Jumanne, 11 Septemba 2018

SHAMBULIO LA SEPTEMBA 11: MIAKA 17 BAADAYE, BADO MAJERAHA HAYAJAPONA


Miaka 17 imepita tangu dunia ilipotingishika kufuatia mashambulizi makubwa ya kigaidi yaliyolenga jengo refu zaidi duniani, World Trade Centre jijini New York na Jengo la Wizara ya Ulinzi (Pentagon) jijini Washington.

Leo Wamarekani wakiongozwa na Rais Donald Trump, wataadhimisha kumbukumbu ya tukio hilo lililotokea Septemba 11, 2001 ambapo zaidi ya watu 3000 walipoteza maisha, shughuli itakayofanyika Shanksville, Pennsylvania nchini humo.

Japokuwa siku nyingi zimepita, bado jinamizi la tukio hilo linaendelea kuwasumbua Wamarekani wengi, hasa wale waliopoteza ndugu zao kwenye tukio hilo baya zaidi katika historia ya ugaidi duniani huku wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu.

Katika maadhimisho hayo, watu wote watasimama kimya kwa dakika moja kuwaenzi wote waliopoteza maisha katika tukio hilo, huku majina ya watu wote waliopoteza maisha yakitajwa.

Wamarekani wengi wameendelea kuisisitiza serikali yao kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii ndani ya ardhi ya nchi hiyo na kufanya kila kinachowezekana kukomesha ugaidi duniani kote.


Mshukiwa mkuu wa matukio hayo, Osama bin Laden aliyekuwa kiongozi wa Kundi la Al Qaeda, aliuawa Mei 2, 2011  Abbottabad, Pakistan na majeshi ya Marekani chini ya Rais Barrack Obama, katika oparesheni iliyopewa jina la Neptune Spear.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni