Ijumaa, 9 Februari 2018

Uhaba wa chakula kukumba nchi za kusini mwa Afrika

Athari za mabadiliko ya tabianchi mashinani picha:


Mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la mpango wa chakula, WFP na lile la chakula na kilimo FAO na ofisi ya usaidizi wa dharura, OCHA yamesema kwamba ukosefu wa nvua mwishoni mwa mwaka 2017 na mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018 unahatarisha uzalishaji wa chakula kwa nchi za kusini mwa Afrika.
Katika ripoti yao wamesema mabadiliko ya tabianchi  kama vile ukosefu wa mvua na ongezeko la joto kusini mwa bara la Afrika vimesababisha upungufu mkubwa wa  uzalishaji wa mazao katika nchi za jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC.
Nchi hizo ni pamoja na Botwana, Malawi, Msumbiji, Afrika kusini na Zimbabwe.
WFP imesema kutokana na mabadiliko ya ghafla ya tabianchi baadhi ya wazalishaji wakubwa kama Afrika Kusini  wameripoti kuporomoka kwa uzalishaji wa mahindi kwa asilimia 22, kitu ambacho kitaathiri eneo kubwa la nchi za kusini mwa Afrika  zinazotegemea mahindi kama chakula kikuu.
Kwa pamoja mashirika hayo yametoa wito kwa nchi za SADC na washirika wengine kutafuta njia mbadala ya kuweza kuokoa uzalishaji wa mazao na mifugo kusini mwa Afrika ili kuokoa maisha ya mamilioni wanaotegemea kilimo katika ukanda huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni