Jumapili, 21 Januari 2018

MFAHAMU MWANAMUZIKI PEPE KALLE

Novemba 28,kila mwaka ndugu,  jamaa na wapenzi wa muziki wa dansi Afrika Mashariki, Kati, Magharibi na Ulimwenguni kwa ujumla, itakuwa ni siku ya majonzi tukiomboleza kifo cha mwanamuziki Pepe Kalle aliyefariki Novemba 28, 1998 kwa ugonjwa wa moyo akiwa na umri wa miaka 47.



Jitu la miraba minne Pepe Kalle  baada ya kuzaliwa Novemba 30, 1951 katika Jiji la Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo  alipewa jina Kabasele Yampanya.

Alikuwa mtunzi, mwimbaji wa muziki wa soukous na kiongozi wa bendi ya Empire Bakuba. Umbo lake kubwa lilikuwa limebeba uzito wa Kilo 136 na urefu wake ulikuwa  Sentimeta 190 ambazo ni sawa na Futi Sita na Inchi tatu.

Pepe Kale alikuwa bingwa wa miondoko ya soukous na kiongozi wa bendi ya Empire Bakuba, ambayo ilikuwa maarufu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 Sauti yake nyembamba iliyokuwa na uwezo mkubwa wa kughani, alikuwa anauwezo mkuwa wa kucheza jukwaani akitikisa umbo lake licha ya kuwa na uzito mkubwa. 

Watanzania wengi tutaendelea kumkumbuka mwanamuziki huyu hasa wakati alipokuja nchini mwetu na kutikisa majiji ya Arusha, Dar es Salam na Mbeya.

Wakati wa ujio wake hapa Tanzania, Pepe Kalle ambaye sauti yake ilikuwa nyembemba na nyororo, alifuatana  na wanamuziki akiwemo mipiga wa gita la besi Lofombo na waimbaji akina Papy Tax, Dilu Dilumona na Djo Djo Ikomo.

Rapa wake mahiri na kiongozi wa  wacheza Shoo Bileku Mpasi na  mbilikimo wawili Emoro na Jolly Bebbe walitoa burudani tosha kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam mwaka 1991. Mwaka uliofuatia wa 1992,  Emoro alifariki dunia  akiwa na bendi yake nje ya nchi  kwa safari za kikazi ya muziki.

‘Kizuri huigwa’ usemi huo ulijionyesha dhahiri baada ya msanii mmoja aliyejulikana kwa jina la Kokoriko, kuweza kuiga miondoko ya uchezaji wa Bileku Mpasi. Msanii huyo alipachikwa jina la Bileku Mpasi wa Tanzania.


Pepe wakati wa uhai wake alirekodi nyimbo zaidi wa 300 na kufyautua album 20 katika miongo miwili ya muziki wake na alijulikana kama ‘Tembo wa Afrika’.  


Historia yake katika muziki inaeleza kwamba alianza muziki rasmi katika bendi  ya Afrikan Jazz ya  Baba yake mzazi Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’  aliyemtengeneza mwanaye huyo.

Baada ya kukomaa kimuziki akatimka na kwenda kujiunga na bendi ya Lipua Lipua iliyokuwa ikimilikiwa na Kiamunagana Mateta  Wanzo la Mbonga ‘Verkeis’
Akipotua Lipua Lipua, haikuchukua kipindi kirefu  akafanywa kuwa  mwimbaji kiongozi  akishirikiana na mwimbaji wengine Nyboma Mwandido.

Safari yake katika muziki haikuishia hapo kwani mwaka 1973  Pepe kale akiwa na Dilu Dilumona na Papy Tax waliondoka katika bendi hiyo ya na  kuunda bendi yao iliyopewa jina la Empire Bakuba.
Jina la Empire Bakuba lilitokana na mashujaa wapiganaji wa makabila ya  Kongo.


Katika miaka hiyo ya 1970 Empire Bakuba na Zaiko Langa Langa ndizo zilikuwa zakitikisa jiji la Kinshasa vilivyo na kujizolea umaarufu mkubwa kwa wapenzi wa muziki wa dansi.

Vibao vya Dadou cha  Pepe Kalle na  Sango ya Mwa ya Papy Tex, iliiweka Empire Bakuba kwenye chati na ikaanzisha mtindo wa Kwasakwasa.

Mwaka 1982 yalipofanyika maadhimisho ya miaka kumi ya bendi hiyo, Empire Bakuba ilipigiwa kura na ikashinda kuwa bendi bora huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zamani Zaire.

Miaka ya 1980 Bakuba ilijizolea wapenzi na mashabiki lukuki
 ikishirikiana na Nyboma Mwandido kurekodi wimbo wa Moyibi mwaka 1988 wimbo ambao uliiongeza bendi hiyo
umaarufu katika nchi zinazozungumza lugha ya kifaransa huko Afrika ya Kati na Magharibi.

Album ya Roger Milla iliyokuwa ikimuenzi na kumsifia mchezaji wa mpira wa miguu Roger Milla ambaye alichezea timu yake ya taifa ya Cameroon akiwa na umri mkubwa kuliko wote mwaka 1990.

Miaka ya 1990 Pepe Kale alitoa album zingine za Gigant Afrique Lager than Life na Cocktail. Nyimbo zingine zilikuwa za Hidaya, Sintia,  Reovisie, Guy guy na Yanga Afrika. Nyimbo zingine zilizotikisa masikio ya wapenzi zilikuwa La- rhumba,Don’t Cry  Yaja, Zouke Zouke Nakutuna na Pon moun Paka Buoge.

 Empire Bakuba ilifanya ziara  sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya  Kongo (DRC) na hata nje ya nchi hiyo.

Kama wanamuziki wengine Pepe Kalle ailiwashirikisha wanamuziki wengine wakongwe katika tasnia ya muziki akina Simaro Lutumba na Nyoka Longo.
Bendi ya hiyo ya Empire Bakuba ilitoweka katika sura muziki baada ya kifo cha kiongozi wake Pepe Kalle.


Watanzania tutaendelea kumukumbuka Pepe Kalle ambaye alipotua Tanzania, ilitunga nyimbo kupitia lugha ya Kiswahili, za Yanga Afrika, akisifia Klabu ya  Yanga iliyokuwa ikitajwa mfadhili wa klabu hiyo  Abbas Gulamali, Hidaya, wimbo alioimba akilalamika kupoteza mkanda wake wa kiuno na  mpenzi Bupe, aliutunga alipotoka jijini la Mbeya kufanya onyesho.


Mwisho.


Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni