Ratiba
ya michuano ya SportPesa Super Cup 2018, inayotarajiwa kuanza
kuunguruma Juni 3 mpaka 10, mwaka huu katika Uwanja wa Afraha mjini
Nakuru, Kenya, tayari imetoka ambapo Yanga itafungua mashindano hayo kwa
kumenyana na Kakamega Homeboys ya Kenya.
Mchezo
huo umepangwa kuanza saa 7:00 mchana, huku Gor Mahia ambayo nayo ni ya
Kenya ikipambana na JKU ya Zanzibar kuanzia saa 9:15 alasiri. Mechi hizo
zote zitachezwa Juni 3.
Simba
ya Tanzania, wao watacheza siku inayofuata dhidi ya Kariobangi Sharks
ya Kenya mchezo utakaopigwa majira ya saa 9:00 alasiri ambapo siku hiyo
itachezwa mechi hiyo pekee. Juni 5, AFC Leopards ya Kenya itakutana na
Singida United kutoka Tanzania.
Mmoja
wa waratibu wa michuano hiyo, Sabrina Msuya, alisema, maandalizi yote
yako vizuri na timu kutoka Tanzania ambazo ni Simba, Yanga na JKU
zinatarajiwa kuondoka kesho Alhamisi, huku Singida United ikisubiri
mpaka imalize mechi yake ya Kombe la FA itakayochezwa Jumamosi hii.
“Mambo
tayari yako safi kabisa kwani ratiba imetoka na timu za hapa nchini
zitaondoka Alhamisi kuanzia saa 3:00 asubuhi ambapo Simba ndiyo itakuwa
ya kwanza ikifuatiwa na JKU ambayo itaondoka Saa 7:00 mchana na baadaye
saa 11:00 jioni, Yanga itafuatia.
“Singida
United yenyewe itaondoka mara tu baada ya mchezo wake wa FA
unaotarajiwa kufanyika Juni 2, mwaka huu huko Arusha,” alisema Sabrina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni