
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) imeendesha mafunzo
kuhusu Mfumo wa Udhibiti wa Viashiria Hatarishi Mahali pa Kazi
yanayofanyika Ukumbi wa VETA mkoani Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu wa Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii, Jinsia
Wazee na Watoto Bw. Maercel Katemba akifungua Mafunzo ya Mfumo wa
Udhibiti wa Viashiria Hatarishi Mahala pa Kazi kwa watumishi wa Idara
Kuu Maendeleo ya Jamii yanayofanyika katika katika Ukumbi wa VETA mkoani
Dodoma.
Mafunzo haya ya siku nne yanajumuisha wakuu wa Idara, wakuu wa
vitengo, wakurugenzi wasaidi na wasimamizi wa udhibiti wa vihatarishi
katika sehemu ya kazi.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Maendeleo
ya Jamii- Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Bw. Marcel Katemba amesema
kuwa suala la udhibiti wa viashiria hatarishi linatokana na matakwa ya
Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 (2010) na Waraka wa Hazina namba
12 wa 2012/2013 unaoitaka kila Taasisi ya Umma kuzingatia uandaaji na
utekelezaji wa Mfumo wa Menejimenti ya Viashiria vya Vihatarishi mahala
pa kazi.
“Mafunzo haya ni nyenzo ya utumishi wa umma katika kudhibiti wa
mifumo ya ndani ya Taasisi na hivyo kuleta ufanisi katika shughuli na
utendaji wa kazi za kila siku na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za
kiutendaji na za fedha zenye kuaminika” alisema Bw. Katemba.
Kaimu Katibu Mkuu Bw. Marcel Katemba amewakumbusha washiriki kuwa,
mafunzo hayo ni mwendelezo wa yale yaliyofanyika mwezi Julai, 2016,
hivyo ni jukumu la pamoja kati ya Menejimenti na watumishi wote wa Idara
kuu ya Mendeleo ya Jamii kwa ujumla wao kusimamia kikamilifu Viashiria
Hatarishi katika Idara na Vitengo husika.
Ameongeza kuwa muendelezo huo utawaongezea uwezo watendaji, kuwa na
uelewa wa pamoja wa kutosha kuhusu viashiria vilivyo katika maeneo ya
kazi.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mratibu Bw. Dickson Rusage amesema
kuwa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni
miongoni mwa Wizara tano (5) kati ya Wizara 21 za Serikali ambazo
zimeweza kuanzisha mfumo wa udhibiti wa viashiria hatarishi mahala pa
kazi na kuutekeleza.
Ameongeza kuwa Idara kuu ya Mendeleo ya Jamii imepiga hatua zaidi kwa
kuwatumia wataalam wake wa ndani katika kutoa mafunzo ya uelewa na
kusimamia udhibiti wa vihatarishi.
Bw. Rusage amebainisha kuwa changamoto zilizopo katika kuendesha
mfumo huo ni pamoja na ukosefu wa rasilimali fedha, mfumo kutopewa
kipaumbele, kutokuwepo dhamira ya dhati katika matumizi ya mfumo,
kutozingatia mfumo katika kufikia malengo ya Wizara, Idara, na Taasisi
husika.
Kwa upande wake Mwezeshaji katika Mafunzo hayo Bw. Moris Jackson
amesema kuwa manufaa ya mfumo wa udhibiti wa viashiria mahala pa kazi ni
kuwa Wizara inayokuwa na mfumo huu, wabia wa maendeleo wataiamini
Taasisi kwamba rasilimali zinazotolewa zitakuwa salama maana viashiria
vinafahamika na vimewekewa mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti kwa manufaa
mapema.
Mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na Maana na
makundi, Faida na Kanuni za Usimamizi wa Viashiria vya Vihatarishi,
Matakwa ya kisheria kuhusu Usimamizi wa Vihatarishi nchini, Muundo na
maeneo muhimu ya kimwongozo, Mgawanyo wa majukumu katika Usimamizi wa
Vihatarishi na nyaraka mbalimbali zitakazotumika wakati wa kuandaa na
kusimamia Vihatarishi.
Mategemeo ya mafunzo hayo ya mahala pa kazi yanalenga washiriki
kuweza kubaini vihatarishi ambavyo viliwekwa mwaka jana na sasa
havitakiwi kuwepo tena, kubaini vihatarishi vipya ambavyo ama
vilisahaulika au vitaibuliwa sasa kutokana na shughuli na kazi za Idara
na Vitengo hasa baada ya mwaka kuisha na kupata maoni na ushirikiano wa
kutosha ili kwa pamoja kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kudhibiti
viahatarisi kazini.