Ijumaa, 1 Juni 2018

Mafuta ya petroli na dizeli yasafirishwa kwa chupa


KISIWANI Mafia, mkoa wa Pwani nchini Tanzania, mafuta ya petroli na dizeli yanauzwa kwa rejareja katika vibanda, huku kukikosekana kituo cha mafuta kukidhi mahitaji ya matumiaji wenye vyombo vya usafiri kisiwani humo.

Mafuta hayo hupimwa kwa chupa, kisha yanauzwa kwa bei ya juu kuliko maeneo ya karibu kama Dar es Salaam.

Wauzaji wanasema sababu kuu ni kutokuwa na usafiri wa kuaminika kuingia na kutoka kisiwani humo.

Wauzaji hufunga safari kutoka Mafia hadi maeneo ya karibu kama Dar es Salaam na Pwani, wananunua mafuta katika vituo vya mafuta kama wateja wengine. Wao huyaweka kwenye pipa na kusafirisha kwa mashua hadi kisiwani Mafia.

Kwa kawaida, hununua mafuta kwa bei ya wastani ya  petroli kwa lita moja, kisha wanaongeza pesa kidogo kwa wanunuzi yanapofika Mafia.

Mashua hizo huweza kuchukua siku kadhaa kutokana na hali ya upepo wa bahari na wauzaji wa mafuta hayo wanasema kuna uwezekano wa mapipa kupasuka katika mashua hizo, hivyo wakaangukia hasara kubwa.

Kwenye vibanda katika eneo hilo, wauzaji wengi wamekuwa wakiogopa kuzungumza kutokana na kutojua hatima ya kazi yao, ingawa wamekuwa msaada mkubwa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri.

Mmoja wa wauzaji, Abdalah Mohamed anasema gharama wanayotumia kununua mafuta na kuuza, wanapata faida ndogo sana kutokana na gharama kuwa ya usafirishaji huo.

''Tunayavusha katika bahari na kuna wakati bahari inachafuka, vitu vinapinduka lakini sasa ndio kazi hiyo,'' anasema Abdallah.

Wanategemea mafuta kuendesha kazi zao, kama vile wamiliki wa magari ya teksi na bajaji, wanasema mafuta yanachukua muda mrefu kufika, hivyo biashara zao zinaathirika.

Bakari Ismail, ni dereva wa teksi anayeeleza namna alivyowahi kusimamisha biashara kutokana na uhaba huo wa mafuta.

''Nimewahi kupaki gari kwa muda wa siku nne, wateja wananipigia simu nawaambia kuwa sina mafuta hadi nilipoyapata, mafuta nikaendelea na biashara,'' anasimulia.

Serikali inawasimamiaje?
Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Nnondoma, anasema wameruhusu uuzaji mafuta katika vibanda, kutokana na usafiri wa mashua hauwezi kuleta mafuta kwa wingi. Kwa hiyo wafanyabiashara hawa wamekuwa na umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa mafuta kisiwani hapa.

''Wafanyabiashara wadogo  wananunua kwa bei ya kawaida na wanakuja kuuza hapa, tumewaruhusu wauze kwa bei ya soko itakavyowaruhusu, kwa sababu akiuza bei ndogo sana, hawezi kupata faida na wanasaidia sana wakazi wa hapa,'' anasema Nnondoma.

Hata hivyo, awali walikuwa wanauza karibu na makazi ya watu, lakini uongozi wa kisiwa hiki uliwahamishia mbali na makazi ya watu. BBC

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni