TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya michuano ya Azam
Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya
wenyeji, Buseresere FC Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza mchana wa leo.
Kiungo wa zamani wa Yanga, Hassan Dilunga alifunga bao la kwanza dakika
ya 52 kwa penalti baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye boksi, kabla
ya winga wa zamani wa Simba, Haroun Athuman Chanongo aliyembadili
mshambuliaji Stahmil Mbonde kipindi cha pil kufunga la pili dakika ya 82
akimalizia krosi ya Salum Kihimbwa.
Kiungo Ally Makalani akakamilisha shangwe za mabao za Mtibwa Sugar ya
kocha Zuberi Katwila kwa kufunga bao la tatu dakika ya 90 kwa shuti la
umbali wa mita 19 kufuatia pasi ya Haroun Chanongo, kabla ya Buseresere
kupata pigo dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika
90 za kawaida kwa mshambuliaji wake, John Evarest ‘Utaka’ kutolewa kwa
kadi nyekundu kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Mtibwa Sugar inakuwa timu ya nne kwenda Robo Fainali ya michuano hiyo,
baada ya Azam FC iliyoitoa KMC ya Kinondoni kwa kuichapa mabao 3-1 jana,
Singida United iliyoitoa Polisi Tanzania jana pia kwa kuifunga mabao
2-0 Uwanja wa Namfua, Singida na Njombe Mji FC iliyowatoa Mbao FC
Jumatano kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni