Leo ni siku ya Mazingira Duniani, ambapo Kampuni ya bima ya afya
nchini ya AAR imepanda miti katika shule ya msingi ya Ushindi iliyopo
eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam ikiwa ni hatua ya kuunga mkono
kwa vitendo utunzaji mazingira.
Wafanyakazi wa kampuni ya AAR wakiwa na wanafunzi hao
AAR imefanya zoezi hilo Jumanne hii ikipanda jumla ya miti 60 katika
shule hiyo ya Umma iliyo kwenye eneo lililo karibu na ofisi za makao
makuu ya kampuni hiyo, katika kuadhimisha siku ya mazingira.
Akiongea baada ya zoezi hilo la upandaji miti, Msemaji wa AAR
Bi.Hamida Rashid amesema kuwa kuboresha na kulinda afya ya jamii ni
sehemu muhimu ya jukumu la kampuni hiyo, hivyo haina budi kusaidia na
kuhamasisha kwa vitendo utunzaji wa mazingira katika jamii
inayotuzunguka kwani ndio msingi wa uhai.
“Tunafahamu mazingira ni muhimu katika maisha yetu kwani ubora wa
afya na uhai wetu unategemea hali ya mazingira yetu. Kama kampuni ya
bima ya afya ambayo hujikita katika kuboresha na kulinda afya ya jamii,
tunaamini kwamba ni jambo lisilowezekana kuwa na jamii yenye afya bora
bila kuhakikisha kuwa jamii inaishi kwenye mazingira bora
yanayohifadhiwa vizuri,” alisema Bi Rashid.
Aliongeza,”Ndio sababu tumeamua kuihakikisha jamii kwa vitendo
kupanda miti, Tunaamini elimu ya mazingira ikitokea vizuri kwa jamii
kuanzia kwa watoto shuleni tutajenga taifa la wachapakazi ambalo ni
rafiki wa mazingira,”
Aidha, Bi.Rashid alitoa wito kwa makampuni mengine pamoja na watu
binafsi kuunga mkono juhudi za serikali kulinda mazingira ili kuhuisha
ukuaji wa taifa lenye watu wenye afya bora. Pia aliwataka walimu
kushirikiana na wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu ya mazingira
kwa vitendo.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ushindi, Mwalimu Elias Katunzi
aliwashukuru AAR kwa kujitolea kuboresha mazingira ya shule hiyo na
kuahidi kuendelea kuwafundisha wanafunzi kuwa marafiki wa mazingira.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni