Zaidi ya nusu ya Watanzania
wamesema kuwa hali ya usalama nchini imeimarika ikilinganishwa na miaka
takriban miwili iliyopita na kuwafanya wananchi waishi kwa utulivu na
amani.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la Kiserikali lijulikanalo kama
Twaweza, Bw. Aidan Eyakuze wakati akiwasilisha matokeo utafiti wa “Hapa
Usalama Tu: Usalama, Polisi na Haki nchini Tanzania” kupitia sauti za
wananchi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Bw. Eyakuze
alisema kuwa takwimu zilizo kusanywa na sauti za wananchi kwa mwaka huu
zimeonesha kuimarika kwa usalama kwa wananchi wa Tanzania Bara
ikilinganishwa na miaka iliyopita.
“Tumeongea na
watu 1805 kuwauliza hali ya usalama katika maeneo wanayoishi na
asilimia 53 ambayo ni sawa na nusu ya Watanzania Bara wamesema hali ya
usalama imeimarika na inaridhisha” alisema Bw.Eyakuze.
Bw.Eyakuze
amesisitiza kuwa wamekusanya taarifa kutoka kwa wananchi wenyewe,
kupitia simu zao za mikononi ambapo wameona kuwa watanzania wengi wapo
kwenye hali ya usalama na hii inamewapa taswira tofauti na taarifa
zinazotolewa na vyombo vya habari.
Aidha, Bw.Eyakuze
amesema kuwa asilimia 47 ya wananchi wanaridhishwa na utendaji kazi wa
jeshi la Polisi nchini kutokana na kuzuia na kutatua uhalifu na kuwajali
wananchi.
Ripoti hiyo
imeonyesha kuwa wananchi wanapata pia ulinzi kutoka kwa polisi jamii,
maarufu kama sungusungu na asilimia 41 ya wananchi wamesema wana vikundi
vya sungusungu katika maeneo yao na wanaridhika na huduma zinazotolewa.
Utafiti huu
ulifanyika mnamo Aprili 2017 ukihusisha mikoa yote ya Tanzania Bara na
wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumuia simu za
mkononi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni