mwana wa liganga blog ni blog ya kutoa taarifa, matukio, yaliyotokea katika ulimwengu hususani katika nchi yaTanzania blog hii inasimamiwa na mwandishi wa habari kitaaluma bwana Deus Thomas liganga.lengo ni kutoa taarifa kwa umma,kwa maendeleo ya taifa na Dunia kwa ujumla kwa mawasiliano kuhusu mtangazo, habari, wasiliana nasi 0659944423,deusliganga@yahoo.com,mzeeliganga@gmail.com
Ijumaa, 26 Januari 2018
MAHAKAMANI: Makosa matano yanayomkabili Tido Mhando
liyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia hasara shirika hilo ya Sh.Mil 887.
Mhando amesomewa makosa yake na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leornad Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
Swai amedai Tido anakabiliwa na makosa matano ya uhujumu uchumi wa kuisababishia mamlaka hasara, lakini pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ametoa kibali kesi hiyo isikilizwe Mahakamani hapo.
Kosa la kwanza la matumizi mabaya ya madaraka, inadaiwa alilitenda June 16,2008 akiwa Dubai kama mtumishi wa TBC alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya uendeshaji wa vipindi kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BVI) bila ya kutangaza zabuni na kuisababishia channel hiyo kunufaika.
Pia anadaiwa June 20,2008 akiwa huko Dubai kama Mkurugenzi Mkuu wa TBC alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya kiutendaji kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni.
Pia Tido anadaiwa alitumia madaraka yake vibaya kati ya August 11,2008 na September 2008 akiwa Dubai kama mwajiriwa wa TBC kwa makusudi alisaini mikataba ya kununua, kusambaza na kusimika vifaa vya kurushia matangazo kati ya TBC na Channel 2 bila kutangaza zabuni ya manunuzi na kuisababishia channel hiyo kupata faida.
Kosa jingine la matumizi mabaya ya madaraka, alilitenda November 16, 2008 akiwa Dubai kwa makusudi alisaini mikataba ya uendeshaji wa miundombinu ya DTT kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni ambapo alisababisha channeli hiyo kupata faida.
Katika kosa la mwisho, inadaiwa aliisababishia mamlaka hasara ya Sh.Milioni 887,112,219.19.
Inadaiwa kati ya June 16 na November 16,2008 akiwa falme za Kiarabu, kama mwajiriwa wa TBC kwa cheo cha Mkurugenzi Mkuu kwa mamlaka yake alilisababishia shirika la TBC hasara ya Sh.Mil 887.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Tido aliyakana ambapo Wakili Swai alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Tido kupitia Wakili wake Ramadhan Maleta aliiomba Mahakama hiyo impatie dhamana.
Kutokana na maombi ya dhamana, Hakimu Nongwa alitoa masharti ya kumtaka Tido atoe fedha taslimu Sh.Mil 444 ama Mali isiyoamishika ya thamani hiyo.
Pia awe na wadhamini wawili ambapo kila mmoja asaini bondi ya Sh.milioni 500, pia hatakiwi kutoka nje ya nchi bila kibali cha mahakama.
Baada ya kupewa masharti hayo, Tido aliweza kuyatimiza kwa kutoa hati ya mali yenye thamani ya Sh.Mil 444 pamoja na kuwa na wadhamini. Kesi imeahirishwa hadi February 23,2018.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni