MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) imefafanua kuhusu viwango vya kodi, anavyopaswa kukatwa mtu binafsi aliyeajiriwa.
Akizungumza kwenye kipindi cha Kodi kwa Maendeleo
kinachorushwa na Shirika la Utangazaji nchini (TBC1) wiki hii, Meneja wa
Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA Makao Makuu, Gabriel Mwangosi
alisema kuwa mwajiri atakata kodi, pale tu ambapo mfanyakazi au
mwajiriwa anapata mshahara, kipato au ujira.
Mwangosi alisema kiwango cha kodi, ambacho mtu
anatakiwa kukatwa kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato, vinatofautiana
kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kulingana na kiwango cha kipato
anachopata mtu kwa mwezi.
Akifafanua kuhusu kodi ya ajira, ambayo mwajiriwa
anakatwa kwenye mapato au mafao yake, Mwangosi alisema kuwa kiwango cha
mshahara au kipato au ujira, kinachotakiwa kukatwa kodi ni kile
kinachozidi Sh 170,000 kwa mwezi.
Alisema kwa kuwa kwenye ajira kuna vyanzo tofauti
tofauti vya mapato kwa mwajiriwa, kama vile motisha (bonus), kamisheni,
ujira, mshahara, malipo ya likizo, posho na mengineyo, ambayo yote
yakijumlishwa yanatengeneza kipato cha mwezi, hivyo kipato hicho kama
hakizidi Sh 170,000 hakikatwi kodi.
Kipato cha Shilingi 170,000 kushuka chini hakina
kodi, kimesamehewa kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato Kifungu namba
10 ukisoma pamoja na jedwali la pili la kodi ya mapato ambalo linaonesha
viwango vilivyosamehewa kodi kuwa ni pamoja na hiki cha Sh 170,000
kushuka chini, alieleza Mwangosi.
Kwa mujibu wa Meneja huyo wa TRA, kiwango kinachozidi
Sh 170,000 lakini hakizidi Sh 360,000 kwa mwezi, kodi yake ni asilimia
tisa. Alisema kwa mfano mtu analipwa Sh 360,000 au 240,000,
kinachofanyika ni kwamba inatolewa Sh 170,000 kwenye kipato hicho na
kiasi kinachobaki ndiyo kinakatwa kodi ya asilimia tisa.
TRA inasema kuwa kwa mwajiriwa anayepata kipato
kinachozidi Sh 360,000 lakini hakizidi Sh 540,000 kwa mwezi, kodi yake
ni Sh 17,100, lakini inajumlishwa na asilimia 20 ya kodi kwa kipato
kinachozidi Sh 360,000.
Vivyo hivyo kwa kipato kinachozidi Sh 540,000 lakini
hakizidi Sh 720,000 kwa mwezi, kodi yake ni Sh 53,100, lakini itaongezwa
na asilimia 25 ya kiwango kinachozidi Sh 540,000.
Kiwango chochote cha kipato cha kuanzia Sh 720,000
kwenda juu kwa mwezi, kodi yake ni Sh 98,100, lakini inajumlishwa na
asilimia 30 ya kiwango kinachozidi Sh 720,000, hivyo kodi kwa mtu
binafsi hata kama analipwa Sh milioni 20 au zaidi, anakatwa kodi kwa
utaratibu huu, alisema Mwangosi.
Alisema kiwango hicho cha kodi cha asilimia 30 kwa
mujibu wa sheria za kodi ya mapato, ndiyo kiwango cha juu zaidi kuliko
kiwango kingine chochote. Alisema kwenye kodi kuna viwango vya asilimia
tano, asilimia 10, asilimia 15, asilimia 20, asilimia 25 na asilimia 30
ambacho ndiyo kiwango cha mwisho kwenye kodi ya mapato.
Mwangosi alisema kuwa mfumo wa kodi ya ajira,
unamtaka mwajiriwa alipe kodi kadri anavyopata kipato (PAYE). Alisema
mwajiriwa anayepata kipato kidogo, pia analipa kodi kidogo na anayepata
kipato kikubwa na kodi pia huwa kubwa.
Punguzo la kodi Kwa mujibu wa Mwangosi, Serikali kila
mara imekuwa ikirejea viwango vya kodi na kuendelea kuvipunguza ili
kuongeza watu wengi zaidi kwenye wigo wa kodi.
Alisema viwango vya kodi vinapokuwa juu sana,
vinawafanya watu kukwepa kodi na ndiyo maana Serikali huvirejea viwango
hivyo kila mara. Alisema kwa zamani asilimia ya kodi ya ajira ilikuwa
kubwa, kwa kuwa ilianzia asilimia 17 baadaye ikashushwa hadi asilimia
15, ikashushwa tena hadi asilimia 14, baadaye asilimia 12 na 11, na sasa
ni asilimia tisa.
Mwangosi alisema kuwa matokeo ya punguzo la asilimia
tisa la kodi ya ajira, alilolitoa Rais John Magufuli, linaonekana zaidi
kwa watu wenye kipato cha chini, tofauti na wenye kipato kikubwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni