Baadhi ya wazazi wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wameonekana
kutolielewa vizuri tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli la kuzuia michango kwa shule za sekondari na
msingi.
Wazazi hao tangu tamko hilo litolewe wamekuwa wakivamia shule mbali
mbali za msingi na sekondari wakitaka kurudishiwa fedha za michango yao.
Kufuatia hali hiyo Baraza la halmashauri ya Mji wa Mbinga limeitisha
kikao cha dharura kujadili changamoto hizo na namna ya kuzitatua.
Tayari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri hiyo, Bw. Donald Msigwa
amewaagiza madiwani walijadili suala hilo kwa kina bila kupingana na
agizo la Rais Magufuli.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Mhe. Egno Kipwere
amesema kuwa agizo la Rais Magufuli halijahalalisha wazazi kurudishiwa
fedha za michango yao ya zamani na halijafuta michango ambayo wazazi
walishakubaliana kuitoa.
Rais John Magufuli alitoa tamko kupiga marufuku michango kwa shule za
msingi na sekondari nchini na kuonya kuwa mtu yeyote atakayekiuka agizo
hilo atachukuliwa hatua kali.
Soma zaidi – Rais Magufuli apiga marufuku michango mashuleni
Chanzo:ITV Tanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni