Serikali
inakusudia kukaa mezani na uongozi wa Hospitali ya CCBRT kujadili kwa
kina ili ianze tena kuipatia ruzuku kama ilivyokuwa awali.
Hayo
yalielezwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu, alipozungumza mbele ya Makamu wa Rais Samia Suluhu
Hassan aliyetembelea hospitali hiyo, Dares Salaam jana.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa CCBRT katika kuhudumia wananchi tena huduma nyingine mnatoa bila malipo.
“Hii
inamaanisha mnatoa huduma zaidi bila kujali faida, mnafanya vizuri
katika huduma za tiba ya mifupa, macho na afya ya mama na mtoto.
“Mnasaidia
mno kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika hospitali zetu za serikali,
ni kweli awali serikali ilikuwa inawapatia ruzuku lakini katika awamu
hii ya tano ilisitishwa.
“Tunakusudia
kukaa nanyi tena mezani tujadiliane na tukubaliane, lengo letu
tunataka ile ruzuku tutakapokuwa tunaileta iwafikie watumishi husika
moja wa moja, tunataka kujua tunawalipa wauguzi au madaktari kiasi
gani,” alisema.
Alisema
CCBRT imekuwa mdau mzuri katika sekta ya afya kwa kushirikiana na
serikali ambako imekuwa ikiwajengea uwezo watumishi wake.
“Kwa
mantiki hiyo tunakusudia kuipandisha hadhi CCBRT na kuifanya hospitali
ya pekee inayoshirikiana na serikali katika kutoa matibabu dhidi ya
tatizo la fistula,” alisema.
Awali,
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Erwin Telemans aliiomba serikali
kuipunguzia kodi hospitali hiyo iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa
jamii.
“Hatua
hiyo itatuwezesha kuendele kununua vifaa tiba vya kutosha na hata
kuwalipa maslahi mazuri wafanyakazi wetu ikizingatiwa kwamba zipo huduma
ambazo wagonjwa huhudumiwa bila malipo ikiwamo ya fistula,” alisema.
Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema serikali imepokea ombi hilo na
italifanyia kazi hasa kupitia meza hiyo ya majadiliano.
“Waziri
amesema itaandaliwa meza ya majadiliano, hivyo ni imani yangu kwamba
mtajieleza vizuri kwa kina kuhusu huduma mnazotoa na kuonyesha matokeo
ya kazi mlizofanya.
“Sisi (serikali) tupo tayari kushirikiana nanyi ili tuendelee kuboresha huduma za afya nchini kwa pamoja.
“Mmenieleza
kwa siku mnapokea wagonjwa wapatao 700, binafsi nimeguswa kwa jinsi
mlivyoboresha afya ya mama na mtoto na namna mnavyowarejeshea furaha
watu waliopoteza viungo.
“Hakika hii ni kazi ya kiungu na mnatoa sadaka kubwa kwa watanzania,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni