Maisha
ni urafiki. Mwanafalsafa mwenye asili ya Kiafrika Martin Luther Jr.
King alipata kusema hivi, “Ukimya wa marafiki zetu unaumiza kuliko
kelele za madui zetu”. Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote. Mwenyezi
Mungu ni rafikiwa kweli katika maisha yetu ya kila siku. Anatulinda.
Anatupenda. Anatubariki.
Anatuongoza
katika njia iliyo takatifu. Tukumbuke jambo moja ambalo ni la mhimu
sana: Hatuwezi kufanikiwa kiroho, kimwili, kiuchumi, kimaadili,
kifamilia, kama hatumtazami Mwenyezi Mungu kama rafiki yetu mwema na
muumba wetu.
Yesu
Kristo aliwahakikishia wanafunzi wake upendo wake kwao kwa kuwaita
rafiki. Tunasoma hivi katika maandiko matakatifu, “Siwaiti tena watumwa,
kwa sababu mtumwa hajui kazi za Bwana wake. Badala yake ninawaita
rafiki, kwa kuwa nilichojifunza kwa Baba yangu nimewajulisha (Yoh
15:15).”
Huu ni urafiki usioweza kuelezeka kwa maneno bali kwa upendo tu. Yesu Kristo ni rafiki yetu. Ni kaka yetu. Ni mkombozi wetu.
Usithubutu
kumuacha Mungu kwa ajili ya chochote, bali acha chochote kwa akjili ya
Mungu, kwa sababu katika maisha chochote chaweza kukuacha wakati wowote.
Lakini Mungu atakuwa nawe siku zote za maisha yako.
Siri
kubwa ambayo unatakiwa kuifahamu ni kwamba; Mwenyezi Mungu ni rafiki
yako mwema hata pale unapokabiliwa na nyakati ngumu katika maisha.
Kuna
mtu ambaye aliota ndoto. Ndoto yake ilimuonesha kwamba alikuwa
anatembea kando ya bahari yenye michanga. Alipokuwa na furaha alitazama
nyuma na kuona nyayo za watu wawili. Alipokuwa na shida alitazama nyuma
na kuona nyayo za mtu mmoja. Ndoto hii ilimtatiza.
Akiwa
bado kwenye ndoto yake alimuuliza Mungu maana ya ndoto yake. Mungu
alimjibu kwa kumwambia: “Unapokuwa na furaha tunakuwa pamoja”. Mtu huyo
alidadisi tena na kuuliza: “Mbona wakati wa shida naona nyayo zangu peke
yangu?” Mungu alimjibu kwa kumwambia: “Wakati wa shida nakubeba
mgongoni ndiyo sababu unaona nyayo za mtu mmoja.”
Urafiki
ni uhusiano wa nafsi mbili wa kimapendo au wa matashi mema. Kwa tafsiri
hiyo, nafsi hizo zinaweza kuwa za jinsia moja au tofauti. Urafiki ni
uhusiano mwema baina ya mtu na mtu, nchi na nchi au jamii na jamii.
Mwenyezi Mungu ametuumba ili tuwe marafiki.
Tunasoma
hivi katika maandiko matakatifu, “Tazama jinsi ilivyo vema na kupendeza
ndugu kukaa pamoja kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani,
yanayoshuka ndevuni, ndevu za Haruni. Ni kama umande wa Hermon,
unaoshuka mlimani pa Sioni. Maana ndiko BWANA alipotawaza Baraka naam,
uzima hata milele (Zaburi133:1-3).”
Kwa
nini Mwenyezi Mungu anapenda tuishi maisha ya urafiki? Sababu kuu ni
hii. Mwanadamu ni kiumbe pekee aliyeumbwa kama Mungu. Mwanadamu ameumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu. Kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni hadhi
kubwa sana.
Hadhi
hii haina ufananisho na kitu chochote kile. Tunasoma hivi katika
maandiko matakatifu, “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa
Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke aliwaumba (Mwanzo1:27).”
Chimbuko
la urafiki wa Mungu na mwanadamu ni kwamba mwanadamu anashiriki sifa za
Kimungu. Urafiki ni tunu katika maisha. Tunahitaji kuuanzisha,
kuuboresha na kuuweka katika mazingira mazuri ya kustawi.
Urafiki
wa kweli haupatikani kwa njia ya magendo au mrungura, wala kununuliwa
kwa fedha, bali unajengwa. Bila urafiki, mbingu ingekuwa haina ladha na
dunia ingegeuka na kuwa jehanamu.
Maisha
ni urafiki. Kati ya zawadi nzuri ambazo tumepokea kutoka kwa Mwenyezi
Mungu ni zawadi ya urafiki. Mke wako ni rafiki yako. Mume wako ni
rafiki yako. Mtoto wako ni rafiki yako. Mzazi wako ni rafiki yako. Kaka
yako ni rafiki yako. Dada yako ni rafiki yako. Jirani yako ni rafiki
yako.
Naomba
kutoa ushauri huu. Nidhahiri na ni kweli kwamba ili uwe rafiki mwema na
msikivu kwa wengine ni lazima kwanza uwe rafiki mwema kwa nafsi yako na
familia yako. Kama umeoa au umeolewa fahamu kwamba rafiki yako wa
kwanza ni mke/mme wako.
Ngoja
niwafunulieni siri ya kuwa na furaha ya kudumu maishani. Anzisha
utaratibu huu katika maisha yako. Kwa wanandoa asubuhi unapoamka kutoka
kitandani muoneshe mke/mme wako tabasamu la upendo mwambie: “Nakupenda
sana mme/mke wangu, bila urafiki wangu na wewe nisingefika hapa nilipo.”
Kisha mbusu, busu takatifu.
Kisha
munong’oneze kwa kumwambia, “Kazi njema mke/mme wangu”. Jioni baada ya
mihangaiko ya kutafuta riziki unaporudi nyumbani sahau magumu
uliyokutana nayo. Epuka kuzileta hasira za kazini nyumbani kwako.
Unapofika nyumbani mwoneshe mke/mme wako tabasamu la upendo mwambie:
“Nakupenda
sana mke/mme wangu”. Kisha mbusu, busu takatifu. Halafu mkaribishe
mwenzako nyumbani kwa kumwambia, “Pole kwa kazi mke/mme wangu, karibu
tena nyumbani.”
Kabla
watoto wako hawajalala usiku waite huku ukiwaonesha uso uliojaa
tabasamu la upendo na kuwambia maneno haya: “Nawapenda sana wanangu”.
Kisha wabariki wakalale.
Kwa
Padre, Mtawa na Askofu asubuhi unapoamka kutoka kitandani inyanyue
mikono yako juu na kumtazama Kristo kuhani wako mkuu, kisha mwambie:
“Ninaomba kuwa Mchungaji mwema na rafiki mwema wa kondoo ninaowachunga.”
Sisi
binadamu tuliumbwa ili tupendwe na tupende. Mwenyezi Mungu alituumba
hivi ili tuwe na mawasiliano na urafiki, ndiyo maana binaadamu hawi
mkamilifu kama hana mawasiliano ya karibu na wengine.
Mwanateolojia
William Backlay alipata kufafanua kwamba, “Msingi mkubwa wa furaha ya
mtu duniani inalala katika uhusiano na wengine”. Unapopata fursa ya
kuishi tambua kwamba hiyo sio tu fursa ya kuishi bali ni fursa pia ya
kujenga urafiki na muumba wako, pasipo kusahau jamii ya watu
inayokuzunguka.
Tufafanue
kidogo namna ya kumpata rafiki wa kweli. Jambo moja tunalotakiwa
kuzingatia ni kwamba tunapoingia katika uhusiano wa kirafiki basi
tujitahidi sana kuishi maisha ya ukweli na uwazi ili tusiharibu uhusiano
wetu na Mungu wetu ambaye anajifunua kwetu kila siku kwa njia ya
marafiki zetu. Mwandishi Kahlil Gibran anasema, “Unaweza kumsahau yule
ambaye mnacheka pamoja, lakini huwezi kumsahau yule ambaye mmelia
pamoja.”
Rafiki
mwema ni yule ambaye anashiriki kwa ukaribu nyakati zote unazopitia
katika maisha. Tunapoingia katika maisha ya urafiki tusitangulize
maslahi fulani, badala yake tutangulize upendo kwanza kama nguzo kuu ya
kuimarisha urafiki wetu. Urafiki wa kweli ni nadra kupatikana. Unaweza kuniuliza:
“Kwa
nini urafiki wa kweli ni nadra kupatikana?” Sababu kubwa ni hii: “Ni
watu wachache sana duniani wenye hadhi ya kupenda na kupendwa bila
masharti.” Sababu ni kwamba watu wengi wanatafuta urafiki wa kupokea
kuliko kutoa.
Ukitaka
kumpata rafiki wa kweli mpime kwanza ndipo umruhusu kuwa rafiki yako,
usiharakishe kumuamini kwa sababu ya maneno yake matamu ama umaarufu
alionao katika jamii au cheo chake au urembo wa sura aliyonayo. Kwa
sababu kuna rafiki wa kudumu na kuna rafiki wa kukimbia wakati wa dhiki.
Tuepuke
urafiki wa kinafiki. Tuwaepuke marafiki wanaotushawishi kutenda dhambi.
Ikiwezekana punguza idadi ya marafiki ulionao, sio busara kuwa na
marafiki wengi, lakini wanafiki. Inatosha kuwa na marafiki wachache
lakini wenye upendo wa dhati.
Kuna
umuhimu wa kufanya utafiti wa kina wa marafiki hao. Kwa sababu ukiwa
tajiri kwa mfano, au mwenye kujiweza kimaisha, utapata marafiki wengi
tu, lakini ukiwa maskini, mgonjwa, mwenye shidashida hauwezi kuwapata
marafiki. Waswahili wana msemo unaosema kwamba, “Mkono mtupu haulabwi”.
Sababu ya hayo yote ni kwamba binaadamu ana upendo wa kimaslahi. Baadhi
ya watu wanasita kuwaonesha masikini upendo badala yake wanawaonesha
matajiri pekee upendo. Utamaduni huu si sahihi.
Mwandishi
E. Fromm anaeleza kwamba, “Kama nampenda mtu mmoja kwa dhati basi
nawapenda watu wote, naupenda ulimwengu, nayapenda maisha. Kama naweza
kumwambia mtu mwingine ‘nakupenda’ basi ni lazima niweze kusema,
nahitaji kuwapenda watu wote bila kuwabagua.”
Tatizo
kubwa na sugu ambalo linawakumba watu wengi ni kwamba wengi tunaanzisha
urafiki pasipo kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Ifahamike wazi kwamba ni
katika Mungu tu ndipo watu wanaweza kujenga urafiki wa kweli na wa
undani kabisa. Mungu akusaidie upate kuyaishi uliyoyasoma katika makala
hii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni