Kuelekea mchezo maalum wa hisani kwaajili ya kuchangia fedha zitakazosaidia mahitaji ya wanafunzi, Mbunge wa Chalinze Mh. Ridhiwani Kikwete amekubali kujiunga na timu ya Alikiba itakayocheza na timu ya Mbwana Samatta.
Ridhiwani amekubali ombi la Alikiba la kuchezea timu yake kwenye mchezo huo kwa kusema heshima aliyopewa na msanii huyo ni kubwa na atashiriki kwani ni hatua muhimu katika kusaidia elimu.
Ridhiwani ameenda mbali zaidi kwa kuifananisha hatua ya Alikiba kumuita kwenye kikosi chake na kitendo cha timu za taifa kuita wachezaji wao kwaajili ya fainali za Kombe la Dunia.
Mchezo huo maalum kwa kuhamasisha uchangiaji wa vifaa na miundombinu mashuleni utapigwa Juni 9, mwaka huu, kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. Samatta atakuwa nahodha wa timu ya marafiki zake na Alikiba atakuwa nahodha wa timu itakayoundwa na marafiki zake.
''Umenipa heshima kubwa kama walivyopewa walioitwa kuwakilisha mataifa yao katika kombe la Dunia. Twende tukasaidie Elimu Tanzania. Mwanzo Mzuri . Haya Ndiyo Watu Wema Ufanya'', amesema Ridhiwani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni