Mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Dodoma imemwachia mwenyekiti wa zamani
wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis
baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya kuifuta kesi iliyokuwa
ikimkabili.
Uamuzi huo umetolewa leo Februari 15, 2018 na hakimu mfawidhi wa
mahakama hiyo, Emmanuel Fovo baada kuridhia ombi la wakili wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswalo Biswalo kuiomba
mahakama kuifuta kesi hiyo.
Desemba 9, 2017, Sadifa alikamatwa na Takukuru akiwa nyumbani kwake
Mailimbili mjini hapa akituhumiwa kugawa rushwa kwa wajumbe wa mkutano
mkuu wa umoja huo.
Mbunge huyo wa Donge na mjumbe wa kamati kuu ya CCM aliyemaliza muda
wake, baada ya kukamatwa alilala mahabusu kwa siku tatu baada ya kukosa
dhamana.
Katika shtaka la kwanza, Sadifa alidaiwa aliwahonga wanachama ili
wamchague Rashid Mohamed Rashid ambaye alikuwa akiwania umakamu
mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.
Shtaka la pili, alidaiwa kuwaahidi kuwalipia gharama za usafiri
wanachama wa umoja huo kwa kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama
zawadi ili wamchague Rashid.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni