

Wageni wameanza kuwasili katika
kanisa la St George, Windsor Castle tayari kwa harusi ya kifalme kati ya
Mwanamfalme Harry na Meghan Markle, ambayo inafuatiliwa na mamilioni ya
watu kupitia runinga, mtandao na redio.
Meghan Markle tayari
ameondoka kwenye hoteli alimolala na yuko safarini kuelekea Windsor
Castle, ambapo atafunga ndoa na Mwanamfalme Harry.Miongoni mwa wageni waliofika ni nyota wa televisheni Marekani Oprah Winfrey na mwigizaji Idris Elba.
George na Amal Clooney, David na Victoria Beckham pamoja na Elton John pia wamewasili.
Mwanamfalme Harry na Meghan Markle watafunga ndoa saa sita mchana saa za Uingereza kabla ya kupita mjini kwa msafara.
Mwanamfalme Harry amepewa cheo cha Mtawala wa Sussex na bibi yake Malkia Elizabeth II, naye Bi Markle sasa atakuwa Mke wa Mtawala wa Sussex, Buckingham Palace imetangaza.
Mwanamfalme Harry, ambaye ni wa sita kwenye orodha ya warithi wa ufalme, pia amepokezwa vyeo vya Earl wa Dumbarton na Baron Kilkeel.
Maelfu ya watu wamefika Windsor kufuatilia harusi hiyo, wengi walikesha kuhakikisha wanapata nafasi nzuri ya kujionea yatakayokuwa yanajiri.
Mwanamfalme Charles, babake Mwanamfalme Harry, ndiye atakayemsindikiza Bi Markel kwenda kwenye madhabahu baada ya babake Thomas kushindwa kuhudhuria harusi hiyo kutokana na sababu za kiafya.
Mkesha wa harusi, Mwanamfalme Harry, 33, aliambia umati wa watu Windsor kwamba anajihisi "mtulivu" na kwamba Bi Markle, 36, anajihisi "vyema sana".
Katika kiapo chake cha ndoa, Bi Markle hataahidi "kumtii" mume wake. Mwanamfalme Harry ameamua kuwa na pete ya ndoa.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni