Jumanne, 27 Februari 2018

Mo Dewji atoa ahadi ya kuongeza Idadi ya Wanafunzi wanaopata ufadhili wa Taasisi yake




Taasisi ya Mo Dewji imetangaza orodha ya wanafunzi 22 wa elimu ya juu waliopata ufadhili kutoka katika taasisi hiyo kwa mwaka wa masomo 2017/2018 kupitia mpango wa Mo Scholars. Wanafunzi hao ni Neema Charles, Winfrida Mrope, Henritha Rwegasira, Monica Ubushimbali, Suzana Mkindi, Hamisa Selemani, Beatrice Shupa, Phoebe Mwankemwa, Amon Abraham, Venance Makambe na Amos Ntandu.

Wengine ni Benjamin Mkondya, Ally Mashaka, Amuniri Sebarua, Iddi Mbilinyi, Samwel Ponda, Eram Temu, Busumilo Tumaini, Cosmadeus Mayunga, Amos Kashinje, Kelvin Ernest na Barnaba Barnaba ambao wote ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Akizungumza kuhusu ufadhili huo, Mwanzilishi wa Taasisi ya Mo Dewji, Mohammed Dewji aliwapongeza washindi kwa kufanikiwa kupata ufadhili huo, lakini akiwataka kujituma ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika maisha yao.

“Mmepata ufadhili huu muutumie vizuri, wapo wengi ambao walituma maombi lakini nyie mmefanikiwa kupata ufadhili. Msome kwa bidii na baadae mpate kazi nzuri ambazo zitawasaidia kupata kipato na kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema Dewji. Dewji alisema aliamua kuanza kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.



Aliongeza kuwa, dhamira yake ni kuona Watanzania wengi wananufaika na mpango huo na amejipanga kuhakikisha kuwa idadi ya wanufaika wa mpango wa ufadhili unaotolewa na taasisi yake unaongezeka kila mwaka.

“Kasi yetu bado ni ndogo sana kulinganisha na ninavyotaka. Wakati tunaanza kutoa ufadhili tuliamua kuanza na wanafunzi 10 lakini mimi nataka tuwape ufadhili Watanzania wengi ikiwezekana tufike hata 100. Kwangu ni jambo jema sana kusaidia Watanzania wenzangu kwa sababu nimezaliwa hapa na nitazikwa hapa sina pengine pa kwenda,” alisema Dewji.


Nae mmoja wa wanafunzi ambaye kabla ya kupata ufadhili aliweka tangazo kwenye mtandao wa kijamii kwamba anauza figo yake, Amos Ntandu aliishukuru Taasisi ya Mo Dewji kwa ufadhili ambao imewapatia kwani baadhi yao waliokuwa wamepoteza matumaini ya kuendelea na masomo, lakini pia kuomba uongozi wa taasisi kuendelea kutoa ufadhili kwa Watanzania ili wapate elimu.

“Mimi nilikuwa tayari kuweka maisha yangu hatarini kwa kutangaza kuuza figo langu, lakini ufadhili huu mliotupatia umebadili maisha yetu. Idadi ya wanafunzi wanaokosa mkopo ni kubwa hivyo nawaomba muwe na moyo wa kuendelea kuwasaidia ili na wao wafikie ndoto zao,” alisema Ntandu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni