Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amemteua Naibu Kamishna wa Polisi, Maulid Makabila kuwa Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (D/DCI) Zanzibar, huku akifanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa.
Kabla ya uteuzi huo, Makabila alikuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia uhalifu makao makuu ya Polisi Dar es Salaam.
Taarifa
iliyotolewa jana Alhamisi Mei 17, 2018 na msemaji wa polisi, Barnabas
Mwakalukwa imeeleza kuwa katika mabadiliko hayo aliyekuwa DCI Zanzibar,
Ramadhan Ng’anzi ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
kuchukua nafasi ya Charles Mkumbo aliyehamishiwa makao makuu ya
upelelezi, Dar es Salaam.
Aliyekuwa
kamanda wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali anakwenda
kuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba. Nafasi yake imechukuliwa
na Kamishna Msaidizi wa polisi, Thobias Sedoyeka aliyekuwa makao makuu
ya upelelezi Dar es Salaam.
“Kamanda
wa polisi mkoa wa Kusini Unguja, Makarani Khamisi amehamishiwa makao
makuu ya upelelezi Zanzibar na nafasi yake kuchukuliwa na kamishna
msaidizi wa polisi, Suleiman Hassan aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa
Kaskazini Unguja,” anasema Mwakalukwa katika taarifa hiyo.
Aliyekuwa
kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hasina Ramadhani Taufiq
anakuwa ofisa mnadhimu makao makuu ya polisi Zanzibar na nafasi yake
inachukuliwa na kamishna msaidizi, Haji Abdallah Haji aliyekuwa ofisa
mnadhimu Mkoa wa Mjini Magharibi.
Taarifa hiyo inaeleza mabadiliko hayo ni ya kawaida yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni