Jumanne, 5 Desemba 2017

Leo ni siku ya kimataifa ya kujitolea ambayo kila mwaka huwa Desemba 5, kauli mbiu mwaka huu ni "jitolee chukua hatua kwanza"




Leo ni siku ya kimataifa ya kujitolea ambayo kila mwaka huwa Desemba 5, kauli mbiu mwaka huu ni "jitolee chukua hatua kwanza"
Ni kijana Hussain Salim mratibu wa miradi na matukio kutoka Rally Tanzania Society, taasisi isiyo ya kiserikali inayohusika na shughuli za kujitolea na inafanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa nchini humo katika kusongesha mbele malengo ya maendeleo endelevu SDGs.
Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya wafanyakazi wake wa kujitolea kama kijana Hussein wana mchango mkubwa, katika kusaidia kufanikisha ajenda ya umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu ya 2030 lakini pia malengo ya jamii wanakojitolea. Hussein ana ujumbe




Hapa ni nchini Sudan Kusini, Solomon Ayiko (kulia) mfanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa akiwa kwenye doria na walinda amani kwenye njia inayotumiwa na wanawake kusaka kuni, eneo ambalo ni hatari zaidi kwa ukatili wa kingono na kijinsia.Pichani mkimbizi wa ndani akiwa amemshikilia Solomon ili asiteleze wanapopita kwenye njia hii yenye maji na madimbwi. (Picha:UNV/(Melanie Moore/ 2016)
Mbali ya mazingira wafanyakazi wa kujitolea wanashiriki katika masuala mengine kadha wa kadha. Sudan kwa mfano kuna wafanyakazi zaidi ya 200 wa kimataifa na kitaifa wanaojitolea kwenye mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kulinda amani Darfur UNAMID, na baadhi ya shughuli wanazofanya ni kujenga barabara, kuwawezesha vijana, kuchagiza masuala ya haki za binadamu, kulinda watoto na kuchangia katika juhudi za kuleta amani na maendeleo .
Kwa mujibu wa Stuart J. Moran meneja wa mpango wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa Darfur bila mchango wao kibarua kingekuwa kigumu

Idara ya Maendeleo ya Jamii yaendesha mafunzo ya udhibiti wa viashiria hatarishi sehemu za kazi


 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) imeendesha mafunzo kuhusu Mfumo wa Udhibiti wa Viashiria Hatarishi Mahali pa Kazi yanayofanyika Ukumbi wa VETA mkoani Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu wa Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii, Jinsia Wazee na Watoto Bw. Maercel Katemba akifungua Mafunzo ya Mfumo wa Udhibiti wa Viashiria Hatarishi Mahala pa Kazi kwa watumishi wa Idara Kuu Maendeleo ya Jamii yanayofanyika katika katika Ukumbi wa VETA mkoani Dodoma.
Mafunzo haya ya siku nne yanajumuisha wakuu wa Idara, wakuu wa vitengo, wakurugenzi wasaidi na wasimamizi wa udhibiti wa vihatarishi katika sehemu ya kazi.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii- Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Bw. Marcel Katemba amesema kuwa suala la udhibiti wa viashiria hatarishi linatokana na matakwa ya Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 (2010) na Waraka wa Hazina namba 12 wa 2012/2013 unaoitaka kila Taasisi ya Umma kuzingatia uandaaji na utekelezaji wa Mfumo wa Menejimenti ya Viashiria vya Vihatarishi mahala pa kazi.
“Mafunzo haya ni nyenzo ya utumishi wa umma katika kudhibiti wa mifumo ya ndani ya Taasisi na hivyo kuleta ufanisi katika shughuli na utendaji wa kazi za kila siku na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kiutendaji na za fedha zenye kuaminika” alisema Bw. Katemba.
Kaimu Katibu Mkuu Bw. Marcel Katemba amewakumbusha washiriki kuwa, mafunzo hayo ni mwendelezo wa yale yaliyofanyika mwezi Julai, 2016, hivyo ni jukumu la pamoja kati ya Menejimenti na watumishi wote wa Idara kuu ya Mendeleo ya Jamii kwa ujumla wao kusimamia kikamilifu Viashiria Hatarishi katika Idara na Vitengo husika.
Ameongeza kuwa muendelezo huo utawaongezea uwezo watendaji, kuwa na uelewa wa pamoja wa kutosha kuhusu viashiria vilivyo katika maeneo ya kazi.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mratibu Bw. Dickson Rusage amesema kuwa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni miongoni mwa Wizara tano (5) kati ya Wizara 21 za Serikali ambazo zimeweza kuanzisha mfumo wa udhibiti wa viashiria hatarishi mahala pa kazi na kuutekeleza.
Ameongeza kuwa Idara kuu ya Mendeleo ya Jamii imepiga hatua zaidi kwa kuwatumia wataalam wake wa ndani katika kutoa mafunzo ya uelewa na kusimamia udhibiti wa vihatarishi.
Bw. Rusage amebainisha kuwa changamoto zilizopo katika kuendesha mfumo huo ni pamoja na ukosefu wa rasilimali fedha, mfumo kutopewa kipaumbele, kutokuwepo dhamira ya dhati katika matumizi ya mfumo, kutozingatia mfumo katika kufikia malengo ya Wizara, Idara, na Taasisi husika.
Kwa upande wake Mwezeshaji katika Mafunzo hayo Bw. Moris Jackson amesema kuwa manufaa ya mfumo wa udhibiti wa viashiria mahala pa kazi ni kuwa Wizara inayokuwa na mfumo huu, wabia wa maendeleo wataiamini Taasisi kwamba rasilimali zinazotolewa zitakuwa salama maana viashiria vinafahamika na vimewekewa mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti kwa manufaa mapema.
Mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na Maana na makundi, Faida na Kanuni za Usimamizi wa Viashiria vya Vihatarishi, Matakwa ya kisheria kuhusu Usimamizi wa Vihatarishi nchini, Muundo na maeneo muhimu ya kimwongozo, Mgawanyo wa majukumu katika Usimamizi wa Vihatarishi na nyaraka mbalimbali zitakazotumika wakati wa kuandaa na kusimamia Vihatarishi.
Mategemeo ya mafunzo hayo ya mahala pa kazi yanalenga washiriki kuweza kubaini vihatarishi ambavyo viliwekwa mwaka jana na sasa havitakiwi kuwepo tena, kubaini vihatarishi vipya ambavyo ama vilisahaulika au vitaibuliwa sasa kutokana na shughuli na kazi za Idara na Vitengo hasa baada ya mwaka kuisha na kupata maoni na ushirikiano wa kutosha ili kwa pamoja kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kudhibiti viahatarisi kazini.

Mwanafunzi Aliyesambaza Picha za Nyufa Hostel za UDSM Atiwa Mbaroni



 Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kumbusho Dawson anashikiliwa na polisi akituhumiwa kusambaza picha kuonyesha nyufa kwenye majengo ya hosteli.


Dawson ambaye ni mbunge wa serikali ya wanafunzi (Daruso) alikamatwa jana Jumatatu Desemba 4,2017 mchana.

Makamu wa Rais wa Daruso, Anastazia Anthony amethibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo jana saa saba mchana.

"Ni kweli Kumbusho alikamatwa jana mchana  na kupelekwa kituo cha polisi cha Chuo Kikuu kwa ajili ya kuhojiwa lakini ilipofika saa tisa alasiri polisi walisema hawana uwezo wa kumuhoji hapa hivyo wakampeleka Oysterbay," amesema Anastazia.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipotafutwa amesema hana taarifa kuhusu tukio hilo. Alisema anasubiri atakapofikishiwa taarifa atazitoa kwa umma.

Godbless Lema, Jerry Muro Wazidisha Utata Safari Ya Mnyika Kuhamia CCM



 Licha ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kukaririw jana kikikanusha fununu zilizozagaa mitandaoni zikielekeza kuwa Mbunge wa Kibamba (Chadema), Mhe. John Mnyika anatazamiwa kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), bado ishara zimezidi kuonesha kuwa safari ya kinara huyo wa upinzani kuelekea CCM imezidi kuiva.

Tetesi hizo zimegonga vichwa vya mitandao ya kijamii jana jioni  baada ya kada wa CCM, Jerry Muro kutumia mtandao wa kijamii wa Instagram kwa kuweka picha ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na John Mnyika na kuandika maneno kadhaa kama ifuatavyo;

“Wanakuita mvulana, basi nenda kwa Baba ukadeke kidogo kule ulikua unakomazwa tu, #safarimojamatata.”






Wakati wengi wakitafakari maneno ya Jerry Muro, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) naye ametumia mtandao wa kijamii kuandika machache yaliyotafsiriwa kama maneno yanayoongelea sakata la Mnyika kutimkia CCM. 
==>Lema ameandika yafuatayo;
.

MAGAZETI YA LEO 5/12/2017



















Jumatatu, 4 Desemba 2017

Mo Dewji ashinda zabuni ya uwekezaji ndani ya Simba SC



 Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji amepita katika mchakato wa kumtafuta muwekezaji wa klabu ya Simba na ofa yake ya Tsh bilioni 20.

 


Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji amepita katika mchakato wa kumtafuta muwekezaji wa klabu ya Simba na ofa yake ya Tsh bilioni 20.

Dewji ambaye amejitokeza na kuwa muwekezaji pekee ambaye aliweka dau kubwa la Tsh bilioni 20 kupata hisa kwa asilimia 51 ndani ya klabu hiyo amekubaliwa kwa dau hilo kwa kupata hisa 49.
Mwenyekiti wa kamati ya mchakato huo wa mabadiliko, Jaji Mihayo amesema, Mo Dewji amepita na kitachofuatia ni majadiliano mengine baada ya mkutano wa leo.
“Mohammed Dewji ndiye mshindi, maana katika kamati yetu. Hivyo yeye ndiye amekuwa mshindi wa kuwania kuwekeza katika klabu ya Simba. Baada ya mkutano huu kutakuwa na majadiliano,” amesema Jaji Mihayo.Tazama video la tukio hilo hapa chini



Makamu wa Rais aongoza siku ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu duniani (+Picha)



Leo ni siku ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu Duniani na ambapo Kitaifa siku hii inaadhimishwa mkoa wa Kusini Unguja. Ambapo mgeni rasmi ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Makamu wa Rais akipata maelezo kutoka kwa kikundi cha Walemavu kutoka Mwembe Makumbi kinachojishughulisha na kutengeneza viatu wakati alipotembelea maonyesho ya walemavu katika uwanja wa Skuli ya Uzini.









Kauli Mbiu ya siku hii ni “Mabadiliko kuelekea jamii jumuishi na maendeleo endelevu kwa wote.”

Jumamosi, 2 Desemba 2017

Watanzania milioni 1.4 wanaishi na virusi vya Ukimwi



Tafiti inaonyesha kuwa watu wazima na watoto wa rika zote wapatao milioni 1.4 wanaishi na virusi vya Ukimwi nchini Tanzania ambao ni sawa na asilimia 2.9 ya watu wote bila kujali umri wao.


Matokeo hayo yanatokana na utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS) ya mwaka 2016/2017 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambao unaonyesha kiwango cha virusi vya Ukimwi nchini kwa watu wazima wenye umri wa miaka 15-49 hii ni asilimia 4.7 wanaishi na VVU.
Utafiti huo uliofanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na kuhusisha Kaya 14,811 zinaonyesha kuwa vijana walio kwenye umri huo (15-24) wengi wao wakiwa wasichana wanapata maambukizi mapya.
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15-19 ni asilimia 0.7 ambapo asilimia 1.0 ni watoto wa kike na asilimia 0.4 ni watoto wa kiume.
Kwa vijana wenye umri wa miaka 20-24 kiwango hicho kimeongezeka na kuwa asilimia 2.2 wasichana wakiwa ni asilimia 3.4 na wanaume ni asilimia 0.9.
Kwa upande wake Mama Samia alisema, “naomba wasichana wabadilike Ukimwi ukikutesa hautakutesa peke yako bali Taifa zima, takwimu hizi zinaonyesha hali si nzuri kwa kundi hili ambalo ndio nguvu kazi ya Taifa, mjitahidi muwe na mienendo inayoeleweka.”

SportPesa waidhamini timu ya Bunge Mashindano ya Bunge Afrika Mashariki






Kampuni ya michezo ya kubashiri ijulikanayo kama SportPesa Limited imeidhamini timu ya mpira wa miguu na kikapu ya Bunge la Tanzania ambao wanatarajia kushiriki mashindano ya wabunge wa Afrika Mashariki mnamno Desemba 3, 2017 katika uwanja wa Taifa, Temeke Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za SportPesa zilizopo Masaki, Peninsula House Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji SportPesa Tanzania Mr. Tarimba Abbas alisema “Tulivyosikia kuwa haya mashindano ya wabunge wa Afrika Mashariki kwa mwaka huu yatafanyika nchini kwetu tuliona ni vyema kuwa wazalendo kwa kuidhamini timu ya mpira wa miguu na pete kwa kutoa vifaa mbalimbali vya michezo kama Jersey, bibs, soksi, pamoja na mipira. SportPesa ni kampuni ya kubashiri michezo mbalimbali ikiwa na kengo kuu la kukuza na kuendeleza sekta ya michezo nchini na ndiyo maana tulianza kwa kudhamini timu za mpira wa miguu za Simba, Yanga na Singida United.
“Mbali na hapo tutatoa tracksuits kwa ajili ya wabunge wote 160 wanaoshiriki katika mashindano hayo siku ya ufunguzi ambapo wabunge hao watafanya maandamano kutoka ukumbi wa PTA SABASABA kuelekea Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuanza michezo mbalimbali ya ufunguzi.”
“Tunapenda kuwapongeza na kuwatakia kila lakheri timu ya Bunge la Tanzania katika mashindano haya na tunaamini wataiwakilisha vizuri nchi yetu” alimaliza Mr. Tarimba


Naye Mwenyekiti wa klabu ya michezo ya wabunge Mh. William Ngeleja alianza kwa kusema “tunapenda kutanguliza shukrani zetu za dhati kwa kampuni ya michezo ya kubashiri SportPesa kwa ushirikiano wao waliouonyesha na kutusapoti katika kuhakikisha timu zetu za mipira wa miguu na pete zinapata vifaa vya michezo kama vile jezi, mipira na soksi.
“Tunatarajia kuanza rasmi mashindano yetu siku ya jumapili tarehe 03, desemba 2017 ambapo kutakuwa na shughuli mbalimbali za ufunguzi huo ikiwemo kukimbia, kuvuta kamba, mpira wa pete, mpira wa wavu pamoja ja mpira wa miguu”.






Yanga yampa wakati mgumu Ngoma



 YANGA imemuwekea ngumu straika wake Donald Ngoma kwanza kuendelea na kazi yake ya kuitumikia timu hiyo, pia mpango wa kwenda Singida United anakotakiwa na Kocha Hans van Der Pluijm.

Klabu hiyo imesema inamsubiri Kocha wao George Lwandamina arejee kutoka mapumzikoni Zambia, ndipo waamue hatima ya Ngoma aliyepitisha muda alioomba kuwa nje ya timu.

Ngoma hivi karibuni aliaga kwenda kwao Zimbabwe lakini alipitisha muda wa kuwa huo bila kutoa taarifa kwa uongozi, hivyo mabosi wake wanasubiri kukaa kikao cha pamoja na kocha ili kujua hatima yake.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Katibu wa Yanga, Charles Mkwasa amesema hawawezi kumtoa Ngoma kumpeleka Singida United kwani bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na timu yao.

“Ngoma bado ni mali yetu na kwa sasa tunataka kukaa naye kuzungumza naye tangu alipoondoka nchini na kwenda kwao Zimbabe kwa ajili ya kupata tiba ya majeraha yake.

“Mshambuliaji huyu bado ana mkataba wa mwaka na nusu hapa hivyo inakua ngumu kumuachia, tunataka amalize mkataba wake uliobakia,” alisema Mkwasa.

Akizungumzia kuhusu hatima ya Ngoma kikosini, Mkwasa alisema; “Inabidi tukae uongozi na kocha ili kujua tunamchukulia hatua gani Ngoma kwani alipitisha muda aliopewa kuwa nje ya timu bila maelezo, tutasikiliza kile anachosema sasa na tutapima kuhusu hatua za kumchukulia.”

Steve Nyerere amjia juu Polepole kuhusu Wema Sepetu



 HABARI inayobamba mitandaoni na kwenye vyombo vya ahabri kuanzia jana jioni ni kuhusu Malkia wa Filamu Bongo, Wema Sepetu kuhama Chadema na kutangaza kurudi kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo uamuzi huo umetolewa ufafanuzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole akisema CCM haina taarifa za Wema kwani hajafuata taratibu kuanzia kwenye shina la chama na si kupitia mitandaoni.

“Chama chetu sio Daladala mtu anaweza kupanda na kushuka wakati wowote, ni heri akabaki hukohuko ama akaanzie kule ambako alichukulia kadi yetu,” aliandika Polepole.

Kauli hiyo imemuibua Staa wa Filamu aliyekuwa rafiki wa karibu wa Wema kabla hajahamia Chadema, Steve Nyerere ambaye amemtolea povu Polepole na kuijibu kauli yake hiyo akiandika;
“Hiki chama hujakiunda wewe wala kukianzisha wewe, umekikuta kama tulivyokikuta wote, kina waasisi wenye uchungu nacho na wako kimya.

“Wewe ni nani ukatishe watu moyo kukitumikia kama vile ndio unakimiliki, tulia polepole chama cha wote hiki, usilete ubinafsi kwenye kutumikia na kujenga ngome, hatuhitaji wenye cement na nondo tu, acha hata mwenye jiwe lake aweke kikubwa nyumba isimame, ni mchango pia” – aliandika Steve Nyerere.

 

Hizi ndio sababu za CCM kumkataa Wema



 Chama cha Mapinduzi CCM kimeweka wazi sababu iliyowafanya wakatae kumpokea msanii Wema Sepetu kwenye chama hicho, ambaye hapo jana ametangaza kurudi kundini.

Akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, kwanza amekanusha kumpokea mwanachama huyo na kusema kwamba, hakufuata utaratibu sahihi kuweza kurejea kwenye chama hicho ambacho alikiasi.

Pole Pole ameendelea kwa kusema kwamba CCM inajidhatiti katika kujijengea misingi imara na wanachama wake, hivyo wanataka mtu ambaye anaenda CCM awe amejidhatiti.

Pamoja na hayo Polepole amekanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni kwamba msanii huyo ameshawishiwa kurudi CCM baada ya kuahidiwa atasaidiwa kumaliza kesi yake inayomkabili mahakamamni, pamoja na kunusuru kubomolewa kwa nyumba yao.

Wema Sepetu ajivua uanachama Chadema, Atangaza kurudi CCM



 Muigizaji wa filamu za kibongo na Miss Tanzania 2006 Wema Sepetu ametangaza rasmi kurudi Chama Cha Mapinduzi huku akidai kwamba hawezi kuishi kwenye nyumba inayomkosesha amani.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Wema Sepetu amesema kwamba anatangaza rasmi kuondoka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ambacho alitangaza kujiunga nacho Februari mwaka huu.

"Siwezi Kuendelea kuishi kwenye nyumba inayo nikosesha amani... Peace of mind is everything for me. Natangaza rasmi kuondoka Chadema na kurudi nyumbani" . Wema Sepetu.