Jumanne, 26 Desemba 2017

Je ni kweli barani Afrika kuna fikra duni?

BARA la Afrika huchukuliwa kuwa ni bara linaloogelea katika dhiki za aina lukuki. Kuanzia ajali zilizo nje ya uwezo wa wakaazi wa bara hilo hadi zile ajali za kujitakia. Yaani tunajulikana kwa shida zilizo nje ya uwezo wetu kama vile ukame, hadi kwa shida za kujitakia kama zile za vita na magonjwa kama kipindupindu.
Lakini huenda kitu kibaya zadi, na kinachoudhi,  tunachotuhumiwa ni kwamba, uwezo wa kufikiri kwa Waafrika ni hafifu. Ndiyo sababu zipo shida nyingi za kujitakia barani. Katikati ya tuhuma hizi, wapo wasomi wa Kiafrika na hata wa ng’ambo wamejitahidi kuitetea Afrika dhidi ya madai haya kwa namna mbalimbali. Utetezi wao unagusa habari  hii ya fikra duni na pia sababu ya umasikini wa Afrika.
Baadhi ya watetezi wa Waafrika, ni kama vile wanakubali kwamba Afrika iko duni ukiilinganisha na Magharibi. Lakini, kwa maoni yao, shutuma ziwaendee watu wa Ulaya kwani historia ikifukuliwa inaonyesha jinsi hapo kale waafrika walivyokuwa na akili na maarifa, kabla ya wazungu kucheza rafu na kuinyanyasa Afrika.
Mawazo ya msomi maarufu wa Afrika, Anta Diop wa Senegal, ndiyo hasa hutumiwa na watu wanaodai kuwa Afrika zamani iling’aa. Hapa hoja siyo tu kwamba uduni wa Afrika ni kutokana na manyanyaso ya wazungu bali ukweli ni kuwa, hapo kale, Afrika iliitangulia Ulaya kwa fikra za kielimu. Afrika inayotajwa hapa ni Misri. Na kama kuna mmoja ataona shaka ikiwa Wamisri ni Waafrika kama sisi wa huku Kusini mwa Sahara, basi ataambiwa kwamba Misri yenyewe ilichota maarifa kutoka Ethiopia –kutoka kwa watu weusi, kutoka kwa Afrika kwelikweli.
Misri ya kale ni kisima cha maarifa. Kwa bahati mbaya lakini, (kulingana na watetezi hawa) kutokana na fitna dhidi ya waafrika, kwa sasa Wayunani ndiyo wanaotambuliwa kama chemchemi ya usitawi wa elimu ya sayansi tunayoifurahia leo. Wayunani waliipata elimu yao Misri. Au walau kwa kukutana na Misri, elimu yao ilipanuka zaidi. Mbinu za kibeberu zinawafanya waafrika wasahau historia yao njema na kudhani kuwa Afrika haijawahi kuipita Ulaya kwa fikra na maarifa.
Wengine wanaotetea mrengo huu, wanakuja wakikwepa kuwa na msimamo mkali kama huo hapo juu, wa kuonyesha kwamba Afrika iliwahi kuwa namba moja. Kwa lugha laini kidogo, wanadai kwamba Misri na Uyunani (Ugiriki ya Kale) ni kama watoto mapacha, wote, kwa wakati mmoja, walibahatika kuibukia na kuwa na kipawa cha maarifa, ila tu, ‘mtoto Uyunani’ (mzungu) akawa mkorofi na akamnyanyasa ‘Mtoto Mmisri’ (Mwafrika).
Utetezi huo waweza kuwa na chembe za ukweli, lakini nadhani vilevile kuwa huu ni utetezi unaokwepa uwajibikaji. Hakuna maelezo ya kuridhisha kwa nini ghafla Afrika iliyong’aa ififie katika karne hizi za zamani sana. Labda maelezo yatakayotolewa baada ya biashara ya utumwa na ukoloni barani Afrika, labda yanaweza kuwa na mantiki kwa nini Afrika idumae, ingawaje nayo, kwa maoni yangu siyo sababu ya kuhalalisha uduni wa Africa mpaka leo. Lakini pia, baadhi ya madai kwamba Afrika hapo kale sana, yaani miaka mia kadhaa kabla ya Kristo ilikuwa na wakaazi wenye fikra na elimu bora kuliko watu wengine wa sayari hii, ni madai ambayo ni vigumu kuthibitika pasi shaka.
Hata kama ni kweli kuwa hapo kale Afrika iling’aa basi hiyo inabaki kuwa historia, na nadhani ni aibu kuendelea kung’ang’ania historia badala ya kupambana kukabiliana na mabadiliko ya historia. Anayepambana ndiye anayeshinda. Kupambana hapa maana yake ni kujibu changamoto za wakati husika kwa kutumia majibu sahihi yanayojibu alama za nyakati. Kusema kwamba ‘tulikuwa na nguvu ila sasa hatuna nguvu’ ni kama vile kukiri kwamba tumetupwa nje ya ulingo, siyo ulingo wa watu wanaopigana kuthibitisha nani mwenye nguvu zaidi, bali ulingo wa wanaopigana na changamoto zao na kuzishinda. Ni kama kusema kwamba, kwa sasa uwezo wetu ni kuwatazama watu wengine wenye uwezo wa kupambana na changamoto na kufaidika japo kidogo na ushindi wanaoupata.
Kama tumeikumbuka historia nzuri ya hapo kale, ni wajibu wetu kukazana bila kupoteza muda wa kuwalaumu wengine kana kwamba wamezishika akili zetu.
Nimeikumbuka hotuba ya Ehud Barak, waziri mkuu wa zamani wa Israel akimkaribisha Papa John Paul II katika eneo la kumbukumbu ya mauaji ya wayahudi. Ehud akasema, ‘Letu ni taifa linalokumbuka’. Taifa linalokumbuka magumu na mema liliyoyapitia, na linapoyatazama magumu, kwa vitendo linanuiya kwa dhati kwamba magumu hayo yasitokee tena kamwe. Ehud Barak anarejea vipindi vigumu na vichungu vya historia ya taifa lake. Wamekataa kuwa wafungwa wa historia bali historia huwafundisha mbinu mpya.
Labda Africa kuna sehemu tulijisahau. Na tunapojitahidi kukumbuka, ukumbusho wetu hauonekani kutunyanyua kutoka hapo tulipo, hautufundishi kujibu alama za nyakati, bali tunatafuta wa kumlaumu zaidi.
Lipo kundi lingine tena linalojaribu kujibu tuhuma kuhusu madai kuwa Afrika ina wenyeji wenye fikra duni. Kundi hili, utetezi wao upo katika madai kuwa, tulinyanyaswa na wafanyabiashara wa utumwa, kisha wasomi wa Ulaya wakatuandika vibaya kwenye vitabu vyao vya kisomi, na hii imechangia kutujengea taswira kuwa wafrika ni viumbe duni. Hata kama sisi ni duni, ni kwa sababu tumefanywa hivyo na wengine. Utetezi kama huu, kadhalika unakwepa uwajibikaji. Ni kweli kwamba hasara ya kihistoria ya biashara katili ya utumwa ni janga baya sana.Dhambi hii ya utumwa ni kweli kwamba iliacha vidonda. Lakini vidonda vinaweza kupona. Tunapaswa kujua kuwa, hata historia chungu inaweza kuwa mwalimu bora. Tena tujue kwamba, Africa siyo sehemu pekee yenye watu waliowahi kunyanyaswa katika historia.
Frantz Fanon, amejitahidi sana kutufundisha waafrika kuwa, historia isisomwe kama kitu kilichoganda. Isomwe kwa jicho linalotazama chanzo cha dhahama fulani, na mawimbi yanayozingira jitihada za kujinasua katika dhahama hiyo. Kwa maoni yangu, mpaka sasa, tunaichukulia historia kama kitu cha kale ambacho hatuna uwezo wa kukijibu. Katika mapambano mawimbi yapo, lakini hatimaye matumaini ni kuyashinda mawimbi haya na hatimaye kuzungusha gurudumu la historia yenye fahari, inayojibu kwa matumaini vipindi vichungu vya tulipotoka.
Kundi lingine la watetezi, limeamua kukanusha kwamba Afrika siyo bara la watu wenye fikra duni. Fikra zetu siyo hafifu, ila tu namna yetu ya kufikiri ni tofauti na namna ya Kizungu ya kufikiri. Yaani kulingana na mazingira na tamaduni zetu, sisi tunajikuta tukiwa na mfumo tofauti wa kifikra. Jiografia, historia, mazingira na mambo mengine mengi ndiyo huunda namna jamii fulani inavyofikiri. Kwa hiyo kuna namna ya ‘kizungu’ ya kufikiri na namna ya ‘kiafrika’ ya kufikiri. Mwandishi Marlene Van Niekerk, anawataja waandishi kadhaa wa falsafa ya kiafrika ambao wanaelekea kuwa katika mrengo huu wa kuona kuwa Afrika ina ‘namna’ yake ya kufikiri. Mmojawapo ni rais wa kwanza wa Senegal Leopold Sedar Senghor. Pia yupo mmisionari Mfransiskani kutoka Ubelgiji aliyeishi na kutafiti katika jamii za kibantu Placide Temples aliyeandika kitabu ‘Bantu Philosophy’. Wengine ni Alexis Kagame wa Rwanda na John Mbiti wa Kenya. Hawa wanaonekana kama watu wema wenye lengo jema la kuonyesha mtindo wa Kiafrika ambao siyo lazima ufanane na wa kizungu. Utajiri wa dunia ni pamoja na kuwa na aina nyingi za mawazo na falsafa. Afrika ni tofauti na Ulaya.
Mawazo kama haya, yanaweza kuwa na ukweli kwa upande mmoja. Lakini yanaweza kujenga njia ya ubaguzi kwa upande mwingine. Huu ni mwanzo wa kusema “nyie mko hivi” na “sisi tuko vile”. Fanon tena, anaonya kwamba, namna hii ya kutofautisha ‘sisi’ na ‘wao’ inaweza hata kuwa msingi imara sana wa ubaguzi. Kama watoto, tutaelekea kusutana; ‘mimi nina hiki, wewe huna; nionee wivu’. Ndivyo anavyoelekea kuonya Fanon ambaye tayari alikwishawasikia wazungu ambao wakiulizwa ‘mtu mweusi ni nani’, wangejibu ‘ni mwanamichezo, ni mkimbiaji, ni jitu lenye nguvu, nk’. Kwa juu juu hizi tunawea kuziona kuwa ni sifa njema, lakini siyo mara zote zinapelekea kuonyesha utu wa mtu mweusi.
Wiki ijayo tutaendelea kutazama mada hii, na majibu ambayo labda ni muafaka zaidi katika kujinasua kutoka katika hali ya udhalili.


source raia mwema gazeti.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni