Ijumaa, 8 Juni 2018

Uongozi wa CUF waiangukia Serikali juu ya kuzuia ruzuku


Uongozi wa chama cha wananchi CUF umeiomba ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kukinusuru chama hicho na hatari ya kufa na kukosa uwezo wa kujiendesha kutokana na kuzuia kwa ruzuku ya chama hicho tangu mwaka 2016 ulipoibuka mgogoro wa kiuongozi katika chama hicho.

Aidha chama hicho kimesema mgogoro uliodumu kwa miaka miwili katika chama hicho umesababishwa kwa kiasi kikubwa na pande mbili zinazotaka kusimamia maslahi yao binafsi badala ya chama huku wakipindisha katiba ya chama kwa makusudi.

Akizungumza na East Africa BreakFast kaimu katibu mkuu wa CUF upande wa Profesa Lipumba Magdallena Sakaya amesema kuwa mgogoro uliopo umetokana na ubinafsi baina ya watu wachache na kusema kuwa lengo la Maalim Seif ni kuua chama.

“Chama ni taasisi na si mtu binafsi ndio maana watendaji sio Maalim Seif wala Profesa Lipumba bali ni wanachama wenyewe, mtu mmoja ndio anaigawanya CUF kwa sababu ya ubinafsi alitaka kuigawanya na kuiua CUF ndio maana tulieleza wazi mbele ya wananchi sababu za kurejea kwa Profesa”, amesema Sakaya

Hivi karibuni wakichangia Bungeni mjini Dodoma baadhi ya wabunge wa CUF walimuomba msajili wa vyama vya siasa nchini na serikali kwa ujumla kuiingilia kati mgogoro wa uongozi uliopo ambao umetishia uimara wa chama hicho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni