mwana wa liganga blog ni blog ya kutoa taarifa, matukio, yaliyotokea katika ulimwengu hususani katika nchi yaTanzania
blog hii inasimamiwa na mwandishi wa habari kitaaluma bwana Deus Thomas liganga.lengo ni kutoa taarifa kwa umma,kwa maendeleo ya taifa na Dunia kwa ujumla
kwa mawasiliano kuhusu mtangazo, habari, wasiliana nasi 0659944423,deusliganga@yahoo.com,mzeeliganga@gmail.com
Jumatano, 14 Februari 2018
MAJIBU YA NEC KWA CHADEMA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezijibu hoja sita za Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu uchaguzi mdogo wa ubunge katika
jimbo la Kinondoni.
Majibu hayo yametoka baada ya Chadema kuilalamikia tume na watendaji wake walioteuliwa kusimamia uchaguzi huo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, NEC ilidai haijapokea
barua yoyote kutoka Chadema licha ya chama hicho kikuu cha upinzani
bungeni, kuvieleza vyombo vya habari kwamba kimeiandikia barua tume
kuhusu wakuu wa wilaya kushiriki mikutano ya kampeni za kuwanadi
wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na tume haijachukua hatua zozote.
Taarifa ya NEC ilibainisha kuwa hoja ya pili ya Chadema ni tume
kuhamisha vituo 46 vya kupigia kura katika kata tatu za Kigogo,
Mwananyamala na Kijitonyama bila kuishirikisha Chadema.
Hoja nyingine ni Msimamizi wa Uchaguzi kutoa uamuzi dhidi ya Chadema
kwenye Kamati ya Maadili kwa uonevu na Chadema kuadhibiwa na Kamati ya
Maadili kwa makosa yanayotuhumiwa kutendwa na mwanachama wa Chadema na
kuwa makosa hayo ni ya kijinai na yalipaswa kushughulikiwa kijinai na si
kukipa adhabu chama hicho.
Pia Chadema ilisema kikao hicho kiliendeshwa na mtu asiyepaswa kuwa Mwenyekiti wa Kamati.
Taarifa ya NEC ilieleza kuwa hoja nyingine ni kitendo cha malalamiko ya
Chadema dhidi ya wakuu wa wilaya kushiriki kampeni za uchaguzi na Kamati
za Maadili kutotenda haki kwa kuwa wenyeviti wake ni makatibu tawala wa
wilaya.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC,
Kailima Ramadhani, ilifafanua kuwa tume haijapokea barua au karatasi
yoyote kutoka Chadema inayoelezea malalamiko yao.
“Ukweli ni kwamba, Chadema hawajawasilisha barua kwa tume. Hata kama
wangewasilisha barua za malalamiko yao, tume ingewaelekeza kusoma na
kuelewa Maadili ya Uchaguzi, kwa kuwa lalamiko namba mbili hadi sita
waliyoyataja kwenye vyombo vya habari yangeweza kushughulikiwa na Kamati
za Maadili ambazo Chadema kama chama chenye wagombea ni sehemu ya
wajumbe wa kamati husika,” alisema.
Kailima katika taarifa hiyo, alisema uhamishaji wa vituo umezingatia
matakwa ya Kanuni ya 21 ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura za mwaka 2008 kama zilivyorekebishwa mwaka 2014.
“Kanuni hiyo ikisomwa pamoja na kipengele cha 9.2(c) cha Kitabu cha
Maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi ya mwaka 2015, vituo vya kupigia
kura havitakiwi kuwa kwenye maeneo ya Kambi za Jeshi, Polisi, maeneo ya
kuabudia kama vile misikiti na makanisa, nyumba za viongozi au mashabiki
wa vyama vya siasa,” alifafanua katika taarifa hiyo.
Kailima pia alisema kuwa kwa kuzingatia matakwa ya kanuni na kipengele
tajwa, Januari 31, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Uchaguzi la
Kinondoni, aliitisha mkutano wa vyama vya siasa vyenye wagombea ubunge
na ajenda ilikuwa ni kuhamisha vituo vya kupigia kura.
“llifanyika hivyo kwa sababu mbalimbali zikiwamo baadhi ya vituo kuwa
kwenye maeneo ya kuabudia, kuwa jirani mno na ofisi ya chama cha siasa,
nyumba za watu binafsi, kwenye maeneo finyu,” alisema.
Alidai kuwa kikao hicho kilishirikisha wawakilishi 16 kutoka vyama 11 vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni.
“Chadema kiliwakilishwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kinondoni,
Mustapha Muro na Katibu wa Chadema wa Wilaya, Shabani Kirita,” Kailima
alieleza katika taarifa hiyo.
Kuhusu malalamiko kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alitoa uamuzi wa uonevu
dhidi ya Chadema kwenye Kamati ya Maadili, Kailima alisema uamuzi
hufanywa na Kamati ya Maadili na si Mwenyekiti wa Kamati.
“Tunaikumbusha Chadema sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi hayampi
Mamlaka Msimamizi wa Uchaguzi kutoa maamuzi kwenye Kamati ya Maadili.
Msimamizi wa Uchaguzi ni Mwenyekiti wa Kikao cha Maadili tu, na kwamba,
maamuzi hufanywa na Kamati ya Maadili na siyo Mwenyekiti wa Kamati,”
alieleza Kailima katika taarifa hiyo.
Kuhusu Chadema kuadhibiwa kwenye Kamati ya Maadili kwa makosa ya
kijinai, Kailima alisema tume imekitaka chama hicho kama hakikuridhika
na maamuzi kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye Maadili ya Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.
Kuhusu malalamiko dhidi ya wakuu wa wilaya kushiriki kampeni za
uchaguzi, Kailima alisema tume inaitaka Chadema kuwasilisha malalamiko
yake kwenye mamlaka husika kwa kuwa sheria na kanuni zimebainisha
mamlaka zinazoshughulikia masuala hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni