Jumamosi, 4 Novemba 2017

Shirika la Msalaba Mwekundu lakiri kupoteza mamilioni ya Ebola

Watu 11,300 walifariki wakati wa mlipuko wa Ebola Afrika Magharibi 2014-15



Wakaguzi wa hesabu katika Shirikisho la Msalaba Mwekundu wamefichua kwamba mamilioni ya dola ambazo zilikuwa zimetolewa kama msaada wakati wa kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola zilifujwa.
Mlipuko huo uliathiri sana nchi za Liberia, Sierra Leone, na Guinea na operesheni kubwa ya kibinadamu iliendeshwa kuwasaidia waathiriwa na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Jumla ya $100m (£76m) pesa taslimu zilitolewa kwa mashirika ya Shirika la Msalaba Mwekundu katika mataifa hayo matatu na Shirikisho kuu la Msalaba Mwekundu mjini Geneva.
Nchini Liberia, $2.7m (zaidi ya £2m) zilitoweka kwa njia ya ulaghai kupitia kuongezwa chumvi kwa vitu vilivyouziwa shirikisho hilo.

Kadhalika, nyingine zilitoweka kupitia mishahara iliyolipwa kwa wafanyakazi hewa.
Nchini Sierra Leone, wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu walikula njama na benki moja kupora zaidi ya $2m. Na nchini Guinea, ambapo uchunguzi bado unaendelea, takriban $1m zilitoweka kupitia kutumiwa kwa risiti feki za ulipaji wa kodi.
Shirika la Msalaba Mwekundi limesema linaomba radhi kutokana na kupotea kwa fedha hizo na likaongeza kwamba limeweka mikakati zaidi ya kifedha kuzuia ufujaji kama huo wa pesa siku za usoni.
Aidha, shirikisho hilo limeahidi kuwaadhibu wafanyakazi ambao itagunduliwa walihusika.
Shirika la Msalaba Mwekundu ni moja ya mashirika yanayoaminika sana duniani na ufichuzi huo huenda ukaathiri sifa zake.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni