Na Rachel Mkundai, Morogoro
Jumla ya wafanyabiashara wadogo wadogo 17,601 waliokuwa katika sekta
isiyo rasmi mkoani Morogoro wametambuliwa na hivyo watapatiwa
vitambulisho maalumu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waweze
kufanya biashara zao bila kusumbuliwa.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa kodi za ndani wa TRA Bw. Elijah
Mwandumbya alipokuwa akitoa maelezo mafupi kuhusu zoezi la kuwatambua,
kuwasajili na kuwapatia vitambulisho maalumu wafanyabiashara wadogo
wadogo walio katika sekta isiyo rasmi wakati wa hafla ya uzinduzi
iliyofanyika katika viwanja vya Masika mjini Morogoro.
Mwandumbya amesema zoezi la utambuzi linafanyika kwa kupitia vikundi vya
wafanyabiashara ambapo katika mkoa wa Morogoro vikundi 1851 vyenye
jumla ya wanachama 17,601 wametambuliwa na watapatiwa vitambulisho
maalumu vyenye jina na mahali wanapofanyia biashara zao ambavyo watadumu
nabyo kwa miaka mitatu.
Ameongeza kuwa kati ya hivyo 1,851, vikundi 473 vimeshapatiwa mafunzo ya
umuhimu wa kutambuliwa, kusajiliwa na kupatiwa vitambulisho vya TRA, na
kati ya hivyo vikundi 143 vyenye jumla ya wanachama 2,324
wameshasajiliwa ili waweze kufanya biashara zao bila usumbufu.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa tunawatambua wafanyabiashara wadogo wadogo
kwa idadi yao kwa ajili ya serikali kupanga mipango mizuri ya kuboresha
biashara zao ziweze kuendelea na vile vile serikali iweze kuweka mipango
mizuri ya kuwapatia huduma mbalimbali,”alisema Bw. Mwandumbya.
Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk.Kebwe Steven Kebwe,
amesema ulipaji wa kodi ni jambo zuri sana na mkoa wa Morogoro ni
miongoni mwa mikoa inayofaidi matunda ya ulipaji kodi kwa kuwa na stendi
nzuri ya kisasa ya mabasi ya abiria, stendi ya Msamvu.
Aidha alitoa rai kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro kutumia fursa
hii ya kujisajili na kupatiwa vitambulisho vya TRA ili mkoa uweze
kuwapatia huduma muhimu kama vile maeneo ya kufanyia biashara ikiwemo
ndani ya stendi ya Msamvu.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni