Jumamosi, 27 Januari 2018

Mbolea ya ruzuku yadakwa ikivushwa kwenda Malawi

Mbolea ikibebwa kuingizwa kwenye malori tayari kwa safari ya kupelekwa mikoani

ZAIDI mifuko 250 ya mbolea aina ya Urea na DAP yenye ruzuku ya serikali, imekamatwa katika Kijiji cha Ilulu wilayani Ileje mkoani Songwe ikiwa inatoroshwa kwa njia za panya kupelekwa nchini Malawi kupitia mto Songwe.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude alisema mbolea hiyo ilikamatwa juzi usiku katika operesheni iliyoendeshwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya. Mkude alibainisha kuwa mifuko hiyo ya mbolea ilikamatwa ikiwa imehifadhiwa katika ghala na nyingine ikiwa imetelekezwa katika Mto Songwe mpakani mwa Tanzania na Malawi.

Alisema katika operesheni hiyo walikamata mifuko 85 ya mbolea iliyokuwa imetelekezwa kandokando ya Mto Songwe na nyingine mifuko 173 ilikamatwa katika ghala lililopo katika nyumba ya Bryson Masebo (73) ambaye alishindwa kumtaja mpangaji wa ghala lake na mmiliki wa mbolea hiyo, hivyo anashikiliwa na polisi.

“Kilichotuwezesha kufika katika ghala hilo ni alama za miguu za ng’ombe waliokuwa wanatumika kuvuta mbolea iliyobebwa kwenye toroli kabla ya kusafirishwa kwa pikipiki, baiskeli na matololi kuelekea nchini Malawi,” alisema. Alisema katika kijiji hicho hakuna wakala wa mbolea na wakulima wanalazimika kwenda kununua Isongole.

Alisema mbali ya kukamata mbolea hiyo, pia walikamata pikipiki, baiskeli na matoroli yaliyokuwa yanatumika kuvusha mbolea hiyo, ambayo wamiliki walikimbia na kutekeleza vyombo vyao baada ya kugundua wanafuatiliwa.

Alisema kitendo kilichofanywa na watu hao ni cha uhujumu uchumi kwa kuwa mbolea hiyo ina ruzuku ya serikali na imetolewa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya wakulima kwa kuwafikishia mbolea kwa wakati, lakini watu wengine wanakwamisha juhudi za serikali kwa kuipeleka hiyo nje ya nchi.

Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Ileje, Fadhili Ishekazoba aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo ili kuzuia vitendo vya uhalifu hasa utoroshaji wa bidhaa zinazotolewa na serikali kwa maendeleo ya wananchi.

Baadhi ya wakulima wilayani Ileje wamelaani kitendo hicho cha kupeleka mbolea nje ya nchini wakati wakulima wakilalamikia ukosefu wa mbolea huku lawama zikielekezwa kwa serikali kuwa haisambazi mbolea ya kutosha.

Owadi Msongole alisema wakulima wamekuwa wakikosa mbolea kutoka kwa mawakala wakiamini kuwa serikali haijasambaza mbolea kumbe kuna watu wachache wanaotaka kujinufaisha kwa kupeleka mbolea nchini Malawi.

“Tukienda kununua mbolea Isongole kwa mawakala tunaambiwa hamna, kumbe inasafirishwa kwenda Malawi kwa njia za panya, wakipatikana hawa watu wachukuliwe hatua kali kwa sababu wanatugandamiza wakulima wadogo,” alisema Msongole.

Taarifa za awali zilidai mbolea hiyo ilikuwa igawiwe bure kwa wakulima na uongozi wa wilaya, lakini kutokamilika kwa taratibu za kisheria kumesababisha hilo kusitishwa kwa muda hadi hapo taratibu hizo zitakapokamilika.

Juni mwaka jana, Mkuu wa Wilaya ya Ileje aliteketeza madaraja yaliyounganishwa kwa njia za panya yaliyokuwa yanatumika kusafirisha bidhaa za magendo likiwemo daraja lililopo katika Kijiji cha Ilulu ambalo lipo umbali wa kilometa tano tu kutoka kilipo kivuko halali cha kupitisha watu na magari wanaoingia na kutoka nchini Malawi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni