kiganjani imeongezeka kutoka laini 2,963,737 mwaka 2005 hadi kufikia
laini 40,002,364, Septemba.
Alisema mpaka kufikia Septemba, watumiaji wa huduma wamefikia 21,611,855.
Source: Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni