Alhamisi, 11 Januari 2018

Meli yenye bendera ya Tanzania imekamatwa nchini Ugiriki



 January 11, 2018 Maafisa wa serikali Ugiriki wanaofanya doria baharini wamesema wameikamata meli iliyokuwa inapeperusha bendera ya Tanzania ambayo ilikuwa imebeba vilipuzi.
Meli hiyo inadaiwa kusafirisha vilipuzi kutoka Uturuki kwenda Libya, kinyume cha sheria iliyowekwa ya kutosafirisha silaha kwenda Libya. Maafisa wanasema meli hiyo ilikuwa imebeba kreti 29 zilizojaa vilipuzi pamoja na kemikali zinazotumiwa kuunda vilipuzi.
Wizara ya Safari za Baharini nchini humo kupitia kwa Afisa Mkuu wa walinzi hao wa Ugiriki Yiannis Sotiriou amesema meli hiyo ilisimamishwa ikiwa katika kisiwa cha Crete kusini mwa Ugiriki  baada ya maafisa kupewa taarifa.
Meli Ilisindikizwa hadi katika bandari mojawapo katika kisiwa hicho cha Crete na kufanyiwa ukaguzi. Sotiriou amesema meli hiyo ambayo ilinaswa Jumamosi ilikuwa pia na kasoro nyingi na haikufaa kuwa baharini.
Nahodha wa meli hiyo kwa jina Andromeda amedai ilikuwa inasafiri kuelekea Djibouti lakini baadaye ikabainika kwamba ilikuwa inasafiri kuelekea mji wa bandarini wa Misrata nchini Libya.
Shirika la AFP linasema mabaharia hao wanane waliokuwa kwenye meli hiyo watafikishwa mbele ya mwendesha mashtaka. Watano kati ya mabaharia hao ni raia wa India, wawili wa Ukraine na mmoja wa Albania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni