Ijumaa, 8 Juni 2018

Mashambulizi dhidi ya Hodeidah ni sawa na kuua raia- OCHA




Shambulio dhidi ya bandari ya Hodeidah nchini Yemen linaweza kuwa na madhara kwa mamia ya maelfu ya raia wasio na hatia nchini humo ikiwemo kupoteza maisha.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imesema hayo leo huko Geneva, Uswisi wakati huu ambapo bandari hiyo ni tegemeo la kufikishia misaada ya kibinadamu.
Takribani watu milioni 8.4 nchini Yemen hawana uhakika wa chakula na wako hatarini kukumbwa na njaa kali.
Akizungumza na waaandishi wa habari hii leo huko Geneva, msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema, “Mashirika ya misaada ya kibinadamu nchini Yemen yana hofu kubwa juu ya shambulio la kijeshi dhidi ya bandari hiyo ya Hodeidah. Umoja wa Mataifa na wadau wake wanakadiria kuwa raia wapatao 600,000 hivi sasa wanaishi Hodeidah.”
OCHA imeonya mara kwa mara juu ya hatari za raia kushambuliwa Yemen wakati wa kampeni za kijeshi zinazohusisha askari wanaoungwa mkono na Saudia Arabia na wapinzani wa kihouthi, kampeni ambayo ilianza mwezi Machi mwaka 2015.
Tangu wakati huo, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesema raia zaidi ya 6,000 wameuawa huzu zaidi ya 10,000 wamejeruhiwa.
“Hali inazidi kuwa mbaya nchini humo wakati huu ambapo tayari miundombinu ya kiuchumi na kijamii imedhoofishwa, ikiwemo winchi za kupakulia shehena kwenye bandari ya Hodeidah,” amesema bwana Laerke.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa OCHA kuendelea kwa kampeni ya kijeshi kwenye  bandari hiyo tegemewa kutakuwa na madhara makubwa lakini, “ mashirika ya kibinadamu  yameshaandaa mpango wa kuchukua hatua. Ikiwa kampeni hiyo ya kijeshi itaendelea kwa muda mrefu, tuna hofu kuwa watu wapatao 250,000 watapoteza kila kitu, hata maisha yao.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni