Ijumaa, 8 Juni 2018

Hatua ya kukomesha plastiki ianzie nyumbani na kwa vitendo : Guterres




 



wakati wa kuchukua hatua kudhibiti uchafuzi wa bahari ikiwemo utokanao na plastini ni sasa, na lazima hatua hizo zianzie nyumbani na kwa vitendo.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya bahari duniani inayoadhimishwa hii leo Juni 8. Guterres amesema ulinzi wa bahari ni muhimu sana kwani bahari ndio kiini cha uhai wa kila kiumbe katika sayari hii.
Mwaka huu maadhimisho yamejikita katika uchafuzi wa bahari utokanao na plastiki, huku kauli mbiu ikisisitiza utokomezaji wa matumizi ya plastiki zinazotumiwa mara moja tu na kutupwa ambazo nyingi huishia baharini.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa asilimia 80 ya uchafuzi wa bahari unatoka nchi kavu ikiwa ni pamoja na tani milioni 8 za plastiki kila mwaka ambazo huathiri mifumo ya maji, jamii zinazotegemea uvuvi, sekta ya utalii, kuua viumbe wa baharini kama kasa na Ndege, nyangumi na hadi kuishia kwenye mifumo ya chakula ambayo dunia inaitegemea.
Guterres ameonya kwamba dunia ispobadili mwelekeo basi uchafu wa plastiki hivi karibuni utazidi idadi ya samaki baharini.
Amehimiza wajibu wa kila mtu na wa pamoja katika kukomesha janga hili linalozuilika la kupunguza uchafuzi wa kila aina baharini ikiwemo utokanao na plastiki na kuahidi kwamba, Umoja wa Mataifa utaongoza kwa mfano na tayari mashirika yake zaidi ya 30 yameanza utekelezaji wa kukomesha matumuzi ya plastiki zinazotumika mara moja tu na kutupwa.
Kwa mukhtada huo Guterres ametoa wito kwa serikali, mashirika ya kibinadamu na asasi za kiraia kwamba, kila mmoja ana wajibu wa kuhimiza jamii kuhusu athari zamabadiliko ya tabia nchi na kutoilinda bahari, akisema hatua madhubuti zisipo chukuliwa kuna uwezekano mkubwa wa kuangamiza kizazi kijacho, hivyo kila mmoja anaweza kuleta mabadiliko leo na kila siku kwa kufanya mambo rahisi tu kama kuepuka bidhaa za plastiki ili kulinda kikazi kijacho dhidi ya zahma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni