Gharib MZINGA
Abdul Lausi na Joseph Ksyupa ni miongoni mwa majina ambayo yameacha
historia kubwa katika soka la Mkoa wa Mbeya, vijana hawa wawili ndio
waliotoa wazo la kuunganisha vilabu viwili vya wilayani Rungwe Tukuyu
Mkoani Mbeya, Mwenge FC na Jamuhuri FC mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Dhumuni kubwa likiwa ni kunyanyua soka la Wilaya hiyo ili kupata timu
itakayowakilisha katika ligi daraja la kwanza (ligi kuu sasa).
Jitihada za Wanatukuyu wakiunganishwa na timu hiyo zilizaa matunda kwa kumpata mdhamini mkuu mfanya biashara Ramnik Patel Kaka.
Timu hiyo ya Tukuyu Stars ‘Banyambala’ ilianza harakati miaka ya
1982, ilifanikiwa kucheza michezo mingi ya kirafiki ya kimataifa ikiwa
ligi daraja la 3 na 2, Ilicheza na timu ya taifa ya Msumbiji pia katika
harakati za kujipanga katika kupigana kupanda ligi daraja la kwanza
(ligi kuu sasa).
Mwaka 1985 Tukuyu Stars ‘Banyambala’ ilifanikiwa kupanda daraja na
kuingia ligi daraja la kwanza rasmi, kikosi cha Tukuyu kiliundwa na
wachezaji nguli kama vile Asanga Aswile, Mbwana Makata, Betwel Afrika,
Daniel Chundu, Chachala Muya, Kelvin Haule, Peter Mwakibibi na wengine.
Mwaka ho 1986 Tukuyu Stars ilifanikiwa kucheza ligi kuu na kubeba
taji la ligi hiyo kipindi hicho ikidhaminiwa na kampuni ya bia ya Safari
Lager.
Hii ni kumbukumbu kubwa katika historia ya soka la Tanzania na Africa kwa ujumla wakivilaza njaa vilabu vikongwe Simba na Yanga.
Baada ya mwaka huo miaka miwili mbele (1988) Tukuyu Stars ilishuka
daraja na kuenda kusikojulikana, ilisababishwa na wachezaji wake wengi
muhimu kuchukuliwa na vilabu vikongwe Simba na Yanga.
Baada ya Tukuyu Stars kuonesha uwezo na uthubutu hakuna timu nyingine iliyowahi kufanya ivyo.
Timu nyingi zimekua zikipanda na kushuka nyingine zikipanda na kubaki
katika ligi huku zikiwa zinasuasua kubakia, Mbeya City msimu wake wa
kwanza ilijaribu kuutafuna mfupa huo lakini ikashindwa, macho mengi
yalielekezwa kwa Singida United huwenda ingethubutu lakini imeshindwa.
Timu nyingi ukiacha Simba na Yanga zimechukua taji la ligi tangu
ikiitwa daraja la kwanza mpaka sasa ligi kuu(VPL) Cosmopolitan 1967,
Mseto 1974, Pan Africa 1982, Coastal Union 1988, Mtibwa Sugar 1999/2000
na Azam FC 2013, lakini Tukuyu tu ndiyo iliyochukua taji hilo kwa msimu
wake wa kwanza.
Nani ataweza kuutafuna mfupa wa Tukuyu Stars ‘Banyambala? KMC, African Lyon, Biashara, Alliance, JKT Tanzania au Coastal Union?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni