Taarifa kutoka magharibi mwa Kenya zinasema kuwa mtuhumiwa wa wizi wa
gari alijisalimisha kwa polisi

baada ya kuvamiwa na nyuki akiliendesha
gari hilo.
Mwandishi wa BBC, Wanyama wa Chebusiri kutoka Nairobi, anasema ripoti
hiyo iliyoripotiwa mara ya
kwanza kwenye gazeti la The Star la nchini
Kenya, imewaacha wengi vinywa wazi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwenye gari aliamini kwamba mshukiwa
alimuwekea dawa ya kulevya kwenye kinywaji katika hoteli moja na
kumfanya apoteze fahamu.
Saa kadha baada ya kurejelewa na fahamu, alipata gari lake halipo.
Mwenye gari alitafuta msaada wa mganga wa kienyeji ambaye alimhakikishia
kwamba mtuhumiwa atavamiwa na nyuki kabla ya kuondoka katika mji wa
Bungoma ulioko magharibi mwa Kenya.
Punde si punde, nyuki walimvamia mshukiwa akiwa ndani ya gari lililokuwa
limeegeshwa pembeni mwa barabara moja maarufu mjini Bungoma.
Katika harakati za kutaka kujinusuru kutoka kwa makali ya nyuki,
mshukiwa alichana mbuga akielekea kituo cha polisi cha Bungoma, huku
akipiga kelele za niokoe lakini wapi, nyuki walikuwa naye 'hapa kwa
hapa'.
Mwanamme huyo alijaribu kutoka katika kituo cha polisi lakini nyuki
walimwandama unyonunyo kabla ya polisi kumuokoa kwa kumfungia ndani ya
seli kwa mahojiano.
Mkuu wa polisi katika eneo la Bungoma David Kirui ameiambia BBC kwamba
nyuki walikuwa wamezingira kituo hicho cha usalama huku mshukiwa akiwa
anahojiwa kwa madai ya wizi wa gari.
Kisa hiki cha nadra kiliwastajabisha na kuwashangaza wakaazi wengi
wakiachwa vinywa wazi, huku wengi wa kijiuliza, je, ushirikina ungalipo?
CHANZO BBC