AFRIKA iko ‘bize’ na mapinduzi ya Robert Mugabe, wanasahau kwamba watu weusi wanakufa kwa kuteswa, wanakufa kwa njaa, wanauzwa kama nyanya sokoni kwenda kutumika kama watumwa katika mataifa ya Kiarabu. Afrika wapo bize na uchaguzi wa Kenya huku Waafrika wakiuzwa huko Libya.
Viongozi wa Afrika wamekuwa ni watu wa kukumbushwa na CNN na BBC ilihali wao ndio wanapaswa kuwa wa kwanza kuibua na kutatua matatizo yao. Afrika kwa ajili ya Waafrika na si Wazungu wala Waarabu waolivamia Libya. Naungana na wakereketwa wote wanaopaza sauti zao kulikemea hili.
Nimeona msanii wa Marekani T. I ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: “Tuliambiwa kwamba colonel Muammar Gaddafi ni dikteta lakini mbona kwenye uongozi wake hakukuwa na biasharaa ya binadamu na utumwa kama ilivyo sasa!” Watu maarufu wengine wengi wameonyesha hisia zao na kupinga vikali biashara hii ya kishetani.
Hapa isiwe tu ni juhudi ya siku moja na kusahau. Tunapaswa kukemea na kuchukua hatua mpaka biashara hii iliyo kinyume na dini pamoja haki za kibinadamu ikome. Lazima tutambue binadamu wote tupo sawa hakuna aliye juu ya mwenzake.
Inakuaje leo Libya inaangamia huku Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Alpha Conde yupo kimya! Watu wetu wanaangamia utafikiri hakuna mtu au mamlaka za kuwalinda na kuwatetea.
Viongozi mnafanya nini kwenye vikao vyenu wakati ndugu zetu wanakufa huko Libya, mnachukua hatua mapema mnapoona upinzani unafanya mikutano, kwanini msichukue hatua juu ya biasharaa hii ya binadamu inayokua kwa kasi Kaskazini mwa Afrika?
Suala la Waafrika kuzama wakielekea Ulaya halijaanza leo, tangu Gaddafi anaondolewa madarakani mwaka 2011. Shirika la habari la CNN ndiyo wameyavumbua haya tangu Novemba 4, mwaka huu, lakini biashara hii ya kununua na kuwatesa binadamu ina miaka mitatu sasa.
Wahamiaji hawa wanakimbia mataifa yao kwa sababu ya njaa, vita, uongozi wa kimabavu usiotambua na kuwahudumia wananchi wake vyema. Libya imegeuka sehemu ya walanguzi. Libya hakuna uongozi imara, Waarabu wamegeuza sehemu ya kujichotea mali na kuondoka.
Inawezekana vipi watu wanachukuliwa mateka na Serikali ya Libya ipo! Afrika imelala fofofo, viongozi amkeni. Fungueni macho bara linateketea. Afrika hamshangai kuona mambo ya ajabu yanayoendelea Libya, mnapataje usingizi kuona watu weusi wanauzwa kibabe tena huku wameshikiwa bunduki shingoni, mnakubali vipi kuona Waafrika wanateseka katika ardhi yao wenyewe.
Vitendo vya kinyama na kikatili juu ya watu wa Afrika sidhani kama vina nafasi katika ulimwengu wa sasa. Watu wanakufa na hakuna kiongozi yeyote Afrika anayekemea uchafu huu unaoendelea juu ya Waafrika wenzetu wanaouzwa.
Libya ilichafuliwa vibaya na vikosi vya dunia kuanzia Machi mpaka Desemba mwaka 2011. Pakawa peupe pee, nchi ikatawaliwa na wauza madawa na matapeli kutoka Uarabuni. Ufaransa, Marekani na Uingereza ni nchi ambazo zingepaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa kipaumbele katika kuisambaratisha Libya.
Kosa kubwa walilolifanya ni kumuua Gaddaf, sasa baada ya mataifa ya Ulaya kuzuia wahamiaji wasiingie Ulaya na mipaka mingi kufungwa, hivyo kundi kubwa la wahamiaji kutoka mataifa ya Cameroon, Alegria, Nigeria, Mali, Ivorycost, Togo, Sudani na Libya wakajikuta wamekwamia ndani ya mipaka ya Libya.
Kulingana na taarifa za kiusalama, Waarabu wakaanza kuwatumia kama watumwa kwa kuwauza nchi za kiarabu ambapo mtumwa mmoja anauzwa kwa Dola za Marekani 400, 500 mpaka 800, ukikataa unapigwa risasi au unapata mateso makali, siri hii ilifichuliwa mapema mwaka huu na CNN.
Watu weusi wamekuwa wakionekana ni watu wa ajabu sana kaskazini mwa Afrika, katika Taifa la Libya kipindi Gaddaf yupo madarakani asilimia 14 walikuwa ni watu weusi. Gadaf alikuwa anawapenda sana watu weusi na wengi wao walikuwa wanapatikana kusini mwa Libya na walikuwa ni wachapa kazi na wanalipwa mishahara mikubwa.
Hata hivyo, walikuwepo watu weusi wengi kutoka mataifa jirani lakini kundi la kigaidi la Al-Qaida walipoingia kumuondoa Gaddafi na vikosi vya dunia, watu weusi wengi walikwama Libya na wengi walichinjwa.
Hii biashara ya utumwa ya kuwatesa watu weusi Libya imeanza muda mrefu ijapokuwa ilikuwa haipewi kipaumbele na mashirika makubwa ya habari kama CNN, FOX NEWZ, ABC, BBC na Aljazeera ndio maana limeonekana ni jambo jipya.
Katika mkutano mkubwa wa viongozi wa Afrika uliofanyika Dakar, Senegal Novemba mwaka huu, ajenda kubwa ilikuwa kujadili juu ya suala la usalama wa Afrika na vitongoji vyake.
Kutoka Afrika Mashariki tuliwakilishwa na Paul Kagame, suala la Libya lilijadiliwa, Kagame alifafanua kwamba lazima Áfrika tujifunze kutatua matatizo ya ndani wenyewe pasipo kutegemea msaada kutoka nje. Kagame alisisitiza juu ya ushirikiano baina ya wanachama lakini pia alijitolea kuchukua wahamiaji 30,000 waliokwama Libya na kuwapeleka nchini kwake kuwaokoa kutoka kwenye biashara ya utumwa.
Nampongeza Kagame kwa kuwa mfano na kuonyesha ubinadamu na utu kwa wenzetu Waafrika. Tutawakumbusha hata kama mnakumbuka, hatuwezi kushuhudia watu weusi wanauzwa kama ngo’mbe huko Libya.
0762155025
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni