
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro
amekanusha uvumi unaonea kwenye mitandao ya kijamii kwamba ana mpango wa
kukihama chama hicho na kuhamia Chama tawala cha CCM.
Kupitia
taarifa yake kwa umma aliyoitoa jana Disemba 6,2017, Mtatiro pia hana
mpango wa kugombea jimbo la Kinondoni lililo achwa wazi kufuatia
aliyekuwa Mbunge wake kupitia CUF, Maulid Mtulia kujiuzulu na kujiunga
na CCM.
“Ndugu zangu, nimeona propaganda nyingi kwenye mitandao juu ya mimi kuhamia CCM au kuwa na mipango ya kuhamia CCM.
"Nataka
niwahakikishie watanzania kuwa SIJAPANGA mipango hiyo na sina nia hiyo.
Na naomba niwajulishe kuwa mtu akiwa anahamia CCM, hamuwezi kuwa na
tetesi, na mimi sina kawaida ya kufanya maamuzi ghafla na kwa
kujificha.
"Ningelikuwa
na nia ya kuhamia CCM ningewataarifu hapa hadharani, miezi kadhaa kabla
ya kufanya hivyo, walau jambo moja ambalo Mungu alinijalia ni kutokuwa
mwoga na mnafiki na alinipa uwezo mkubwa wa kufanya jambo naloliamini,”
alisema na kuongeza.
“Pili,
nimepokea meseji nyingi sana zikiniomba nigombee ubunge jimbo la
Kinondoni baada ya Mbunge wa (CUF – Lipumba), Ndugu yetu Maulid Mtulia
kuhamia CCM. Nataka niweke msimamo wangu mapema, kwamba sina na sikuwahi
kuwa na ndoto za kugombea ubunge wa jimbo la Kinondoni,
Masuala
ya kugombea ubunge kwenye majimbo ni masuala mapana, yanahitaji
maandalizi, ukaribu wako na wapiga kura na historia yako na jimbo hilo.
Kwa kiasi kikubwa hakuna kigezo hata kimoja kati ya hivyo ambacho
nimekikaribia, kwa hiyo sitoweza kugombea kama nilivyoona baadhi ya
fikra za watu mitandaoni.”
Mtatiro
amewahakikisha wanachama wa CUF kwamba anaendelea na majukumu yake ya
Kamati ya Uongozi CUF, pamoja na kushirikiana na kila mtanzania kwa njia
mbalimbali katika kuijenga nchi.
“Na
kupitia michango yangu hiyo naendelea kuijenga Tanzania na hata kuunga
mkono juhudi chanya za Rais wetu kuijenga Tanzania huku zile juhudi hasi
za Rais huyo huyo hasa kwenye eneo la Demokrasia, Utawala Bora na
Uchumi, nikizikemea kila siku.
"Mwisho,
wapo wendawazimu wanachekelea, wanafurahia na ama kutamani vyama vya
upinzani vife. Ukiona elimu ni ghali, hebu jaribu ujinga,” amesema.
Hata
hivyo, Mtatiro amesema anaendelea kuwaheshimu wanaohamia CCM, kwa
uhuru, utashi na mapenzi yao au kwa kununuliwa, kutokana kwamba sio wa
kwanza wala hawatakuwa wa mwisho kufanya hivyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni