Serikali
ya Tanzania na Rwanda kupitia mawaziri wanaohusika na ujenzi wamesaini
makubaliano ya kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Isaka hadi
Kigali ifikapo Oktoba mwaka huu.
Tukio
hilo limewakutanisha mawaziri watatu wa Tanzania ambao ni Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame
Mbarawa, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga pamoja na
Waziri wa Ujenzi wa Rwanda, James Musoni huku wakiwa wameongozana na
wataalamu mbalimbali wa miundombinu kutoka nchi hizo.
Kabla
ya kusaini makubaliano hayo yaliyofanyika jana Januari 20,2018 ,jijini
Dar es salaam, mawaziri wamepokea rasimu ya ujenzi wa reli hiyo na
kuijadili kabla ya kupitisha rasmi.
"Reli
hii ni biashara, lazima tufanye haraka, itasaidia kukuza uchumi nchini,
kuongezeka fedha za kigeni, barabara zetu zitadumu, watu wetu watakuza
biashara zao, "amesema Waziri Mpango.
Kwa
mujibu wa mapendekezo ya rasimu hiyo iliyoandaliwa na makatibu wakuu
kutoka Rwanda na Tanzania, mradi huo ulioanza mchakato wake miaka mitatu
iliyopita, sasa utaanza ujenzi wake rasmi baada ya kuwekwa jiwe la
msingi Oktoba mwaka huu na marais wa nchi hizo.
Makubaliano
yaliyofanyika jana Jumamosi ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya
wakuu wa nchi hizo mbili kupitia ziara ya rais Paul Kagame Januari 12,
mwaka huu.
Akiwasilisha
rasimu hiyo kabla ya kupitishwa, Mkurugenzi wa Miundombinu kutoka
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Rogatus Mativila amesema
rasimu imependekeza njia mbili za ufanikishaji wa mradi huo wenye urefu
wa kilometa 521.
Mativila
amesema njia ya kwanza ni kushirikisha sekta binafsi na njia ya pili ni
kutumia bajeti za serikali mbili kwa kila nchi kugharamia kipande
kilicho katika nchi yake.
Kabla
ya kusaini, Waziri Mpango amesema Januari 29, viongozi hao wanakutana
tena katika vikao vya ndani kwa ajili ya kujadili upatikanaji wa
gharama za mradi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni