mwana wa liganga blog ni blog ya kutoa taarifa, matukio, yaliyotokea katika ulimwengu hususani katika nchi yaTanzania blog hii inasimamiwa na mwandishi wa habari kitaaluma bwana Deus Thomas liganga.lengo ni kutoa taarifa kwa umma,kwa maendeleo ya taifa na Dunia kwa ujumla kwa mawasiliano kuhusu mtangazo, habari, wasiliana nasi 0659944423,deusliganga@yahoo.com,mzeeliganga@gmail.com
Alhamisi, 11 Januari 2018
Mvua yaleta maafa Morogoro
Mvua zinazoendelea kunyesha zimebomoa nyumba kadhaa huku zingine zikizingirwa na maji Kata ya Mafisa, Kihonda Manispaa ya Morogoro.
Mvua hizo ambazo bado zinaendelea kunyesha tangu asubuhi zimeziba njia kadhaa mkoani humo na kusababisha mafuriko na kusababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kwenda shule.
Maeneo mengine ya manispaa hiyo yaliyokumbwa na mafuriko hayo ni pamoja na Kichangani, Mazimbu, Chamwino, Mbuyuni, Kilakala, Boma na sabasaba.
Aidha shughuli za biashara kwenye maduka yaliyokuwa katikati ya Manispaa hiyo zilisimama kufuatia maji kuingia kwenye maduka hayo na kusababisha uharibifu wa bidhaa mbalimbali.
Madhara mengine yaliyotokana na mvua hiyo ni kuharibika kwa miundombinu ya barabara kutokana na kujaa maji na hivyo wananchi kulazimika kuvushwa kwa kubebwa mgongoni kwa Sh1000
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wamiliki wa maduka katika eneo la Ahmadiya Baraka Mahube amesema mvua zinazonyesha kila mwaka katika eneo hilo zimekuwa zikisababisha madhara kutokana na kuziba kwa mifereji.
Hata hivyo Mahube amewarushia lawama Halmashauri ya manispaa hiyo kwa kushindwa kurekebisha miundombinu huku akisema kuwa hasara aliyopata mwaka huu ni kubwa kuliko za miaka ya nyuma.
Naye diwani wa kata ya Mafisa ambako ndiko kwenye madhara makubwa Daud Salumu amesema kuwa nyumba mbili zilizopo kwenye kata yake zimebomoka na nyingine zimezingirwa na maji.
Salumu amesema kuwa kila mwaka kata yake inakumbwa na mafuriko hivyo ipo haja kwa Halmashauri kuangalia namna ya kuepuka mafuriko hayo ya mara kwa mara.
Kata nyingine iliyoathirika na mvua hiyo ni kata ya Kihonda ambapo diwani wa kata hiyo Castory Ndulu amesema kuwa nyumba tano zimebomoka na nyingine zimezingirwa na maji.
Ndulu amesema kuwa madhara mengine yaliyotokana na mvua hiyo ni kusombwa kwa mifugo wakiwemo mbuzi, kuku na bata hata hivyo hakuna madhara yoyote ya vifo wala majeraha na kwamba tathimini inafanywa kujua madhara hayo.
Kwa upande wake mhandisi wa Tarura mkoa wa Morogoro Lusingi Mashashi amesema kwa sasa wanawashirikiana na Halmashauri ya manispaa ya Morogoro katika kuhakikisha miundombinu yote ya barabara inarekebishwa ikiwa ni pamoja na kuzibua mifereji ili kuruhusu maji yaliyosimama kupita.
Mhandisi Mashashi amesema kuwa pamoja na kwamba barabara za mijini na vijijini ziko chini ta Tarura lakini bado wanaendelea kushirikiana na kufanya kazi pamoja na Manispaa kwa kuwa kwenye barabara yapo masuala yanayowahusu Manispaa.
Kutokana na mafuriko hayo jeshi la zimamoto na uokoaji limetaja changamoto ya ukosefu wa vifaa vya uokoaji hali iliyosababisha kikosi hicho kitumie vifaa duni katika kazi ya uokoaji ikiwemo Kamba.
Kaimu kamanda wa jeshi hilo Inspekta Shomary Sala amesema katika eneo la Kihonda waliweza kumuokoa mwanafunzi ambaye amesombwa na maji wakati akivuka mto hata hivyo alieleza kuwa ujenzi holela ndio chanzo cha mafuriko katika maeneo hayo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni