Jumamosi, 17 Machi 2018

Uingereza Yaitaka Tanzania iiunge Mkono Mgogoro Wake na Urusi

Serikali ya Uingereza imeitaka Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuiunga mkono katika kupinga kitendo cha Urusi kutumia sumu aina ya novichok katika jaribio la kumuua jasusi wa Kirusi, Sergei Skripal na binti yake, Yulia.

Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita huko Salisbury, Uingereza na kwa sasa Skripal na Yulia wana hali mbaya hospitali.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke alisema nchi yake haitavumilia majaribio yoyote ya mauaji ya watu wasio na hatia ndani ya ardhi yake.

Cooke alisisitiza kwamba ni wazi Urusi ilihusika kwenye jaribio hilo na walipewa nafasi ya kueleza kwa nini waliamua kutumia sumu hiyo ndani ya Uingereza licha ya kwamba matumizi ya kemikali kama silaha ni kinyume cha sheria za kimataifa. Hata hivyo, alisema mpaka sasa hawajatoa maelezo kuhusu suala hilo.

“Baadaye leo (jana) nitaonana na waziri wa mambo ya nje ili kumweleza kuhusu jambo hili na kuomba ushirikiano wa Tanzania. Ninaamini Tanzania iko pamoja nasi katika hili,” alisema balozi huyo.

Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Tanzania kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Susan Kolimba alisema hawezi kulizungumzia kwa sasa.

Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga hakupatikana kuzungumzia suala hilo .

Mpaka sasa Uingereza inaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Austalia na Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato). Pia, imeripoti suala hilo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Pia imewatimua maofisa 23 wa intelijensia wa Urusi na imefuta ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov.

Vilevile, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ametangaza kwamba hakuna waziri yeyote au mtu kutoka familia ya kifalme atakayehudhuria Fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kufanyika Juni huko Urusi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni